24.4 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

JK aibua mambo urais CCM

Jakaya-KikweteEsther Mbusi na Aziza Masoud, Dar es Salaam
SIKU moja baada ya Rais Jakaya Kikwete kuwaonya wagombea urais ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) pamoja na kuzungumzia mchakato wa kura ya maoni ya Katiba Mpya, wasomi mbalimbali wametoa maoni yao kuhusu hotuba yake.
Aliyekuwa Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Azaveri Lwaitama, alisema rais anashauriwa vibaya kuhusu mchakato wa Katiba Mpya kuelekea katika kura ya maoni.
Alisema tayari viongozi wa dini wamemsihi kutoharakishwa kwa mchakato huo na kulazimisha kufanya hivyo ni hatari kwa mustakabali wa Katiba tarajiwa.
“Viongozi wa dini wamesema Jaji Joseph Warioba ambaye ni mwanachama hai wa CCM naye ameonya kuhusu uharakishwaji wa mchakato wa Katiba hii, ambapo rais anasema kura ya maoni ni katikati ya Aprili na gharama zake hazipo.
“Katiba ni muhimu kuliko wagombea wa CCM, hivyo mchakato wake usivurugwe,” alisema Dk. Lwaitama.
Kwa upande wake, Mhadhiri Mwandamizi wa Sayansi ya Siasa kutoka Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino (SAUT), Profesa Mwesiga Baregu, alisema kauli ya Rais Kikwete kuhusu mgombea urais wa CCM inaonyesha chama hicho hadi sasa hakina mgombea.
Alisema Rais Kikwete alikuwa anazungumza kama kiongozi, lakini hajafikiria kama upinzani pia unaweza kutoa rais.
“Alikuwa anazungumza kama kiongozi, hajafikiria mgombea urais anaweza akatoka upinzani, lakini katika chama chake si kwamba wagombea hawajajitokeza, ila waliojitokeza hawatoshi.
“Amesaidia kuona kuwa CCM hadi sasa haina mgombea urais, hivyo Watanzania watafute mbadala Ukawa,” alisema Baregu.
Akizungumzia kuhusu mchakato wa kura ya maoni, Baregu alisema alianza kuuharibu tangu awali wakati akifungua Bunge la Katiba kwa kutoa mawazo yake bungeni.
“Ukawa tofauti yao si Serikali tatu, mimi sielewi hata kapata wapi haya maneno, malalamiko ya Ukawa yalianzia kwake alipozindua Bunge, alichangia kuharibu mambo mengi, ambayo yalikuwa yanawapa mamlaka wananchi yamekatwa katika rasimu,” alisema Profesa Baregu.
Alisema Rais Kikwete asione jambo hilo ni jepesi kwa kuwa rasimu iliyokuwa na vitu vya msingi ilipinduliwa na kusababisha wananchi kugawanyika.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Benson Bana, alisema Rais Kikwete amesisitiza wananchi wasiridhike na wagombea waliopo, hivyo jamii inapaswa kuwaibua wagombea wapya suala ambalo ni la msingi kwa sasa.
“Kuna haja ya marais wastaafu watusaidie hatua ya kuibua mgombea mpya wa urais ambaye atakuwa bora kama Mwalimu Nyerere alivyomuibua Mkapa.
“Nadhani hilo ndilo lingekuwa la msingi zaidi… wananchi pekee tutakuwa na kazi kubwa tukisema tufanye hivyo,” alisema Dk. Bana.
Juzi Rais Kikwete, akizungumza katika kilele cha maadhimisho ya miaka 38 ya CCM mjini Songea, aliwaonya watu wanaotaka kuwania urais kupitia chama hicho, akisema endapo watavunja sheria na kanuni, wasikilaumu chama hicho bali wajilaumu wenyewe.
Kuhusu Katiba inayopendekezwa, alisema anaamini itapita katika kura ya maoni Aprili 30, hata kama Ukawa wanapambana kupiga kampeni ya kuihujumu ili kupigiwa kura ya hapana.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles