Viongozi wa dini wameahidi kushirikiana na Serikali katika kuendelea kutoa elimu kwa waumini wao kuhusu magonjwa ya milipuko kama kipindupindu, Marburg, na mpox. Ahadi hiyo imetolewa katika mkutano uliofanyika Oktoba 26 jijini Dar es Salaam, ambapo Waziri wa Afya, Jenister Muhagama, aliwakilishwa na Naibu Waziri Dk. Godwin Mollel.
Mkutano huo ulilenga kuweka tahadhari dhidi ya magonjwa ya milipuko na kusisitiza umuhimu wa bima ya afya kwa wote.
Mwakilishi wa makanisa ya CCT, Askofu Gabriel Magwega, alisema kuwa makanisa yatashirikiana kupeleka elimu kwa waumini wao ili waweze kufahamu namna ya kujikinga na magonjwa haya.
“Tutatumia nafasi zetu kuwasaidia waumini katika nyumba za ibada ili wanapoziona dalili za magonjwa ya milipuko waweze kuchukua hatua haraka kwa kufika vituo vya afya,” alisema Askofu Magwega.
Kaimu Mufti wa Tanzania, Sheikh Ally Ngeruko, alitoa shukrani kwa Serikali kwa ushirikiano wao na viongozi wa dini. Alisema kuwa Rais Samia Suluhu Hassan anaendelea kuwa mstari wa mbele katika kuimarisha mahusiano na viongozi wa dini ili kuhakikisha mafanikio katika sekta mbalimbali za kijamii. “Hatutamuangusha Rais Samia. Tutatoa elimu ya kujikinga na magonjwa haya kwa waumini wetu katika nyumba za ibada,” aliongeza.
Sister Florida Bonifasi, mwakilishi wa Baraza la Maaskofu, alihimiza viongozi wa dini kuendelea kutoa elimu hiyo kwa kina kwa waumini wao.
Akizungumza katika mkutano huo, Dk. Mollel alisisitiza kuwa viongozi wa dini wana nafasi kubwa ya kuunganisha jamii kwa kuzingatia kuwa afya bora ni msingi wa uchumi imara. “Tunahitaji msaada wenu kwa kuwa ninyi mna nafasi ya kuunganisha jamii, na afya ikiwa imara, pia uchumi unakuwa na ustawi,” alisema Dk. Mollel.
Aliongeza kuwa Tanzania ni salama kwa sasa, lakini tahadhari inahitajika kutokana na kwamba magonjwa hayo yameathiri nchi jirani. Rais Samia ametenga fedha na vifaa vya afya mipakani ili kudhibiti maambukizi kabla ya kuingia nchini.