26.5 C
Dar es Salaam
Tuesday, January 18, 2022

YANGA IMEANGUSHWA NA MENGI MICHUANO YA AFRIKA

Na ABDUL MKEYENGE-DAR ES SALAAM


NI simanzi.Ndiyo simanzi imetawala kwa mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara timu ya Yanga, baada ya kufungwa mabao 4-0 katika michuano ya Afrika na timu ya Mouloudia Club Alger ya Algeria.

Hii si taarifa nzuri inayoweza kupendwa na Wanayanga ambao wakati huu wanapitia kipindi kigumu kwenye historia ya klabu yao. Yanga wamekutana na kipigo hicho, huku wakiwa na hali mbaya ya kifedha iliyotajwa kuwafanya wawakose baadhi ya wachezaji wao waliokataa kuongozana na timu nchini humo kutokana na malimbikizo ya mshahara wake. Ni simanzi kwa kweli.

Mpaka Yanga imetolewa kwenye michuano hiyo ya kimataifa na sasa kugeukia michuano ya ndani pekee, imeangushwa na vitu vingi vilivyowafanya washindwe kutamba msimu huu na kushindwa kutinga hatua ya makundi ambayo msimu uliopita ilitolewa kwenye hatua hiyo.

Yafahamu baadhi ya mambo hayo yaliyowafanya watolewe na kurudi nyumbani wakiwa na lundo kubwa la mabao, huku kwenye ligi ya ndani wakiwa hawako katika kiwango chao bora.

Matatizo ya Mwenyekiti

Tangu Februari 2017, Mwenyekiti na mfadhili wa klabu hiyo Yussuph Manji kuwa na matatizo yake binafsi hali ya kikosi cha Yanga kuyumba ilianzia hapa. Matatizo hayo ya Manji yaliingia mpaka ndani ya timu ambako hakukujengwa misingi sahihi ya uendeshaji na kufanya taarifa nyingi za huzuni kuanza kusikika klabuni hapo.

Manji ni kila kitu Yanga. Hivyo alivyokuwa na matatizo hayo kwa hali yoyote ile lazima klabu ikutane na wakati mgumu. Wachezaji wanashindwa kupata stahiki zao kwa wakati na kufanya Obrey Chirwa na Vincent Bossou kutajwa kuigomea safari ya Algeria kutokana na mishahara wanayoidai klabu.

Kama Yanga wanahitaji kufanya vizuri kwenye michezo ya ligi ya ndani na msimu ujao warejee tena kwenye michuano ya kimataifa wanahitaji kujipanga upya juu ya hali hii iliyonayo klabu hivi sasa.

Ubora wa timu kiujumla

Licha ya timu kuwa katika matatizo ya kifedha, lakini ndani ya uwanja Yanga imeshuka kiwango chake. Wachezaji hawana morali ya upambanaji kama msimu uliopita na kuifanya kila mtu aitazame Yanga kwenye kila jicho. Wapo wanaosema wachezaji wana uchovu baada ya kucheza kwenye kiwango kikubwa msimu uliopita, huku wengine wakisema suala la kutosajili wachezaji kwenye maeneo muhimu limeifanya timu iwe kwenye sura hii. Kila mmoja anasema lake.

Kufanya vizuri kwa Yanga ndani ya msimu huu michuano ya kimataifa kulihitaji ubora wa timu kiujumla na ubora wa wachezaji binafsi. Lakini Yanga imeenda katika michuano ya kimataifa ikikosa ubora wa kikosi chao na ubora wa wachezaji wao binafsi ambao msimu uliopita Yanga walikuwa na vitu vyote viwili.

Mabadiliko ya benchi la ufundi

Sehemu nyingine iliyowazima Yanga msimu huu ni kwenye eneo hili muhimu kikosini.

Tangu kuanza kwa msimu huu Yanga hawakuwa na imani na kocha wao Mdachi Hans Van Pluijm na mara kwa mara kutoka taarifa kuwa Mdachi huyo ataondolewa na kuja kocha mpya.

Hali hii sintofahamu ilimfanya Pluijm kuitazama zaidi kesho yake kikosini na sio kujikita katika mbinu za ufundishaji na kuipa timu mafanikio. Haikuchukua muda kile alichokuwa akikisikia Pluijm kuwa atatimuliwa kilikuja kuwa kweli, kocha huyo akaondoka na George Lwandamina akaja kuchukua nafasi yake.

Kila kocha akija ndani ya kikosi anakuja na mbinu zake za ufundishaji na hali hii ndiyo iliyoirudisha nyuma Yanga ambao tayari walikuwa na kikosi chao cha kwanza kilichokuwa na maelewano mazuri ndani ya uwanja.

Majeraha kwa wachezaji muhimu

Hali za nyota wake Thaban Kamusoko, Donald Ngoma, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ , Ammis Tambwe, Juma Abdul kuwa na majeraha kila wakati, nayo imesababisha Yanga kuwa na hali hii ya sasa.

Wachezaji hao ni sehemu ya wachezaji muhimu waliokuwa na mchnago mkubwa msimu uliopita ambao Yanga walikuwa na kikosi bora, lakini msoimu huu wengi wamekuwa katika majeraha na kuifanya timu ikose ‘mseto’ wake.

Baada ya Ngoma na Tambwe kuwa katika majeraha hayo, ikawalazimu Yanga kuwategemea Chirwa na Simon Msuva katika suala la kufunga mabao, lakini bado umuhimu wa Ngoma na Tambwe ulionekana katika mingi ambayo timu ilikuwa ikicheza.

Morali ya mashabiki kwa timu

Msimu huu mashabiki wa Yanga wamekuwa wazito kuiunga mkono timu yao kama ilivyokuwa msimu uliopita ambako madshabiki walikuwa wakihama viwanja na timu yao. Kila iliko Yanga kuna mashabiki ilikuwa lazima uwaone jukwaani wakihamasishana kushangilia, lakini msimu huu hali hii haiko tena.

Mshabiki ni mchezaji wa 12 uwanjani. Yanga ilikosa mchezaji wake wa 12 na kufanya wachezaji wenyewe kukosa hamasa ambayo walizoea kuipata kutoka kwa mashabiki wao.

Usajili

Hili ni eneo jingine kubwa lililochangia kuanguka kwa kiwango cha timu msimu huu. Benchi la ufundi lioliloingia Dirisha dogo la usajili limeshindwa kusoma alama za nyakati kwa kusajili wachezaji ambao walikuwa wakihitajika kikosini.

 Yanga ilikuwa na mahitaji ya kiungo cha ukabaji ambacho wachambuzi wa masuala ya soka nchini wamekuwa wakisema tangu kuondoka kwa wachezaji Frank Domayo na Athuman Iddy ‘Chuji’, Yanga imekosa wachezaji sahihi wa kucheza eneo hilo.

Kuna wakati kiraka Mbuyu Twite aliyejiunga na Fanja ya Oman alikuwa akicheza eneo hilo na kupunguza matatizo ya safu ya ulinzi, Lwandamina alikuja kumtema katika dirisha dogo na kumsajili kiungo Justice Zulu ambaye anatajwa kutokuwa na ubora mkubwa.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
174,926FollowersFollow
531,000SubscribersSubscribe

Latest Articles