Mwandishi Wetu na Mashirika ya Habari
UNAWEZA kusema hali si shwari tena duniani kutokana na virusi vya corona kuendelea kusambaa na kufika katika nchi takribani 40 huku mataifa mbalimbali yakionekana kuchukua hatua za kujifungia mipaka.
Athari pia imeonekana wazi kwenye uchumi baada ya masoko kuendelea kuanguka katika maeneo mbalimbali duniani.
Wakati mataifa mbalimbali duniani yakiendelea kuchukua hatua za kujilinda kwa kujifungia mipaka na watu waliokuwa China vilikoanzia virusi hivyo, Nigeria na nchi tano nazo tayari zimekumbwa na upepo huo mbaya.
Jana Nigeria ilithibitisha kuwepo kwa mtu mmoja mwenye maambukizi ya virusi vya corona na hivyo kuingia katika orodha ya nchi tatu barani Afrika baada ya Misri na Algeria.
Mgonjwa huyo, raia wa Italia anayefanya kazi nchini Nigeria inaelezwa alisafiri kwa ndege kwenda mji wa kibiashara wa Lagos akitokea Milan Februari 25.
Mamlaka zinasema anaendelea vizuri na hakuna dalili ya hatari na hivi sasa anapatiwa matibabu hospitalini jijini Lagos.
Mamlaka zimesema zimeanza kuwatambua wale wote waliokaribiana naye tangu aliporejea Nigeria.
Zaidi ya watu 80,000 wameripotiwa kuathirika katika nchi 40 na zaidi ya watu 60 wamepoteza maisha nje ya China ingawa idadi ya maambukizi nchini humo imeendelea kushuka.
NCHI ZAZIDI KUFUNGA MIPAKA
Nchi ya India nayo imetangaza kuchukua hatua inayofanana na ile ilichokuliwa mwanzo kabisa na Marekani na nchi nyingine za Ulaya ya kupiga marufuku raia waliokuwa China kuingia nchini humo.
Katika taarifa yake India imeeleza kuwa raia yeyote wa kigeni aliyekuwa China baada ya Januari 15, 2020 hataruhusiwa kuingia nchini humo kupitia usafiri wa anga, barabara au majini na katika mipaka yake yote na nchi za Nepal, Bangldesh na Myanmar.
Hatua hiyo ya India imekuja baada ya ile ya Saudi Arabia ya kuzuia wageni wote wanaoingia nchini humo kwa safari za kidini, ikiwemo wanaotembelea miji mitakatifu katika dini ya Kiislamu – Makka na Madina.
Bado haijajulikani kama ibada ya Hija, ambayo inategemewa kuanza mwishoni mwa mwezi Julai iwapo itaathirika na zuio hilo kutokana na kusambaa kwa virusi vya corona duniani.
Urusi nayo ilikuwa ni miongoni mwa nchi za mwanzo kutangaza kufunga mipaka yake na China kama njia ya kujilinda na maambukizi ya virusi hivyo.
Mapema hivi karibuni Urusi pia ilitangaza kuzuia raia wa Iran kuingia nchini humo.
Urusi pia ilisema itazuia raia wa Korea Kusini kuingia nchini humo kuanzia Machi 1.
Nchi hizo zote mbili, Iran na Korea Kusini zimeshambuliwa na virusi hivyo.
Mamlaka ya nchini Iran inasema virusi hivyo vimesababisha vifo vya zaidi ya watu 24 hadi sasa, huku idadi ya walioathirika ikiwa ni karibu ya 250.
Jana Wizara ya Afya ilitangaza kufuta sala ya Ijumaa katika miji mikubwa yote.
Waislamu wanasali mara tano kwa siku, lakini sala ya Ijumaa inaonekana kama ni muhimu sana.
Korea Kusini kwa upande wake imetoa rekodi inayoonyesha watu 2,000 wameathirika na virusi hivyo huku 13 wakipoteza maisha.
Urusi pia imezuia raia wa China kuingia nchini humo.
Afrika Kusini nayo inaonekana kutaka kuelekea njia hiyo hiyo, kutokana na uamuzi wa Rais wake, Cyril Ramaphosa wa kuwaondoa raia wa Afrika Kusini 132 wanaoishi mjini Wuhan nchini China.
Uamuzi ulitangazwa siku ya Alhamisi baada ya kikao cha baraza la mawaziri kutokana na maombi ya wana familia wa raia hao wanaoishi Wuhan.
Haikuelezwa ni lini wataondoshwa huko lakini serikali imesema raia 132 kati ya 199 wanaishi mjini Wuhan wameomba warejee nyumbani.
Hakuna kati yao aliyegundulika kuathirika na virusi au kuwa na dalili za ugonjwa huo, lakini watawekwa karantini kwa siku 21 watakapowasili nchini Afrika Kusini kama ”hatua ya tahadhari”, ofisi ya rais imetangaza.
Sanjali na hilo, Shirika la ndege la Afrika Kusini limesitisha safari za moja kwa moja kwenda China.
ATHARI KWENYE MASOKO
Wakati kukiwa na orodha ya mashirika kadhaa ya ndege yaliyotangaza kusitisha safari zake nchini China kutokana na mlipuko wa ugonjwa huo, Shirika la ndege la nchini Uingereza la EasyJet limesitisha pia baadhi ya safari zake nchini Italia ambako virusi hivyo vimeonekana kutikisa na kusababisha vifo na maambukizi kwa watu kadhaa.
Katika taarifa yake iliyotolewa jana EasyJet ilisema imesitisha baadhi ya safari zake za ndani na nje ya Italia na katika mataifa mengine ya Ulaya kutokana na mlipuko wa virusi hivyo.
EasyJet pia imesema itapunguza matumizi yake, ikiwa ni pamoja na mishahara, kusitisha kuajiri watu wengine na kutoa mafunzo.
Shirika la ndege la British Airways nalo linatarajia kusitisha baadhi ya safari zake katika nchi za Italia, Singapore, na Korea Kusini.
Shirika hilo la ndege limesema pia litasitisha safari za kwenda na kurudi 56 kutoka katika viwanja vya ndege vya Heathrow na Gatwick na nyingine kadhaa za Italia ikiwamo Milan, Bologna, Venice na Turin kati ya Machi 14 – 28.
Pia itasitisha safari za kurudi sita kutoka Heathrow kwenda Singapore kila baada ya siku nyingine hadi Machi 15 ambapo itakuwepo safasi moja tu kwa siku
Wakati huo huo, Soko la hisa la Australia Ijumaa – lilishuka kwa 3.3% hadi 6,441.
ASX200 imeanguka zaidi ya 10% tangu rekodi yake ya hivi karibuni ya 7,162 Alhamisi iliyopita.
Hili ndilo anguko kubwa la kila wiki kwa soko la Australia tangu mwaka 2008, wakati wa mtikisiko wa uchumi duniani.
NCHI TANO ZATHIBITISHA MAAMBUKIZI MAPYA
Nchi za New Zealand, Netherlands, Belarus, Nigeria na Lithuania zimethibitisha kisa cha kwanza cha virusi vya corona.
Hali hiyo inaonyesha kitisho cha kuendelea kuenea kwa virusi hivyo katika nchi nyingine duniani.
MASHINDANO YASITISHWA
Umoja wa nchi za Kiarabu umesitisha mashindano ya fainali za baiskeli kwa mwaka huu wa 2020 baada ya Waitaliano wawili wanaoshiriki kwenye timu kuonekena kuambukizwa virusi hivyo.
Waitaliano hao sasa wanachunguzwa.
Wengine waliokaribiana na Waitaliano hao watawekwa chini ya uangalizi.
MICHUANO YA OLYIPIKI HATARINI
Waandaaji wa mashindano ya Olimpiki kwa mwaka huu wa 2020, Japan wamesema watatangaza wakati wowote wiki ijayo juu ya mipango ya michezo hiyo katika wakati huu ambako virusi vya corona vimeendelea kuwa tatizo la kidunia.
Tayari watu nane wamefariki dunia nchini Japan, huku karibu 200 wakiwa wameathirika na virusi hivyo ( maambukizi hayo ni mbali na yale ya kwenye meli ya Diamond Princess).