23.3 C
Dar es Salaam
Thursday, June 13, 2024

Contact us: [email protected]

VIWANGO VIKUBWA VYA RIBA HUUA BIASHARA NDOGO NDOGO

Gavana wa Benki Prof Benno Ndulu
Gavana wa Benki Prof Benno Ndulu

Na Joseph Lino,

VIWANGO vikubwa vya riba vinaathiri biashara za kati na ndogo ndogo katika nchi za Afrika Mashariki.

Tafiti zinaonesha upatikanaji wa mikopo ya riba nafuu unaweza kuchochea ukuaji wa biashara hizi ambazo ni  tegemeo kubwa kwa nchi hizi.

Biashara za kati na ndogo ndogo Afrika Mashariki zinapaswa kuangalia njia za kuongeza ufanisi wao na kuboresha usimamizi wa madeni, pia kuona hatari ya viwango vya juu vya riba namna vinavyoathiri biashara zao.

Mkurugenzi wa Sage Afrika Mashariki, Billy Owino, anasema kampuni yake inayoshughulika na mahesabu, mifumo ya mishahara na malipo, anaelezea kuwa wafanyabiashara wadogo wanaojenga biashara huwa na shinikizo la kupanda kwa viwango vya riba kuliko wenye biashara kubwa.

“Wenye Biashara kubwa na watunga sera za Serikali wanapaswa kuangalia namna ya kusaidia biashara ndogo ndogo, kusimamia changamoto wanazokabiliana nazo kutokana na viwango vya juu vya riba,” anasema Owino.

Alibainisha kuwa biashara za kati na ndogo ni nguzo ya  uchumi katika Kanda ya Afrika Mashariki kwa kuzalisha mapato makubwa, kodi na ajira.

Nchini Kenya biashara za kati na ndogo zinakadiriwa kuchangia asilimia 80 ya nafasi za ajira.

Sekta ya biashara za kati na ndogo ndogo huwa inajenga ukuaji wa uchumi na mapato ya kodi, ndio maana nchi za kanda hii huweka kipaumbele biashara kama hizi.

Sarafu ya Afrika Mashariki

Ingawa viwango vya riba vimeanza kupungua kwa kiasi fulani Afrika Mashariki, lakini bado viwango ni vikubwa kwa nchi kama Uganda na Kenya ambapo Benki Kuu ilifanya hivyo miaka miwili iliyopita ili kulinda sarafu isishuke, lakini hiki kimekuwa kikwazo cha ukuaji wa biashara ndogo ndogo kwa mujibu wa Owino.

Nchini Tanzania viwango viko juu sana na Serikali inaomba mabenki yashushe lakini hayasikii kutokana na ukata ulioshamiri, baada ya kutoa fedha zake kwenye mabenki ya biashara.

Owino anaelezea kuwa kwa upande mwingine, riba kubwa inamaanisha kuwa wateja wengi wana kiasi kidogo cha fedha kwa ajili ya kutumia, hasa katika bidhaa za hali ya juu.

Aidha, inamaanisha kuwa  wenye biashara ndogo ndogo wanalipa zaidi kwenye huduma, mikopo ya gari, mikopo ya kibiashara na madeni.

Mkurugenzi huyo anafafanua zaidi kuwa tofauti na biashara kubwa, biashara ndogo ndogo zinahitaji upatikanaji wa mikopo kwa ajili ya ukuaji wa biashara au kuziba mapengo ya hali ngumu ya biashara kwa sababu hawana akiba kubwa ya fedha.

Owino anasema ulipaji wa viwango vya kodi vya hali ya juu kunaweza kuathiri uendelevu wa biashara kwa wale ambao tayari hali ni ngumu kibiashara na wapo hatarini kufunga au kufilisika.

Kuingilia kati kwa Serikali 

Nchi za Afrika Mashariki zimechukua hatua  za kukabiliana na madhara ya viwango vikubwa vya riba juu ya walaji na wafanyabiashara ndogo ndogo.

Kwa mfano, Kenya ilianzisha sheria ya kukabiliana na viwango vya riba benki kwa asilimia 4 juu ya viwango vya Benki Kuu.

Ingawa hii imesaidia kuzuia viwango vya malipo ya riba kwenye benki kutozwa kwa wateja wao, lakini kuna hatari isiyotarajiwa kama benki kutoza ada nyingine kwa ajili ya kufidia mapato yanayopotea kwenye riba.

Wazo jingine na uwezo wa kufanya tofauti ni Serikali kusaidia kufadhili biashara ndogo ndogo kwa njia ya kiasi cha fedha kidogo.

“Kwa kusaidia ukuaji wa biashara kupitia mikopo yenye viwango vya riba vya chini, Serikali inaweza kusaidia kutengeneza ajira na mapato ya kodi kwa ajili ya wakati ujao.

“Benki za maendeleo ambazo zinaendeshwa na Serikali na  taasisi za kimataifa kama vile International Finance Corporation, wanaleta mabadiliko tofauti, lakini fursa ya kupata fedha bado ni ndogo miongoni mwa biashara ndogo za Afrika Mashariki,” anasema Owino.

Punguza gharama:

Angalia njia za kupunguza upotevu na uzembe wa fedha katika biashara ili uweze kulipia madeni kwa kasi au kuepuka kuchukua mkopo. “Imarisha mfumo wa mahesabu ambao unaweza kukusaidia kuelewa zaidi matumizi yako ili uweze kutafuta njia ya kupunguza gharama.

Vinginevyo, kaa chini na wauzaji wako wakuu na kujaribu kujadili masuala ya mikopo vizuri ambayo kama unaweza ukapata kwa siku 30 kulipa kwa hisa bila riba, hiyo ni vyema kuliko kutumia hawala (overdraft) ambayo unaweza kupata fedha bila kuwa na pesa kwenye benki.

Ni vizuri basi wakopeshaji wako wajue mara moja kuwa unahangaika kufanya malipo yako.

Hii itakupa nafasi ya kujadili suala upya badala ya kuingia katika madeni makubwa na adhabu ya riba au kuharibu uhusiano wako na benki au wauzaji.

Kumbuka vipaumbele vyako ni kulipa madeni yote yenye viwango vikubwa zaidi kwanza na kuwa makini katika usimamizi wa wadaiwa wako mwenyewe, kwa kuhakikisha unadhibiti mikopo yako na mchakato wa ukusanyaji.

Benki Kuu yaingilia kati

“Benki Kuu ya Tanzania imesema kupungua kwa hatari  za mikopo (credit risk), itawezesha mabenki na vyombo vingine vya fedha kukopesha  zaidi  kwa watu binafsi na kuacha kutegemea usalama kutoka soko la taasisi za umma,” anasema Gavana  wa BoT,  Prof. Benno Ndulu.

Akizungumza kwenye hafla ya 18 ya Vyombo vya Fedha jijini Arusha wiki iliyopita, anasema kazi ya vyombo vya fedha  ni kuwezesha sekta binafsi kuchuma mali kwa kutumia uwezo wa ushindani uliopo.

“Ikichangiwa na kuwepo na taarifa sahihi za wakopaji gharama ya mikopo,  inaweza kupunguzwa na hivyo kuwezesha watu wengi kukopa kwa riba nafuu. Vyombo vya fedha ni vya msingi katika kutoa mikopo katika kuunga mkono maendeleo ya viwanda na kilimo  ambavyo ni  msingi wa kukuza biashara ya nje,” alisisitiza Gavana Ndulu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles