29.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

NCHI MASKINI ZINAPOKUWA WAFADHILI WA NCHI TAJIRI

Profesa Prosper Ngowi
Profesa Prosper Ngowi

Na Justin Damian aliyekuwa Norway,

WAKATI nchi nyingi zinazoendelea zikihangaika usiku na mchana kupata fedha kwa ajili ya utekelezaji wa bajeti zao, mabilioni ya dola yamekuwa yakipotea kutokana na suala la uha mishaji haramu wa fedha.

Uhamishaji huu wa fedha kutoka nchi moja kwenda nchi nyingine, umekuwa ukifanywa na watu pamoja na makampuni makubwa ambayo hutumia mbinu mbali mbali kutekeleza nia yao ovu na kusaidiwa na usiri uliopo katika utaratibu wa masuala ya kifedha ulimwenguni.

Kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa mwezi Desemba mwaka 2015 na asasi binafsi inayojihusisha na utafiti wa masula ya uhamishaji haramu wa fedha duniani yenye makao yake makuu jijini Washington Marekani inayojulikana kama Global Financial Integrity, nchi zinazoendelea zilipoteza dola za Kimarekani trilioni 7.8 kati ya kipindi cha mwaka 2004-2013. Mbaya  zaidi Ripoti hiyo inasema kuwa, tatizo hilo limekuwa likiongezeka kwa asilimia 6.5 kwa mwaka.

Wakati kiasi hicho kikipotea, inakadiriwa kuwa, jumla ya watu milioni 18 wanapoteza maisha kutokana na matatizo mbali mbali yanayotokana na hali ngumu ya kiuchumi katika nchi zinazoendelea kwa mwaka. Kiasi hiki ni wastani wa watu 50,000 kwa siku.

Mwandishi wa Makala haya alipata bahati ya kuhudhuria mkutano mkubwa uliofanyika katika mji wa Bergen nchini Norway uliojadili juu ya mambo mbalimbali kuhusiana na suala hilo pamoja na mengine.

Mkutano huo wa siku mbili ulioandaliwa na taasisi ya utafiti ya Chr. Michelsen Institute (CMI) ya Norway kwa Kushirikiana na Shule ya Uchumi ya Norway (NHH) pamoja na Tax Justice Norway uliwaleta wataalamu mbalimbali ambao wamefanya kazi katika eneo hilo pamoja na kufanya utafiti.

Profesa wa Uchumi katika Chuo Kikuu cha Mzumbe tawi la Dar es Salaam Prosper Ngowi alikuwa ni mmoja kati ya Watanzania wachache waliohudhuria mkutano huo na kutoa mada ya namna ambavyo watafiti na waandishi wa habari wanaweza kufanya kazi kwa pamoja katika jitihada za kukabiliana na matatizo mbali mbali ikiwamo tatizo hili.

Mwandishi wa makala haya alipata nafasi ya kuzungumza mambo mbali mbali na Profesa Ngowi juu ya ukubwa wa tatizo la uhamishaji fedha na alikiri kuwa suala hilo ni tatizo kubwa na kwamba limekuwa likihusisha upotevu wa kiasi kikubwa cha fedha

“Ni mabilioni ya dola kwa mwaka. Ni tatizo linalohusu makampuni, watu binafsi kama vile wanasiasa, wanamichezo maarufu na wengine. Shida kubwa ni kuwa fedha hizi zinaweza kuwa ni fedha zilizopatikana isivyo halali, ikiwemo biashara ya madawa ya kulevya, usafirishaji binadamu, uharamia, rushwa.

Ni tatizo kubwa kwa sababu fedha hizi zingebaki nchini zingebaki katka nchi hizi masikini zingesaidia maendeleo ya uchumi kama kujenga miundombinu kama barabara, reli, viwanja vya ndege nk. Pia zingesaidia upatikanaji wa huduma za jamii kama maji, afya, elimu nk. Vipo vifo ambavyo vingeweza kuepukikia kama fedha hazingekuwa zikitoroshwa,” anafafanua Prof Ngowi

Akizungumzia chanzo cha tatizo hilo anasema “tatizo ni namna fedha hizi zinavyokuwa zimepatikana. Kama ni fedha haramu na chafu, kunakuwa na haja ya wahusika kuwa na usiri na fedha hizi. Pia kuna hoja kuwa zinatoroshwa kukwepa kodi katika nchi zinakotoka.Mfano ni fedha katika Panama papers. Ubinafsi na uroho na ulafi uliopitiliza husababisha wahusika kutorosha fedha hizi. Pia hili ni tatizo la kimaadili,”

Mhadhiri huyo ambaye ni nguli katika masuala ya uchumi anasema Tanzania ni moja kati ya nchi ambazo zimeathirika na tatizo hili. Anasema tatizo lipo Tanzania na ni kubwa .

