MONROVIA- LIBELIA
HASIRA zimetawala kwa wananchi wa Liberia ambao wamepanga kuandamana kutaka majibu juu ya upotevu wa mamilioni ya dola za serikali.
Mwaka jana ilibainika dola za Liberia bilioni 15.5 (ambazo ni sawa na dola za Marekani milioni 104 au Euro milioni 82) za sarafu mpya zilizozua utata zilitoweka katika bandari ya nchi hiyo.
Zaidi kulikuwa na ufujaji wa dola za Marekani milioni 25 ambazo ziliingizwa kwenye uchumi wa nchi hiyo mwaka jana.
NINI KINATOKEA
Septemba, 2018 vyombo vya habari vya nchi hiyo viliripoti kuwa kontena lililokuwa limejaa noti mpya za dola za Liberia zilizochapwa nchini Sweden lilitoweka wakati likiingia bandarini kati ya mwaka 2016 na 2017.
Benki Kuu ya Liberia ilipinga madai hayo ikieleza kuwa fedha hizo zilikuwa zimehifadhiwa.
Miezi michache kabla ya taarifa hizo, Rais George Weah, ambaye aliingia madarakani Januari 2018, alitangaza kuwa Benki Kuu ya nchi hiyo itaingiza dola milioni 25 kwenye mzunguko wa uchumi ili kuondoa dola ya zamani ya Liberia.
Dola ya Liberia imekuwa ikipoteza thamani tangu Julai 2017 hali iliyochangia gharama kubwa na mfumuko wa bei.
Kwa sababu hiyo, kila siku bidhaa zimeendelea kupanda bei kwa mtu wa kawaida nchini humo.
Zoezi la fagia fagia la Rais Weah ambalo lilifanyika kati ya Julai na Oktoba mwaka jana lililenga kupunguza kiasi cha fedha za ndani katika uchumi ili kupunguza kushuka kwa thamani zaidi.
Hata hivyo bado kuna maswali mengi ambayo hayajajibiwa kuhusiana na zoezi hilo na taarifa za kutoweka kwa makontena yenye dola.
Ripoti mbili za uchunguzi juu ya suala hilo zilizofanywa na Timu ya Rais ya Uchunguzi (PIT) na nyingine ya ushauri inayojulikana kama Kroll zilibaini dosari kubwa jinsi sera ya serikali ilivyotekelezwa katika kila kesi.
Si PIT au Kroll hazikuweza kujibu juu ya dola mpya iliyochapwa ya Liberia au zile za Marekani zilizoongezwa.
Kwa mujibu wa Kroll, dola bilioni 5 za Liberia kati ya Jumla ya dola bilioni 15.5 zilichapishwa na kusambazwa kulingana na sheria ya Liberia.
Ilibainika kuwa Benki Kuu haikupata kibali cha kisheria kuruhusu kiasi kilichobaki cha fedha, lakini iliingia mkataba mwingine wa kuruhusu kuchapa na kusambaza fedha nchini Liberia.
Kroll pia ilibaini kuwa ziada ya dola za Liberia bilioni 2.6 zilichapishwa kwa kuongeza kile ambacho hakikuwekwa wazi awali. Ripoti ya PIT nayo imeeleza hivyo hivyo.
Bado kuna taarifa chache kuhusu kiasi hicho cha ziada na Gavana wa zamani wa Benki Kuu, Milton Weeks, na naibu wake Charles Sirleaf walikamatwa kwa mapendekezo ya PIT.
Sirleaf, ambaye ni mtoto wa kiume wa rais wa zamani wa nchi hiyo, Ellen Johnson-Sirleaf na Weeks wanatarajia kufikishwa mahakamani wiki zijazo.
Rais huyo wa zamani Sirleaf amesema mwanaye na Weeks wamepigwa marufuku kutoka nje ya nchi hiyo.
Waandamanaji wanaamini kuwa baada ya matokeo hayo uchunguzi unaofuata utamlazimisha rais wanchi hiyo kuchukua hatua.