24.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Viongozi wa Bavicha kortini wakishtakiwa kwa uchochezi

 

Viongozi wa Chadema wakiwa mahakamani.
Viongozi wa Chadema wakiwa mahakamani.

Na RAMADHAN HASSAN, DODOMA

VIONGOZI wa Baraza la Vijana la Chama cha Demokrasia na Maendeleo Chadema (BAVICHA) jana walipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Wilaya ya Dodoma mjini wakikabiliwa na mashtaka ya  kukutwa na maandishi ya uchochezi.

Washtakiwa hao   ni Patrobas Katambi (33) mkazi wa Dar es Salaam ambaye ni Mwenyekiti wa Bavicha, Julius Mwita (30) Katibu wa Bavicha mkazi wa Dar es salaam, George Tito (28) Mwenyekiti wa baraza hilo Mkoani Mbeya.

Katika kesi hiyo upande wa mashtaka uliwakilishwa na Mawakili wa serikali, Beatrice Nsana na Lina Magoma huku    washtakiwa walikuwa wakitetewa na Mawakili watatu wa kujitegemea, Fred Kalinga, John Gigongo na Isack Mwaipopo.

Akiwasomea mashitaka mbele ya Hakimu Mkazi, James Karanyemaha, Wakili wa serikali, Lina Magoma alidai washtakiwa walikutwa na maandishi yenye lugha ya uchochezi kinyume na kifungu cha 32(2) cha sheria ya magazeti namba 229 iliyofanyiwa marejeo 2002.

Alidai Julai  9 mwaka huu katika baa ya Cape Town katika Manispaa ya Dodoma, washtakiwa walikutwa na fulana zenye maandishi ya ‘Mwalimu Nyerere Demokrasia Inanyongwa’ na  ‘Tuungane tuukatae Udikteta Uchwara’.

Washakiwa walikana tuhuma na  upande wa mashtaka uliomba tarehe ya kutajwa   shauri hilo kwa vile upelelezi unaendelea.

Hakimu Karayemaha  alisema dhamana iko wazi kwa washtakiwa kwa kila moja kuwa na wadhamini wawili wa kuaminika wenye barua kutoka kwa mtendaji kata na wawe na mali isiyohamishika yenye thamani isiyopungua Sh milioni moja.

Pia hakimu huyo aliwataka wa wadhamini kuhakikisha washtakiwa wanahudhuria mahakamani kila tarehe ya kesi na kama kuna sababu ya msingi mdhamini afike mahakamani kutoa taarifa.

Alisema mshtakiwa ambaye atafanya kosa lolote la jinai akiwa nje kwa dhamana, dhamana yake itafutwa.

Washtakiwa walitimiza mashauri yao na kuachiwa kwa dhamana.

Kesi hiyo imepangwa kutajwa tena Julai 26 mwaka huu.

Katika kesi nyingine Mjumbe wa Baraza Kuu la Chadema, Joseph Kasambala, (32) alipandishwa kizimbani kujibu tuhuma za  kutumia maandishi ya uchochezi.

Ilidaiwa na Wakili wa Serikali Beatrice Nsana kuwa Julai 9, mwaka huu katika Kituo Kikuu cha Polisii, mshtakiwa alikutwa akiwa na fulana yenye maandishi ya ‘Mwalimu Nyerere Demokrasia imenyongwa’.

Mshtakiwa alikana shtaka hilo na kuachiwa kwa dhamana na kesi hiyo itatajwa tena Julai 26, mwaka huu.

Akizungumza  nje ya mahakama, Katambi ambaye ni mwenyekiti wa Bavicha alisema   wanachokiona ni ubaguzi na ugandamizaji wa demokrasia  lakini hawatakata tamaa ya mapambano.
Alisema walikuwa wakitoka Butiama na wakiwa katika safari ya kurudi  Dar es Salaam, waliamua kukaa mahali ili kuweza kupata chakula.
“Tuliamua kupumzika Dodoma lakini tulipokuwa tunapata chakula walitokea askari na kutuzunguka walikuwa kama 30 na walitumia nguvu kutudhibiti na kutulazimisha kwenda kituo cha polisi,” alisema
lakini baadae wakapata taarifa kuwa sababu ni kuvaa fulana.

Wakati huo huo, Jeshi la Polisi Mkoani hapa limeanza kufanya doria mchana kwa kutumia magari lengo likiwa ni kupambana na wale wakaoleta vurugu   mkoani hapa.

Jana katika mitaa ya Dodoma zaidi ya askari 200 wakiwa na magari 27 wakiongozwa na Kamanda wa Polisi Mkoani hapa, Lazaro Mambosasa, walifanya doria na mazoezi kwa vitendo.

Zoezi hilo ambalo lileta taharuki kwa wananchi kutokana na askari hao kuwa na silaha, lilianza saa 1.00 asubuhi   hadi  saa 7.00 mchana  ambako askari hao walipita katika mitaa kadhaa ya mkoani hapa.

Kamanda   Mambosasa alisema hilo ni zoezi la kuuweka sawa Mkoa wa Dodoma kwa wale ambao wataleta vurugu katika siku za hivi karibuni.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles