24.4 C
Dar es Salaam
Wednesday, May 25, 2022

Rais Magufuli aanika utajiri wa Gesi, kuhamasisha matumizi

Na Faraja Masinde

RAIS Dk. John Magufuli amesema Tanzania inafuti za ujazo bilioni 138 kwenye Ziwa Rukwa za gesi aina ya helium ambazo zinaweza kuhudumia dunia kwa miaka 20.

Rais Magufuli ametoa kauli hiyo leo Novemba 13, 2020 jijini Dodoma wakati akifungua bunge la 12 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuahidi kuendelea kuimarisha sekta ya nishati.

“Tuna gesi aina mbalimbali, kama vile ethane, helium, ambayo hivi karibuni zimepatikana futi za ujazo bilioni 138 kwenye Ziwa Rukwa, ambazo zinaweza kuhudumia dunia kwa miaka 20. Hii ndiyo sababu, kila siku nimekuwa nikisema, sisi sio masikini; sisi ni matajiri. Nchi yetu ni tajiri sana.

“Sambamba na hayo, kuhusu nishati, kwenye miaka mitano ijayo, tutaanza utekelezaji wa Miradi ya kielelezo (flagship projects) ya Bomba la Mafuta kutoka Hoima nchini Uganda hadi Bandari ya Tanga lenye urefu wa kilometa 1,445 pamoja na Mradi wa Kusindika Gesi Asilia (LNG) Mkoani Lindi,” amesema Rais Magufuli.

Aidha, amesisitiza Watanzania kuendelea kutumia gesi asilia pamoja na ile ya mitungi kwenye maeneo mbalimbali.

“Zaidi ya hapo, tutaendelea kuhamasisha matumizi ya gesi asilia na gesi ya mitungi majumbani, kwenye taasisi, viwanda na magari ili kupunguza uharibifu wa mazingira na athari za mabadiliko ya tabianchi,” amesema Rais Magufuli.

Aidha, akizungumzia kuhusu sekta ya nishati, nchini amesema serikali itaendelea kuimarisha miundombinu ya nishati na pia kuboresha upatikanaji wa huduma za umeme.

“Katika hilo, tunakusudia kukamilisha ujenzi wa Bwawa la kufua Umeme la Nyerere litakalozalisha Megawati 2,115 na kuanza ujenzi wa miradi mingine ya umeme wa maji Ruhudji Megawati 358; Rumakali Megawati 222; Kikonge Megawati 300 na pia umeme wa gesi asilia Mtwara Megawati 300; Somanga Fungu Megawati 330, Kinyerezi III Megawati 600 na Kinyerezi IV Megawati 300; pamoja na miradi mingine midogo midogo.

“Aidha, tunakusudia kuzalisha umeme Megawati 1,100 kwa kutumia nishati jadidifu (jua, upepo, jotoardhi),” amesema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
192,160FollowersFollow
541,000SubscribersSubscribe

Latest Articles