Ramadhan Hassan -Dodoma
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Dk.John Magufuli amesema katika miaka mitano ijayo Serikali yake inakusudia kuviboresha vitambulisho vya wajasirimali ili waweze kutambulika benki na hivyo kupata mikopo.
Akizungumza jana wakati akizindua Bunge la 12,Rais Magufuli alisema wakati wa kipindi cha kampeni aliahidi kwenye miaka mitano ijayo Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya kufanyia biashara kwa wajasiriamali wadogo.
“Kama mnavyofahamu kwenye miaka mitano iliyopita,tulianzisha utaratibu wa kutoa vitambulisho maalum kwa wajasiriamali wetu wadogo.
Kwenye miaka mitano ijayo tunakusudia kuviboresha vitambulisho ikiwemo kuweka picha na taarifa nyingine muhimu kama ilivyo kwenye vitambulisho vya Taifa na pasipoti.
“Hii itawezesha wafanyabishara watakaotumia vitambulisho hivyo kutambulika,ikiwemo kwenye benki na hivyo kupata mikopo kwa ajili ya kukuza biashara.
Alisema hali hiyo itawezesha wafanyabishara wadogo kukuwa kiuchumi na kutajirika ambapo alisema hilo ndio lengo la Serikali.
“Tunataka wafanyabishara wetu wadogo wawe wanakuwa na kutajirika na sio siku zote wabaki kuwa wafanyabiashara wadogo,”alisema.