Na Kulwa Mzee-Dar es Salaam
MARA kadhaa tumekuwa tukikumbushana kuhusu haki za watoto na wajibu wa kila mmoja kuhakikisha analinda haki hizo.
Wadau mbalimbali na Serikali kila wakati wamekuwa wakisisitiza na kuwaelimisha Watanzania kuhusu haki hizo, lengo likiwa ni kuhakikisha mtoto hanyanyasiki katika mazingira ya aina yoyote.
Ushauri umekuwa ukitolewa kwa wanafamilia, wahakikishe wanakuwa makini katika mazingira ya nyumbani, wanatakiwa kuacha tabia ya kuwalaza watoto chumba kimoja na wageni hata kama ni ndugu.
Hayo yanafanyika si kwa kuwanyanyapaa wageni bali kwa kuwalinda watoto na watu ambao si waungwana, hawajui thamani ya mtoto.
Sheria ya Mtoto namba 21 ya mwaka 2009 ya Tanzania inasema hakuna anayeruhusiwa kumdhuru, kumwumiza au kumnyonya mtoto.
Yeyote anayejua kwamba kuna mtoto anayeonewa au kutendewa vibaya hana budi kutoa taarifa kuhusu vitendo
hivyo.
Wazazi na walezi hawana budi kuwalinda watoto dhidi ya madhara yoyote. Vilevile ni lazima wahakikishe kwamba watoto wanapata chakula, mavazi na mahali salama pa kuishi.
Ni kinyume cha sheria kwa mtu yeyote kumnyanyasa mtoto eti kwa sababu ni msichana au mvulana au kwa sababu ya umri wake, dini, asili yake au kwa sababu yeye ni fukara.
Nimeguswa kuandika haya baada ya kuona mtu aliyepewa madaraka akiaminiwa kwamba anaweza kushirikiana bega kwa bega na Serikali ama wadau katika kuhakikisha mtoto analindwa anafanya unyama kwa watoto.
Hivi karibuni iliripotiwa kwamba Ofisa Mtendaji wa Kata ya Mkuyuni wilayani Nyamagana mkoani Mwanza, James Chiragwire (42), alikuwa akishikiliwa na Polisi kwa tuhuma za kumbaka mtoto ambaye ni mwanafunzi wa Shule ya Msingi Nyabulogoya mkoani humo, mwenye umri wa miaka 11.
Inadaiwa kuwa mtuhumiwa kabla ya kutokea kwa tukio hilo alikuwa na mazoea ya kumchukua mtoto huyo na kuingia naye ndani kwake na kumpatia fedha na zawadi ndogondogo, siku ya tukio alipofika nyumbani kwao alimkuta mtoto peke yake alimchukua na kumfunga kitambaa usoni kisha akaingia naye ndani kwake na kumfanyia ukatili huo.
Mtoto huyo alifanyiwa uchunguzi na daktari na kubainika kweli aliingiliwa kimwili na alipatiwa matibabu katika Hospitali ya Mkoa ya Sekou Toure.
Kaimu kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Kamishina Msaidizi wa Polisi, Augustino Senga, alitoa wito akiwataka wakazi wa Mwanza kuwa makini wakati wote na watoto wadogo na kusema kuwa wasiachwe peke yao ili kuepusha vitendo kama hivyo.
Tukio hili linaacha maswali mengi ambayo hayana majibu hasa kwa kuzingatia mtuhumiwa ni kiongozi, majibu yatapatikana pale tu mahakama itakapoanza kusikiliza kesi hiyo na kufikia hukumu.
Tunajiuliza kwanini watoto wananyanyasika kwa kiwango hiki, wakaishi wapi ambako watakuwa salama, watacheza wapi ili wawe salama, vitendo kama hivi vinasababisha watoto kuchungwa sana hadi uhuru wao wa kucheza unatoweka, badilikeni Watanzania, kuweni na mioyo ya kibinadamu.