27.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, October 16, 2024

Contact us: [email protected]

Vinara wakwepa kodi kortini

Mfanyabiashara Mohamed Mustapha (anayeongea na simu) na wenzake, wakiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam jana kukabiliana na tuhuma za kuibia Serikali kodi ya Sh milioni 7 kwa kila dakika kwa kipindi kirefu.
Mfanyabiashara Mohamed Mustapha (anayeongea na simu) na wenzake, wakiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam jana kukabiliana na tuhuma za kuibia Serikali kodi ya Sh milioni 7 kwa kila dakika kwa kipindi kirefu.

Na PATRICIA KIMELEMETA,

MFANYABIASHARA bilionea aliyetajwa na Rais John Magufuli kuwa anajipatia fedha kati ya Sh milioni saba hadi nane kwa dakika moja, Mohamed Mustafa Yusufali, maarufu kama ‘Choma’ na wenzake wanne, wamepandishwa kizimbani.

Mfanyabiashara huyo ambaye pia ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Superior Financing Solution Limited na wenzake, walipandishwa kizimbani jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam wakikabiliwa na mashtaka 199, yakiwamo ya uhujumu uchumi, utakatishaji fedha na kuisababishia Serikali hasara ya zaidi ya Sh bilioni 15.

Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Alloyscius Gonzaga Mandago, Isaack Kasanga, Taherali Sujjauddin Teharali na Mohamed Kabula.

Rais Magufuli alimtaja mfanyabishara huyo, mwishoni mwa Juni mwaka huu. Kutokana na hesabu ya Sh milioni saba anayoingiza kwa dakika moja, hutengeneza Sh milioni 420 kwa kila saa moja, sawa na Sh bilioni 5.2 kwa saa 12 na Sh trilioni 16 kwa mwezi ambazo halipi Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT).

Washtakiwa hao wanaotetewa na jopo la mawakili takribani watano, akiwamo Hudson Ndusiyepo, walisomewa mashtaka yao mbele ya Hakimu Mkazi, Huruma Shahidi na Wakili wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Leornad Swai, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Shadrack Kimaro na Pius Hilla waliokuwa wakipokezana.

Katika mashtaka hayo, makosa makubwa yalikuwa yamegawanyika katika njia tatu ambayo ni kughushi, kuwasilisha kwa taarifa za uongo, uhujumu uchumi na utakatishaji fedha.

Wakili Swai, alidai shtaka la kwanza la kughushi linamkabili Choma, ambaye anadaiwa Februari 6, 2013 jijini Dar es Salaam, akiwa na nia ya kudanganya alitengeneza nyaraka za uongo kwa ajili ya kuonyesha Kampuni ya Festive General Business Limited imesajiliwa Tanzania, taarifa ambazo si za kweli.

Inadaiwa pia Februari 12, 2013 Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam kwa nia ovu, aliwasilisha taarifa za uongo ofisi za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mkoa wa Kinondoni ili kuonyesha Kampuni ya Festive General Business imesajiliwa na imelipa kodi.

Wakili Swai, alidai mshtakiwa huyo alitenda kosa jingine la kughushi, Novemba 23, 2012 akiwa Dar es Salaam kwa lengo la kupokea ama kuwasilisha nyaraka za uongo ili kuonyesha Kampuni ya Cebers General Co. Limited inafanya kazi kihalali, ilhali ni uongo.

Kosa jingine, inadaiwa Novemba 27, 2012 Kinondoni, Dar es Salaam, kwa nia ovu aliwasilisha nyaraka hizo ofisi ya TRA wilayani humo ili kuonyesha kampuni hiyo inafanya kazi nchini kihalali na inalipa kodi.

Pia inadaiwa Choma, alitenda kosa jingine la kughushi Julai 11, 2014, akiwa Dar es Salaam kwa lengo la kupokea ama kuwasilisha nyaraka za uongo ili kuonyesha Kampuni ya Emi General Properties Limited imesajiliwa nchini na inafanya kazi kihalali, wakati ni uongo.

Alidai Julai 15, 2014  Kinondoni kwa nia ovu, Choma aliwasilisha nyaraka hizo katika ofisi za kodi ili kuonyesha kampuni ya Emi General Properties Limited ni kampuni iliyosajiliwa nchini na inafanya kazi kihalali pamoja na kulipa kodi.

Pia Choma, anadaiwa alitenda kosa jingine la kughushi Novemba 6, 2012, Dar es Salaam kwa lengo la kupokea ama kuwasilisha nyaraka za uongo ili kuonyesha Kampuni ya Fast Future Trading Limited ni kampuni iliyosajiliwa nchini na inafanya kazi kihalali, hali ya kuwa ni uongo.

Naye Wakili Kimaro, alidai Novemba 9, 2012, kwa nia ovu Choma aliwasilisha nyaraka za uongo katika ofisi ya kodi wilayani Kinondoni ili kuonyesha kampuni ya Fast Future Trading Limited ni kampuni iliyosajiliwa nchini na inafanya kazi kihalali pamoja na kulipa kodi.

Pia wakili Hilla, alisema shtaka la 198 linawakabili washtakiwa wote, ambalo ni utakatishaji fedha. Inadaiwa walilitenda kati ya Januari 2011 hadi 2016, Dar es Salaam.

Inadaiwa Choma, akiwa kama Mkurugenzi wa Kampuni ya Superior Financing Solution Limited aliwasilisha uhalisia wa ukweli, chanzo cha usafirishaji fedha Sh bilioni 1.9.

Inadaiwa kiasi hicho, walionyesha  kinakopeshwa na walizipokea fedha hizo kwa ajili ya kukopesha ambapo walionyesha kiasi hicho kililipiwa kodi.

Pia katika shtaka la 199 la uhujumu uchumi,  Wakili Hilla alidai  Choma alilitenda kati ya Januari 2008 hadi 2016, jijini Dar es Salaam.

Inadaiwa aliisababishia Serikali hasara ya Sh bilioni 15, 645,944,361 kutokana na vitendo viovu alivyovifanya.

Wakili Hilla alidai shtaka jingine linawakabili Amandago na Kasanga, ambapo inadaiwa Oktoba 30, 1995 wakiwa Dar es Salaam walighushi nyaraka za uongo kwa ajili ya kuonyesha Kampuni ya Rafiki Commodities (T) Limited ni kampuni halali iliyosajiliwa nchini, wakati ni uongo.

Kosa jingine  linawakabili Taherali na Kabula, ambao wanadaiwa Mei 16, 2011 kwa nia hovu walitumia nyaraka za uongo kwa ajili ya kuonyesha Kampuni ya Jambo Products (T) Limited kuwa ni kampuni halali iliyosajiliwa hali ya kuwa wakitambua ni uongo.

Baada ya kusomewa mashtaka hayo, Hakimu Shahidi alisema washtakiwa hawatakiwi kujibu chochote kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo.

Naye Wakili Hilla, aliieleza mahakama kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado unaendelea, hivyo aliiomba kupanga tarehe nyingine.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Julai 25, mwaka huu kwa ajili ya kutajwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles