NA EVANS MAGEGE, Dar es Salaam
VIONGOZI wa Afrika wameelezwa si wasimamizi wazuri wa maendeleo ya watu wao jambo ambalo limesababisha bara hilo kuendelea kuwa masikini na tegemezi kwa mataifa makubwa.
Hayo yalielezwa na baadhi ya marais wastaafu katika, wasomi na viongozi kutoka nchi mbalimbali za Afrika, Dar es Salaam jana, kwenye mkutano kuhusu jinsi ya kuliondoa bara hilo katika dimbwi la umaskini na unyonge.
Katika mkutano huo wa siku mbili, baadhi ya washiriki walionyesha wasiwasi kuhusu jinsi viongozi katika bara hilo wanavyosimamia rasilimali za nchi zao, ingawa wana mvuto wa siasa.
Mkutano huo uliodhaminiwa na taasisi mbalimbali, umeandaliwa na Taasisi ya Uongozi Dar es Salaam inayoongozwa na Rais mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa.
Akijibu maswali ambayo pamoja na mambo mengine yalilenga mienendo ya viongozi wa Afrika kama wanaweza kuleta mabadiliako yanayotarajiwa, Rais Mstaafu wa Afrika Kusini, Thabo Mbeki, alisema kuna wasiwasi mkubwa kuhusu viongozi wa Afrika kama wanaweza kuzikwamua nchi zao kwenye umaskini na unyonge.
“ Kuhusu ubora wa viongozi …sijui nitumie lugha gani ya kidiplomasia. Kuna wasiwasi mkubwa… hata mimi nina wasiwasi na aina ya viongozi tulionao katika siasa na hata biashara.
“Kama wangekuwa na mfumo mzuri wa mawasiliano kati yao na wananchi ungekuwa msingi bora wa kusukuma mbele gurudumu la maendeleo ya waafrika,” alisema Mbeki.
Alisema kiongozi bora ni yule anayeimarisha mawasiliano yake na wananchi kwa lengo ya kuongoza na kusimamia yale yanayotakiwa na wananchi ili kwa pamoja waweze kujenga uchumi wenye kuwaletea maendeleo.