31.9 C
Dar es Salaam
Monday, December 5, 2022

Contact us: [email protected]

Profesa Muhongo anastahili kuwa mfano  

1NA BENJAMIN MASESE, MWANZA

NAWEZA kusema elimu, busara na nia ya dhati ya Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, ndiyo inayomtofautisha na mawaziri  pamoja na wabunge wengine wa chama tawala sambamba na upinzani.

Wapo baadhi ya wabunge, wananchi na hata viongozi wengine wa Serikali wamekuwa wakishindwa kumwelewa Profesa Muhongo, tabia yake na mwenendo wa uongozi ambapo wengi huishia kusema ana kiburi na dharau.

Profesa Muhongo ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini (CCM), amekuwa  ni miongoni mwa mawaziri ambao wizara zao zinakumbwa na kashfa mbalimbali na kufikia kujiuzulu katika awamu ya nne ya utawala wa Rais mstaafu Jakaya Kikwete, lakini kutokana na umuhimu wake, Rais Dk. John Magufuli, ameendelea kumwamini na kumrejesha katika nafasi yake.

Hivi karibuni Profesa Muhongo akiwa mkoani Mara, alifanya jambo la uungwana la kuamua kuweka pembeni itikadi za siasa na kuwaunganisha wabunge wote wa Mkoa wa Mara na kuwapatia msaada wa vitabu 25, 000 vya sayansi na hisabati kwa ajili ya shule za sekondari vyenye thamani ya Sh milioni 500.

Kwa tabia yake ya uwazi, Profesa Muhongo aliamua kumwomba Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Dk. Vicent Nnano na  viongozi wengine ili kushuhudia makabidhiano hayo.

Kwa mujibu wa Profesa Muhongo, lengo la kukabidhi vitabu hivyo kwa wabunge hao ni kuhakikisha elimu hususan katika masomo ya sayansi inaboreshwa ili kuwa na wanasayansi wengi zaidi.

Profesa Muhongo hakuishia hapo, aliwaahidi wabunge wote wa mkoa huo kwamba kabla ya Desemba 25, mwaka huu atatoa vitabu vingine katika shule ambazo zitakuwa zimejenga maktaba.

Ni wabunge wachache wanaoweza kupata msaada kutoka kwa marafiki wake kwa ajili ya kusaidia shule zilizo kwenye jimbo lake kisha kuwagawia  wabunge wenzake bila kujali itikadi za vyama.

Profesa Muhongo alidai kwamba lengo lake ni kuona  Mkoa wa  Mara unarudisha hadhi yake ya ufaulu shuleni, hasa katika masomo ya sayansi kama ilivyokuwa huko zamani.

Hakika Profesa Muhongo ameonyesha nia njema kwa wabunge wa Mkoa wa Mara, ni vema wawakilishi hao wa wananchi wakawa na ajenda moja ya maendeleo kwa wananchi  ili kuwa mfano kwa mikoa mingine.

Profesa Muhongo alikuwa na uwezo wa kusambaza vitabu hivyo katika jimbo lake na kuondoa kabisa uhaba wa  vitabu, lakini kutokana na mahaba ya maendeleo ya mkoa huo, akaamua kuwagawia wenzao.

Sote tulishuhudia jinsi wabunge wa Mkoa wa Mara walivyoonyesha kushikamana na kumpongeza Profesa Muhongo kwa uamuzi wake wa kupunguza adha hiyo ambapo Katibu wa Umoja wa Wabunge wa Mkoa wa Mara ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Serengeti (Chadema), Marwa Ryoba, alisema  Muhongo  ameonyesha upendo na uzalendo.

Uungwana  wa Profesa Muhongo si kwamba upo kwa wabunge wa Mara pekee la hasha, akiwa mkoani Kagera ameagiza Bodi ya Wakurugenzi  kwa kushirikiana na Menejimenti ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kuhakikisha inaanza mchakato wa kuwapa mikataba ya ajira  vibarua na watu wengine waliotumikia shirika hilo kwa muda mrefu bila kuwapo upendeleo.

Pia  katika  kuhakikisha anajali wananchi, Profesa Muhongo ameagiza Tanesco kufungua ofisi katika maeneo ya vijijini  kwa lengo la kuepusha usumbufu wa wateja kusafiri umbali mrefu kutafuta huduma kwenye ofisi za shirika hilo.

Yote hayo ni mambo mazuri ya Waziri Muhongo  ambaye anapaswa kuungwa mkono na kila mtu anayependa maendeleo bila kujali itikadi za siasa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
205,586FollowersFollow
558,000SubscribersSubscribe

Latest Articles