KAMPUNI ya Mawasiliano ya Vodacom Tanzania, imesema kuwa itaendelea kushirikiana na Serikali kwa kuunga mkono jitihada za Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani.
Akizungumza jana katika kilele cha wiki ya Usalama Barabarani, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mawasiliano na Uhusiano wa Vodacom Tanzania, Rosalynn Mworia, alisema Vodacom itaendelea kuunga mkono jitihada za Serikali za kutokomeza matukio ya ajali nchini.
“Kama kampuni ya mawasiliano, tumekuwa tukiendesha kampeni inayojulikana kama ‘Wait to Send’ ambayo imekuwa ikihamasisha madereva kutotumia simu za mkononi wakati wanaendesha vyombo vya moto, ikiwamo kutoendesha vyombo vya moto wakiwa wametumia vinywaji vyenye kilevi,” alisema Mworia.
Awali akizungumza katika kilele hicho, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Yussuf Masauni, alisema bado kumekuwa na matukio mengi ya ajali za barabarani nchini zinasosababisha vifo vya wananchi wengi, hivyo kuna haja ya kuongeza nguvu katika kampeni za usalama barabarani ili kupunguza tatizo hilo.
Masauni alitumia nafasi hiyo kuyapongeza makampuni ya kibiashara na mashirika yasiyo ya kiserikali yanayosaidiana na Serikali kupitia Jeshi la Polisi kufadhili na kuendesha kampeni za usalama barabarani.
“ Pamoja na kuwepo na matukio mengi ya ajali, Serikali inafarijika kuona yapo makampuni ya kibiashara na mashirika yasiyo ya kiserikali ambayo yanashirikiana kwa karibu na Serikali kupitia Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani kuendesha kampeni za usalama barabarani kwa jamii ikiwamo kufadhili shughuli za uhamasishaji usalama katika Wiki hii ya Nenda kwa Usalama Barabarani,” alisema.