LOME, TOGO
MAELFU ya waandamanaji walimiminika katika barabara za mji mkuu wa Togo, Lome hapo juzi, ikiwa ni mara ya tatu ndani ya wiki moja wakimtaka Rais Faure Gnassingbe aondoke madarakani.
Mwezi uliopita, Rais huyo aliyepo madarakani kwa zaidi ya miaka 15 aliahidi serikali yake itafanya mazungumzo na vyama vya upinzani, lakini hakuna hatua zilizopigwa kufikia hilo.
Wapatanishi wa kanda ya magharibi mwa Afrika wakiwemo Rais wa Ghana Nana Akufo Addo na wa Guinea Alpha Conde wamekuwa wakijaribu kuanzisha mazungumzo kati ya pande hizo mbili.
Maandamano ambayo yameshuhudiwa Togo tangu Agosti yameandaliwa na muungano wa vyama 14 vya upinzani.
Vyama hivyo pamoja na mambo mengine vinataka ukomo wa mihula ya Rais kuwa miwili, na Rais Gnassingbe aliyeingia madarakani mwakla 2005 akimrithi baba yake Gnassingbe Eyadema aliyefariki dunia baada ya kuiongoza Togo kwa miaka 38, azuiwe kugombea urais katika uchaguzi wa mwaka 2020.