28.7 C
Dar es Salaam
Friday, May 24, 2024

Contact us: [email protected]

VYUO VIJIKITE KUANDAA WAHITIMU SOKO LA AJIRA

Na JUDITH MHINA – MAELEZO

HIVI karibuni Sekretarieti ya Ajira kupitia kwa Ofisa Mawasiliano na Msemaji wake, Riziki Abraham, alipokutana na waandishi wa habari, alisema Serikali imetoa ajira 52,000, lakini waombaji wengi wa ajira walishindwa kuitwa kwenye usaili baada ya kushindwa kukidhi vigezo vilivyoainishwa kwenye mchakato wa kuomba ajira husika.

Wakati umefika sasa wa kukubali kuwa changamoto hii ipo, ni kubwa na inahitaji mkakati wa dhati ili kuweza kuinua uelewa na ufahamu wa jinsi ya kuwawezesha wahitimu wa vyuo mbalimbali nje na ndani ya nchi kuweza kuomba ajira.

Watanzania tuichukue changamoto hii kuwa fursa kwa vyuo vyetu mbalimbali kuona uwezekano wa kuweka japo kwa muda mfupi kutoa mafunzo ya kuomba ajira, unatakiwa kufanya nini unapoomba ajira na kwa kiasi gani unatakiwa kuwa makini katika kufuata masharti yaliyowekwa katika kuomba ajira husika.

Hii ikiwa ni pamoja na kujua jinsi ya kuandika wasifu wake binafsi kama kielelezo cha kuthibitisha yeye ni nani na amepitia katika shule na vyuo gani mpaka hapo alipo. Aidha, ana uzoefu wa taaluma gani kutokana na shule na vyuo alivyosoma, ikiwamo kufanya kazi za majaribio katika maeneo mbalimbali wakati akiwa mwanafunzi au mwanachuo.

Vilevile, shule zetu za sekondari na za msingi ni muhimu kuanza mazoezi ya kuandika barua ya maombi ya kazi tangu elimu ya awali, ili unapofika elimu ya juu kama Vyuo inamrahisishia Mhadhiri kuwapitisha kama kuwakumbusha umuhimu wa kuandika barua ya maombi ya kazi kwa makini.

Ukilinganisha nafasi zilizotolewa na serikali 52,000 walioomba 56,815, walioitwa kwenye usaili, 29,674 na kuacha nafasi 22,326 ambao nao walitakiwa waitwe kwenye usaili kushindikana.

Aidha, sababu za msingi zilizotolewa na Sekretarieti ya Tume ya ajira za kutochaguliwa kwa wanavyuo hao ni kutofuata masharti yaliyowekwa kwenye taratibu za kuomba ajira.

Riziki amesema jumla ya maombi yaliyopokelewa kupitia njia ya uwasilishaji wa kielektroniki ni 56,815 na baada ya kufanyiwa kazi waliokidhi vigezo kwa mujibu wa sifa zilizokuwa zimeainishwa kwenye matangazo ya ajira husika, waombaji 29,674 waliitwa kwa ajili ya usaili.

Sababu nyingine zilizoainishwa ni baadhi ya waombaji ajira kutofahamu namna ya kuandika barua ya maombi ya kazi, kutothibitisha nyaraka zao, hususan kwa wale waliosoma nje ya nchi, kutozingatia masharti kwa ujumla, ikiwepo kuwasilisha nyaraka pungufu, kudanganya kutoa wasifu usio wa kweli.

Hata hivyo, baadhi ya waombaji wamewasilisha picha katika mfumo tofauti na bila kujali mandhari na mavazi waliyovaa, kupakia vyeti visivyohitajika katika maombi kama vile transcript, result slip na kuandika wadhamini wachache ambao si wahusika.

Riziki amesema: “Mpaka sasa Sekretarieti ya Ajira imepata vibali vya kazi 239, kati ya hivyo baadhi vimefanyiwa mchakato, ikiwa ni pamoja na Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Chuo cha Sayansi na Tiba Muhimbili (MUHAS) na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)”.

Vijana tuchangamkie ajira zinazotolewa, kwa kuwa kumekuwa na tabia ya kulaumu serikali kuwa haitoi ajira, lakini tuzingatie masharti yote pamoja na vigezo vilivyoainishwa ili tuweze kupata fursa hizo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles