30.9 C
Dar es Salaam
Wednesday, October 30, 2024

Contact us: [email protected]

VITA LIGI YA MABINGWA ULAYA WIKI HII TUMWACHIE MUNGU

BADI MCHOMOLO NA MITANDAO


SIKU zote bahati haijirudii mara mbili hasa katika soka, inakuja mara moja na hiyo ya pili inatakiwa jitihada zako.

Wanasema ukibebwa unatakiwa ujishikize ili uweze kufika sehemu ambayo umekusudia, lakini kama utashindwa kujishikiza basi unaweza kuachwa njiani watu wakaendelea na safari.

Hakuna ambao waliamini kama Barcelona ilitumia jitihada zake yenyewe kuweza kupata ushindi dhidi ya PSG katika hatua ya 16 bora kwenye mchezo wa pili wa marudiano ambapo Barca walitakiwa kushinda mabao 5-0 kuweza kusonga mbele.

Waliweza kufanya hivyo kwa kushinda mabao 6-1 na kusonga hatua inayofuata. Wengi waliwatupia lawama PSG kuruhusu idadi hiyo kubwa ya mabao baada ya mchezo wao wa awali PSG kushinda mabao 4-0.

Lakini wengi waliamini kuwa Barcelona walishinda na kusonga mbele hatua inayofuata kutokana na kubebwa na mwamuzi wa mchezo huo.

Japokuwa walionesha kiwango kizuri lakini ushindi wao ulitokana na kubebwa na wakajishikiza vizuri. Swali lililobaki kwa mashabiki hao ni je, Barcelona wataweza kusonga mbele nusu fainali dhidi ya Juventus?

Barcelona vs Juventus

Wiki iliyopita mashabiki wengi walikuwa na furaha kubwa kuona Barcelona ikipoteza mchezo wao dhidi ya bibi vizee wa mjini Turin, Juventus kwa kichapo cha mabao 3-0.

Hii iliwapa faraja wengi ambao walichukia Barcelona kushinda kwao dhidi ya PSG, lakini mchezo huo ulikuwa wa kwanza hatua ya robo fainali na sasa ni marudio hivyo Barcelona wapo kwenye mipango ya kulipiza kisasi.

Imani kubwa ya wengi ni kwamba, Barcelona safari yao katika michuano hiyo ya Ligi ya Mabingwa imefikia mwisho, ila wapo ambao wanaamini kuwa soka ni mchezo wa makosa hivyo Juventus wanaweza kufanya makosa na Barcelona wakatumia nafasi hiyo na kushinda kisha kusonga mbele.

Barcelona wanahitaji mabao 4-0 kuweza kusonga mbele hatua ya nusu fainali, lakini kutokana na ukuta wa Juventus, Barcelona kuweza kusonga mbele basi tumwachie Mungu.

Wapo wanaoamini kuwa Barcelona ni klabu ambayo inaweza kubadili matokeo muda wowote na kuishangaza dunia hasa pale wanapokuwa kwenye uwanja wa nyumbani wa Camp Nou.

Camp Nou ni miongoni mwa viwanja ambavyo vinaingiza idadi kubwa ya watazamaji huku kikichukua watu 99,354, hivyo Barcelona wanakuwa wanajitanua vizuri mbele ya mashabiki wao, je, wanaweza kutamba katika mchezo wao wa keshokutwa dhidi ya Juventus?

Monaco vs Dortmund

Huu ni mchezo mwingine ambao utapigwa keshokutwa, mchezo huo utakuwa mgumu sana kutokana na tofauti ya mabao waliyonayo.

Mchezo uliopita Dortmund walikuwa kwenye uwanja wa nyumbani na walikubali kichapo cha mabao 3-2, hivyo mchezo huo ujao Dortmund wanahitaji ushindi wa mabao 2-0 ili kusonga mbele, wakati huo wapinzani wao wanahitaji sare ya aina yoyote, ushindi na hata wakifungwa bao 1-0 bado watasonga mbele.

Chochote kinaweza kutokea hasa kutokana na ubora wa Dortmund hasa katika safu ya ushambuliaji ambayo inaongozwa na Pierre Aubameyang, inaweza kufanya maajabu na kushangaza mashabiki.

Real Madrid vs Bayern Munich

Huu ni mchezo mwingine ambao unatarajia kuteka hisia za mashabiki na wadau mbalimbali wa soka duniani kwa ujumla.

Kwa upande wa mashabiki wa Arsenal ni wazi dua zao kubwa ni kuiombea Bayern Munich kichapo kingine ili iweze kuyaaga mashindano hayo, hiyo ni kutokana na Arsenal kukubali kichapo cha jumla ya mabao 10-2 huku kila mchezo hatua ya makundi Arsenal wakifungwa mabao 5-1.

Bayern Munich walikubali kichapo cha mabao 2-1 kwenye uwanja wa nyumbani wa Allianz Arena kwenye mchezo wa kwanza.

Mchezo wa kesho Bayern wanahitaji ushindi wa mabao 2-0 ili kusonga mbele. Mchezo huo utakuwa na ushindani wa hali ya juu kutokana na ubora wa timu hizo.

Wengi wanaamini Bayern wanaweza kufanya maajabu makubwa katika mchezo huo kutokana na ubora wa kikosi chao msimu huu, wakati huo imani ikiwa ndogo kwa Real Madrid kuweza kulinda ushindi wao wa mchezo uliopita.

Leicester City vs Atletico Madrid

Mchezo uliopita Atletico Madrid walikuwa kwenye uwanja wa nyumbani na kufanikiwa kushinda bao 1-0, lakini mashabiki wengi walipingana na bao hilo.

Wengi kwenye mitandao ya kijamii walidai kuwa bao hilo la mkwaju wa penalti haikuwa penalti sahihi kwa kuwa mshambuliaji wa Atletico Madrid, Antoine Griezmann, alichezewa vibaya nje ya 18 lakini mwamuzi aliweka tuta.

Baadhi ya wachambuzi wa soka waliweka wazi kuwa haikuwa penalti sahihi, ilikuwa ni kosa la mwamuzi ila tukio lilifanyika nje ya 18 na mshambuliaji huyo kuangukia ndani ya boksi kisha mwamuzi kuruhusu penalti ambayo iliwaua Leicester City.

Lakini Leicester City ni klabu pekee kutoka nchini England ambayo imebaki katika michuano hiyo, hivyo imeonesha ushindani wa hali ya juu ikiwa ni mara yake ya kwanza kushiriki michuano hiyo.

Wapo ambao wanaamini Leicester City kesho wanaweza kufanya maajabu kwenye uwanja wao wa nyumbani kutokana na mchezo wao uliopita dhidi ya wapinzani hao kuonesha ukakamavu wa hali ya huu.

Lakini yote kwa yote wiki hii itatoa timu nne ambazo zitashiriki nusu fainali na nne zitayaaga mashindano hayo, zipi zitaingia nusu fainali? Tumwachie Mungu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles