25.2 C
Dar es Salaam
Monday, April 22, 2024

Contact us: [email protected]

MAGUFULI: MACHINGA RUKSA POPOTE

machingaa

Na WAANDISHI WETU-DAR ES SALAAM/MWANZA

RAIS Dk. John Magufuli ameagiza wafanyabiashara ndogo ndogo, maarufu machinga, wasibughudhiwe na wasiondolewe katika maeneo ya katikati ya miji wanayofanyia biashara kwani hakuna sheria inayowazuia.

Rais Magufuli alimwagiza Waziri na Katibu Mkuu katika Ofisi ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kusitisha mara moja utekelezaji wa kuwaondoa wafanyabiashara hao.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais – Ikulu, Gerson Msigwa, Rais Magufuli akiwa na Makamu wake, Samia Suluhu Hassan, alitoa agizo hilo jana Ikulu na kuonya kuwa kiongozi yeyote ambaye hayupo tayari kulitekeleza aachie ngazi.

“Kuna tabia wakuu wa mikoa, wilaya na wakurugenzi kufukuza wamachinga bila kufuata utaratibu, kama kuna asiyekubaliana na maagizo yangu, anaona yanamkwamisha, aache kazi hata leo.

“Maagizo yamekuwa mengi, mengine yanakuwa na mwelekeo wa kuchonganisha Serikali na wananchi, nilizungumza hadharani sipendi wamachinga wafanye biashara kwenye hifadhi ya barabara, lakini hakuna sheria katika nchi hii inayosema mtu wa biashara ndogondogo au machinga hatakiwi kufanya biashara katikati ya miji.

“Wamachinga wasibughudhiwe, hawakupenda kuwa machinga, naagiza Waziri na Katibu Mkuu katika Ofisi ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kusitisha mara moja kuwaondoa machinga katika Jiji la Mwanza pamoja na mikoa mingine mpaka hapo mamlaka husika zitakapokamilisha maandalizi ya maeneo watakapohamishiwa na kwa kuwashirikisha wamachinga wenyewe,” ilisema taarifa ya Ikulu ikimkariri Rais Magufuli.

Aidha video iliyosambaa katika mitandao ya jamii jana, inamwonyesha Rais Magufuli akimweleza makamu wake umuhimu wa jambo hilo.

“Nimeona nikuite wewe pamoja na hawa wa Tamisemi kwa ishu moja tu, unajua pamekuwa na maagizo mengi mengi, na maagizo mengine yanakuwa na mwelekeo wa kuchonganisha wananchi na Serikali, kwa bahati nzuri tuliozunguka kuomba kura kwa wananchi ni mimi na wewe pamoja na wabunge ndio wanajua shida halisi za wananchi.

“Kwa hali inavyoelekea, pameanza kuwa panajitokeza amri za ajabu, hasa zinazotolewa na viongozi tuliowaamini kwamba watatekeleza yale tuliyowaambia.

“Suala lililoniudhi ni hili suala la wamachinga… mimi na wewe tulizungumza kwamba tutatengeneza mazingira mazuri kwa watu hawa, watafutiwe maeneo ya kufanya biashara zao kwa utaratibu ulio mzuri.

“Ishu iliyojitokeza Mwanza nawapongeza wamachinga hawakuleta fujo, nilizungumza kwenye mkutano wa Biafra hadharani, kwamba hawa wamachinga msiwatoe mjini na kama mnatengeneza mazingira mtengeneze mazuri ya kufanya biashara ili wasizagae.

“Nilitoa mfano kwamba wanaweza kufunga barabara katikati ya mji, mkasema kwamba ndio sehemu yao kufanya biashara, lakini utaratibu umekuwa ondokeni mjini nenda Kiloleni… wanakoenda wala hawajawatengenezea mazingira mazuri, palikuwa na wanawake wanakaa Feri kuuza samaki, eti wanatolewa na kupelekwa sehemu gani, huko atauzaje samaki wake?

“Wakitaka kuwahamisha wazungumze nao kwa utaratibu mzuri na wanakowapeleka liwe ni eneo rafiki kwao na watafaidika kufanya biashara, na polisi wanatumika vibaya, wanapaswa kuzungumza nao kwanza.

“Ni lazima tujipange kutengeneza mazingira mazuri, tunapokuwa na wafanyakazi hewa zaidi ya 19,000, wanafunzi zaidi ya 65,000, mishahara hewa, hawapaswi kushangaa tunakuwa na wamachinga wengi katika nchi hii.

“Tuliwatengeneza sisi, ni lazima tuwatengenezee mazingira mazuri ya kuishi, wawaache wamachinga wafanye biashara kwenye mazingira yao.

“Nitoe wito kwa wamachinga, amri yangu hii isiwe chanzo cha wao kufanya biashara na kujenga mabanda kila mahali, hivyo basi wanapofanya biashara wasijenge mabanda kwa sababu yanachafua mandhari ya miji.

WACHIMBAJI WADOGO

Katika hatua nyingine Rais Magufuli ameagiza Wizara ya Nishati na Madini kusitisha mara kuwaondoa wachimbaji wadogo katika Kijiji cha Nyaligongo kilichopo katika Kata ya Mwakitolyo mkoani Shinyanga na badala yake waachwe waendelee na shughuli zao, na leseni ya mwekezaji anayedai eneo hilo ni lake aondolewe.

“Wale waliofukuzwa Shinyanga wabaki palepale, kama ni leseni ya huyo mwekezaji ifutwe, Makamu wa Rais fuatilia hili, mweleze Waziri wa Nishati na Madini, waache kufukuza wananchi hovyohovyo, wale wanapata riziki yao, wanasomesha watoto wao, lakini wanafukuzwa tu.

“Na hizi ndiyo ajira zenyewe, tulisema tunatengeneza ajira, wewe mwekezaji ni mmoja unakwenda kuwafukuza watu 5,000? Haiwezekani na wala haingii akilini,” alisisitiza Rais Magufuli.

Pia alikemea vitendo vya wawekezaji wakubwa kupewa maeneo ambayo wachimbaji wadogo wanaendesha shughuli zao tena kwa mtindo wa kutengeneza nyaraka zinazonyesha mwekezaji husika alipewa eneo hilo kabla ya wachimbaji wadogo na kusisitiza kuwa mchezo huo hautavumiliwa.

Alisema maagizo yake hayana maana kuwa wamachinga na wachimbaji wadogo waendeshe shughuli zao kwa kuvunja sheria bali wazingatie sheria na mamlaka zisiwanyanyase watu wanyonge.

 MWANZA

Tamko hilo la Rais Magufuli limeibua shangwe, vifijo na nderemo na kuwarejesha machinga waliokuwa wameondolewa katikati ya jiji la Mwanza na kubadili hali ya simanzi na huzuni iliyokuwa imetawala kwa muda wa siku tatu.

Wafanyabiashara hao na mafundi magari waliondolewa kupitia operesheni iliyofanywa na uongozi wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza na Manispaa ya Ilemela kwa kuvunjiwa vibanda vyao vilivyokuwa katika maeneo ya mjini.

Machinga hao walitakiwa kwenda katika maeneo ya Kiloleli, Nyegezi stendi, Buzuruga na mafundi wanaotengeneza magari  katikati ya mji walitakiwa kuhamia eneo la  Temeke-Mhandu na Sinai Mabatini.

Mwenyekiti wa Machinga Mkoa wa Mwanza, Said Tembo, alisema  anamshukuru Rais Magufuli kwa kusikiliza kilio chao kwa kuwa operesheni iliyokuwapo ilikuwa ya mateso, manyanyaso na maumivu makubwa kwa wanyonge.

Agosti 13 mwaka huu, Rais Magufuli aliutaka uongozi wa Jiji na Manispaa za Dar es Salaam kutowaondoa wafanyabiashara ndogo ‘machinga’ katika maeneo waliyopo hadi watakapowatengenezea utaratibu mzuri wa kufanya biashara zao.

Agosti 26 mwaka huu Waziri wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, George Simbachawene, alimwagiza Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kuwaondoa wafanyabiashara hao maeneo ya Kariakoo kwa sababu wanaleta usumbufu na uchafu.

HABARI HII IMEANDALIWA NA KULWA MZEE, JONNES RESPICHIUS (DAR ES SALAAM) NA JUDITH NYANGE (MWANZA)

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles