28.2 C
Dar es Salaam
Monday, February 6, 2023

Contact us: [email protected]

Meya Dar atembelea shule alizosoma Tarime

isaya-mwitaNa MWANDISHI WETU, TARIME

MEYA wa Jiji la Dar es Salaam, Isaya Mwita, ametembelea kijijini kwao pamoja na shule alizosoma.

Mwita alifanya ziara hiyo wiki iliyopita akianzia kijijini kwao Bulembo, Wilaya ya Tarime mkoani Mara, kisha akatembelea Shule ya Msingi Kemange pamoja na Shule ya Sekondari Tarime.

Katika ziara hiyo, Mwita alilenga kujua changamoto zinazoyakabili maeneo hayo na kuangalia namna ya kuyatatua kwa kushirikiana na wahusika.

Akiwa katika Shule ya Sekondari Tarime, Meya Mwita alisema anaikumbuka shule hiyo kwa kuwa ndiko alikopatia elimu yake ya sekondari.

“Nimesoma hapa kwa shida sana lakini hii ndiyo shule iliyonifikisha hapa nilipo. Kwa hiyo nisipotambua mchango wa walimu wa shule hii, nitakuwa sina fadhila. Kwa kuwa natambua umuhimu huo katika maisha yangu, ndiyo maana leo nipo hapa kuomba ushirikiano wa kutatua kero zinazowakabili.

“Changamoto mlizozieleza hapa siwezi kuzitolea majibu kwa sasa ila ninazichukua nikaangalie ni namna gani ninavyoweza kusaidia.

“Kuhusu hilo suala la michepuo ya elimu, nitawasiliana na waziri wa elimu ili tuangalie namna ya kurudisha michepuo iliyoondolewa ili iweze kurudishwa,” alisema.

Awali, Mkuu wa Shule hiyo, John Marwa, alimwambia meya huyo kwamba shule hiyo inakabiliwa na uhaba wa vitabu vya masomo ya sayansi na masomo mengine.

“Pia tunakabiliwa na uhaba wa walimu wa masomo ya sayansi na pia idadi ya wanafunzi ni kubwa ikilinganishwa na idadi ya walimu tulionao.

“Yaani hapa walimu wa masomo ya sanaa ni wengi ila wanafunzi ni wachache, lakini walimu wa masomo ya sayansi ni tatizo.

“Kwa hiyo tunaomba utusaidie kufikisha kero hii kwa wahusika ili waangalie namna ya kutusaidia,” alisema Mwalimu Marwa.

Pamoja na kutembelea maeneo hayo, Meya Mwita alitembelea pia wafungwa walioko katika Gereza la Wilaya ya Tarime na kutoa msaada wa sabuni za kufulia.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,471FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles