31.2 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Hakuna demokrasia isiyo na mipaka – JPM

Ramadhan Hassan -Dodoma

RAIS Dk.John  Magufuli amekumbusha kuwa hakuna demokrasia isiyo na mipaka na kwamba lengo lake ni kuleta maendeleo na sio fujo.

Kauli hiyo aliitoa jana bungeni wakati akifungua Bunge la 12 ambapo alisema katika  miaka mitano ijayo,Serikali  itaendeleza jitihada za kukuza na kuimarisha demokrasia, kulinda uhuru na haki za wananchi na vyombo vya habari.

“Hata hivyo, ningependa kukumbusha kuwa  lengo la demokrasia ni kuleta maendeleo na sio fujo  na hakuna demokrasia isiyo na mipaka.

“Aidha, Uhuru na Haki vinakwenda samabamba na wajibu. Hakuna uhuru au haki isiyo na wajibu. Vyote vinakwenda sambamba,”alisema.

Pia alisema wamejipanga kuendelea kuimarisha na kukuza uhusiano  na nchi mbalimbali kwa kuzingatia Sera  ya Mambo ya Nje inayoweka msisitizo diplomasia ya kiuchumi.

“Tutakuza urafiki na ujirani mwema na pia tutashiriki kikamilifu kwenye shughuli za Kikanda, Kibara na Kimataifa, hususan kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa. Tutaendelea pia kushiriki kwenye shughuli za kulinda amani.

SINA MZAHA ANAYEHATARISHA AMANI

Rais Dk. Magufuli amesema jambo muhimu atakalolipa kipaumbele katika miaka mitano ijayo ni kuendelea kulinda na kudumisha tunu za taifa ambazo ni amani, umoja na mshikamano, uhuru na mapinduzi matukufu ya Zanzibar.

“Katika hilo, naahidi kushirikiana kwa karibu na Rais mpya wa Zanzibar, Dk. Hussein Mwinyi. Kamwe, hatutakuwa na mzaha na yeyote mwenye kutaka kuhatarisha amani ya nchi yetu, mwenye nia ya kuvuruga umoja na mshikamano wetu na pia kutaka kutishia uhuru wetu, muungano pamoja na mapinduzi matukufu ya Zanzibar,” alisema.

UTAWALA BORA

Pia  alisema kipaumbele cha pili cha serikali yake kitajikita katika kuendelea kuimarisha utawala bora hususan kwa kusimamia nidhamu kwenye utumishi wa umma na kuzidisha mapambano dhidi ya rushwa, wizi, ufisadi na ubadhirifu wa mali za umma.

“Kwenye miaka mitano iliyopita tuliwachukulia hatua za kinidhamu watumishi 32,555 na kuiwezesha nchi yetu kufika nafasi ya kwanza kati ya nchi 35 za Afrika kwa kupambana na rushwa, kwa mujibu wa Transparency International na pia kushika nafasi ya 28 kati ya nchi 136 duniani kwa matumizi mazuri ya fedha za umma kwa mujibu wa utafiti wa Jukwaa la Dunia la Uchumi, mwaka 2019.

“Hata hivyo, watumishi wazembe bado wapo, wala rushwa bado wapo na pia wezi na wabadhirifu wa mali za umma bado wapo.

“Kwa hiyo kwenye miaka mitano ijayo, tutaendelea kushughulikia matatizo hayo. Kwa kifupi niseme, utumbuaji majipu unaendelea,” alifafanua.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles