26 C
Dar es Salaam
Monday, March 4, 2024

Contact us: [email protected]

Vita ya urais yatua bungeni

Mh.-Stephen-WassiraNa Maregesi Paul, Dodoma

VITA ya urais imetua bungeni, baada ya mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola (CCM), kuwatahadharisha Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu na Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Steven Wasira, kwamba harakati zao za kugombea urais hazitafanikiwa kama watashindwa kutatua kero za wananchi.
Akichangia taarifa ya utekelezaji wa kazi za Kamati ya Ardhi, Maliasili na Mazingira kwa kipindi cha mwaka 2014 mjini Dodoma jana, Lugola alisema kama mawaziri hao watataka kufanikiwa, lazima waonyeshe uwezo wa kutatua kero zinazowakabili wananchi katika maeneo yao.
Akimzungumzia Wasira, alisema waziri huyo anatakiwa kuitumia vizuri nafasi yake kutatua kero za wakulima wa pamba nchini kwa kuwa Serikali imekuwa ikiwapelekea mbegu zisizoota na kuwafanya waendelee kuwa masikini.
“Mheshimiwa Wasira, mimi nakuamini sana, naomba utumie ‘u-Tyson’ wako kutatua kero za wakulima wa pamba wa Kanda ya Ziwa na usitumie ‘u-Tyson’ wako katika majukwaa ya siasa peke yake.
“Mimi nakuhakikishia nitakuunga mkono, na kwa sasa nafanya uchunguzi kuhusu fedha zinavyoliwa katika Bodi ya Pamba Tanzania na nitakapoukamilisha, nitaleta bomu hilo hapa bungeni.
“Mheshimiwa Wasira, hata yale mambo yako unayohangaika nayo, nakwambia hutafanikiwa kama utashindwa kutatua kero ya wakulima wa pamba,” alisema Lugola bila kutaja ni mambo gani anayohangaika nayo Wasira, ingawa ni wazi alimaanisha urais.
Akimzungumzia Waziri Nyalandu, alisema anatakiwa kutatua kero za wananchi wa Jimbo la Mwibara, ambao mara kadhaa wamekuwa wakiwapoteza ndugu zao kutokana na kuliwa na mamba na viboko.
“Mheshimiwa waziri, nimewahi kukwambia wananchi wa Mwibara wanaliwa na mamba na viboko, lakini hutaki hata kwenda kuwasaidia.
“Nakwambia kama hutafanya mkutano na hao viboko na mamba wako hao, hata huo urais unaoutaka hutafanikiwa. Mamba na viboko wanatafuna wananchi wangu na juzi juzi wamemtafuna mwananchi aliyekuwa akinisaidia kwenye kampeni, sasa unataka nirudishwe hapa bungeni na akina nani kama wananchi wangu wanaliwa?
“Nakwambia hayo mambo unayohangaika nayo hutafanikiwa kwa sababu huwezi kushindwa kuwadhibiti wanyama halafu ukataka kuingia Ikulu, hutafanikiwa,” alisema Lugola.
Akizungumzia sekta ya maji, Lugola aliwataka wananchi wa Jimbo la Bunda na Mwibara, wasiipigie kura CCM wakati wa uchaguzi mkuu mwaka huu kama Serikali itashindwa kutekeleza miradi ya maji katika maeneo yao.
“Pale Bunda kuna mradi wa maji kutoka Ziwa Victoria, hadi sasa haujatekelezwa jambo linalowafanya wananchi wanywe maji machafu.
“Kuna miradi mingine jimboni kwangu katika vijiji vya Bulamba na Kibara nayo haijatekelezwa. Kwahiyo wananchi wa Bunda na Mwibara kama mnanisikia, nawaomba wakati wa uchaguzi mkuu msiipigie kura CCM kama miradi ya maji haitakuwa imetekelezwa.
“Naamini wakati wa uchaguzi mkuu CCM itaendelea kushinda, lakini hata mimi mwenyewe msinipigie kura kama hiyo miradi haitakuwa imetekelezwa kwa sababu mmekuwa mkifanya kazi kubwa ya kuitetea na kuibusu CCM bila mafanikio,” alisema Lugola.

Lukuvi alipuliwa

Katika hatua nyingine, Lugola alimlipua Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, kwamba anashirikiana na baadhi ya wawekezaji kuihujumu Halmashauri ya Manipaa ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.
Akichangia taarifa ya utekelezaji wa kazi za Kamati ya Ardhi, Maliasili na Mazingira kwa kipindi cha mwaka 2014, Lugola alisema Lukuvi amekuwa mstari wa mbele kumtetea mwekezaji wa kigeni katika mradi wa Kinondoni Villa, wakati akijua kufanya hivyo analikosesha mapato taifa.

Alisema kitendo cha Lukuvi, kimemfanya mwekezaji huyo awe na kiburi cha kutowaheshimu Watanzania.
“Mheshimiwa Spika, migogoro ya ardhi ni ya kihistoria katika nchi hii, na haitakwisha kama viongozi wa Serikali hawataacha tabia ya kuwabeba watu.
“Wako viongozi wengine ndio wanaomiliki maeneo na wako viongozi wengine ndio wanaowabeba wawekezaji kwenye mbeleko wakati wakijua wanakiuka sheria.
“Kwa mfano, kuna yule mwekezaji wa Oysterbay Villa, yeye aliingia mkataba wa uwekezaji wa viwanja viwili na Manispaa ya Kinondoni na wakati anaingia mkataba huo, Lukuvi ndiye aliyehusika akiwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam.
“Huyu Lukuvi ndiye aliyehakikisha huyu mwekezaji anapata lile eneo na sasa ndiye ameteuliwa kuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
“Yule mwekezaji anabebwa na Lukuvi na ndiye anayempa kiburi cha kuwadharau Watanzania, kwa sababu siku moja sisi Kamati ya Bunge tulikwenda pale akatuzuia kuingia kwenye mradi.
“Yule mwekezaji anajifanya ni ‘baunsa’, alituzuia kuingia pale, lakini mimi nikatumia ‘ubaunsa’ wangu kumhakikishia kwamba, Tanzania kuna mabaunsa zaidi yake, nikamdhibiti, tukafanikiwa kuingia.
“Nawaambia yule mwekezaji anabebwa na mbeleko ya Lukuvi na nakuhakikishia Lukuvi usipoacha kumbeba, ipo siku nitaichoma hiyo mbeleko yako,” alisema Lugola.
Pia, alionyesha kutoridhishwa na tukio la askari polisi kumpiga Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, kwa kulieleza Bunge kwamba nguvu zilizotumika kumdhibiti pamoja na wenzake, ziwe zinatumika kuwadhibiti viongozi wanaosababisha migogoro katika maeneo mbalimbali nchini.
Hata hivyo, kauli ya Lugola ya kumshambulia Lukuvi ilipingwa na Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (Chadema), ambaye alimtetea kwa kusema ndiye aliyesaidia kuboreshwa kwa mkataba wa mradi huo kutoka miaka 99 iliyokuwa imekubaliwa hadi chini ya miaka hiyo.
“Mheshimiwa Kangi, katika hili naomba nimtete Lukuvi kwa sababu ndiye aliyesaidia kuboresha mkataba ule. Naomba nimtetee Lukuvi kwa sababu alijitahidi sana kutatua ule mgogoro katika eneo hilo, nakuomba Mheshimiwa Kangi katika hili tusimlaumu Lukuvi,” alisema Zitto.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
584,000SubscribersSubscribe

Latest Articles