27.5 C
Dar es Salaam
Sunday, December 3, 2023

Contact us: [email protected]

BODI YA KOROSHO YATAKIWA KUFANYA TATHMINI

Na Mwandishi Wetu -DODOMA

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa, amezitaka Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi pamoja na Bodi ya Korosho Tanzania zifanye tathmini ya maandalizi ya msimu ujao kwa wakati na zimpatie taarifa mara moja.

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo juzi wakati akizungumza na wadau wa zao la korosho kwenye kikao alichokiitisha ofisini kwake mjini Dodoma kujadili mwenendo wa zao la korosho na ununuzi wa pembejeo.

“Lipo tatizo la tathmini ya maandalizi ya msimu kutofanyika kwa wakati na kusababisha matatizo kutotatuliwa kwa wakati. Bodi na Wizara zitoe tathmini ya maandalizi ya msimu ujao kuhusu vyama vya ushirika vilivyojipanga, upatikanaji wa vifaa kama magunia na nyuzi, maghala, masoko, mizani, minada, malipo na mfumo wake,” alisema.

Kutokana na hali hiyo, aliitaka Wizara ya Kilimo pamoja na Bodi ya Korosho zitoe tathmini ya maandalizi ya msimu ujao katika maeneo ya mashamba, miche, pembejeo na viatilifu.

Alisema tangu Serikali iamue kusimamia mazao makuu matano ya pamba, chai, kahawa, korosho na tumbaku hajapata muda wa kukaa na kuongea na wadau wote.

“Serikali imeamua kufuatilia usimamizi wa mashamba, kusimamia upatikanaji wa mbegu, miche na pembejeo; kufuatilia uvunaji na mfumo wa masoko ya korosho na pia kufuatilia mfumo wa ushirika katika baadhi ya mazao,” alisema.

Alisema hivi sasa zao la korosho linalimwa katika wilaya 50 kwenye mikoa 11 ya Dodoma, Iringa, Lindi, Mbeya, Morogoro na Mtwara. Mingine ni Njombe, Pwani, Ruvuma, Singida na Tanga.

“Katika msimu wa mwaka 2016/2017, zao la korosho lilikuwa ni moja kati ya mazao ya kibiashara yenye tija na faida nyingi kwa kuliingizia Taifa fedha za kigeni kiasi cha Dola za Marekani milioni 346.6.

“Katika msimu wa mwaka 2017/2018, watendaji hawana budi kujipanga vizuri ili zao hilo liendelee kuliingizia Taifa dola nyingi zaidi kwa kuwa Serikali imetoa viatilifu bure,” alisema.

Alisema Agosti mwaka huu, alipofanya ziara mkoani Tabora, alielezwa kwamba Wilaya ya Uyui na Tabora Manispaa zimeanza kulima zao hili kama zao mbadala ili kuinua uchumi wa wananchi wake.

“Tabora itakuwa mkoa wa 12, kwa hiyo Wizara ya Kilimo itembelee maeneo haya na kuona inawezaje kuwasaidia, ikaangalie uzalishaji ukoje kwani mti unaweza kukubali kuota pale Tabora, lakini usizae kwa wingi kama ilivyo kwa mikoa mingine,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
579,000SubscribersSubscribe

Latest Articles