“Tunapozungumzia ‘Mabilioni ya Uswisi’ ndiyo mambo haya ya utoroshwaji. Pia katika Panama papers tunaambiwa wapo watanzania kadhaa. Ni tatizo ambalo madhara yake kwa Tanzania ni makubwa ambavyo nimeeleza hapo mwanzoni,” anasema

Kuhusiana na jitihada mbali mbali zinazofanyika kukabiliana na tatizo hili hapa nchini anasema “juhudi mbalimbali zinafanyika . Hata hivyo ili mafanikio yaweze kupatikana katika suala hili, juhudi za kitaifa tuu hazitoshi. Hili ni tatizo la kimataifa na linahitaji juhudi za pamoja za kimataifa. Nchi ambazo ni ‘tax haven’ kwa maana ya maficho ya fedha zinazotoroshwa lazima zitoe ushirikiano.

Hili limekuwa tatizo kwa sababu nchi hizi zinafaidi kutokana na fedha hizi. Hata hivyo kuna juhudi za kimataifa za kutaka uwazi zaidi zinaendelea. Nchi kama Uswisi imetoa ahadi ya kutoa ushirikiano zaidi na Tanzania kwa mfano,”

Prof Ngowi anasema kuna haja ya kufanya mambo mengi na hasa juhudi za pamoja za kimataifa; kufanya tatizo hili lifahamike na athari zake kwa nchi ni muhimu pia.

“ Pamoja na haya, ni vizuri kujua kuwa hili ni tatizo la kimaadili vilevile. Viongozi wa dini wana nafasi kubwa sana katika kupunguza na hata kumaliza tatizo hili kwa kuwakemea na kuwafundisha waumini wao,” anaeleza

Kuhusu mchango wa vyombo vya habari anasema vyombo vyote vya habari vina wajibu wa kuelimisha, kuhabarisha na kuchunguza (investigative journalism) jambo hili. “Mfano katika Panama papers waandishi wa habari walifanya kazi kubwa sana sehemu mbalimbali kama vile Iceland ambapo Waziri mkuu aliwajibika kwa kujiuzulu,”

Akiwasilisha mada katika mkutano huo, Raymond Baker ambaye ni rais wa taasisi ya Global Financial Integrity alisema taarifa mbali mbali zinaonyesha kuwepo kwa kiasi kikubwa cha fedha ambacho kimekuwa kikitoka nchi maskini kwenda nchi tajiri.

“Hii inaonesha kuwa badala ya nchi tajiri kuzisaidia nchi maskini,nchi maskini zimekuwa zikizisaidia nchi tajiri,” anasema

Baker anasema wakazi wa nchi zinazoendelea wanamiliki  jumla ya Dola za Kimarekani 4.4 trilioni katika akaunti za nje ya nchi zao ambako fedha zao pamoja na taarifa hufanywa siri kubwa.

“Kiasi cha fedha ambazo zinafichwa kwenye akaunti za nje kimekuwa kikiongezeka kwa  asilima 12 kwa mwaka. Nchi zinazoendelea ndizo zimekuwa vinara wa kuhifadhi fedha kwenye akaunti za nje ukilinganisha na nchi zilizoendelea huku suala la kuweka fedha kwenye  akaunti za  nje limekua kwa kasi kwa nchi zinazoendelea kuliko nchi zilizoendelea huku nchi zilizopo kusini mwa jangwa la Sahara Afrika zikiongoza kwa  asilimia 20,” anaeleza

Baker anasema jumla ya watu milioni 18 wanapoteza maisha kutokana na matatizo mbali mbali yanayotokana na hali ngumu ya kiuchumi katika nchi zinazoendelea kwa mwaka. Afafanua kuwa kiasi hicho ni wastani wa watu 50,000 kwa siku.

“Swali la kujiuliza hapa ni kuwa, watu wangapi wangeweza kati ya watu 50,000 wangeweza kuishi kutokana na mabilioni ambayo hutoroshwa kutoka nchni? Je, ni kiasi gani cha mapato ambacho serekali za nchi zinazoendelea zingekipata kwa ajili ya maendeleo ya wananchi wake? Je ni kiasi gani sekta binafsi ingekipata kwa ajili ya kuwekeza na kutengeneza ajira? Haya ni maswali ambayo ni lazima tujiulize na kuyapatia majibu,” anasema Baker

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles