Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital
Viongozi wawili kati ya 36 wa Jumuiya za Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu Zanzibar (JUMIKI), Sheikh Farid Hadi Ahmed na Mselem Ali Mselem waliokuwa wanakabiliwa na kesi ya ugaidi wameachiwa huru.
Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Sylvester Mwakitalu amesema leo Jumatano Juni 16, 2021 kuwa amewafutia mashtaka viongozi wote wa jumuiya hiyo na kilichobaki sasa ni taratibu za kutoka gerezani.
Wawili hao ambao walikuwa mahabusu tangu mwaka 2014 pamoja na wenzao kutokana na kukabiliwa na mashtaka hayo ambayo hayana dhamana wameachiwa huru jana Jumanne Juni 15, 2021 baada ya DPP kuwafutia mashtaka yaliyokuwa yakiwakabili.
Aidha, taarifa za kuachiwa huru kwa viongozi hao zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii kuanzia jana jioni zikieleza kuwa viongozi hao wawili ndio wameachiwa huru na mmoja wa mawakili wao, Juma Nassoro amelieleza kuwa wameshapelekwa majumbani mwao.