27.1 C
Dar es Salaam
Wednesday, June 12, 2024

Contact us: [email protected]

Taharuki Operesheni Ukuta

Msemaji wa chama cha Mapinduzi (CCM), Christopher Ole Sendeka, akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi ndogo ya Makao Makuu Lumumba, Dar es Salaam jana. Kushoto ni Mkuu wa Utawala CCM Lumumba, Bakari Hamis.
Msemaji wa chama cha Mapinduzi (CCM), Christopher Ole Sendeka, akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi ndogo ya Makao Makuu Lumumba, Dar es Salaam jana. Kushoto ni Mkuu wa Utawala CCM Lumumba, Bakari Hamis.

* CCM, Jaji Mutungi wapinga tamko la Chadema

* Wasomi wahoji ziara za Rais Magufuli mikoani

Na GABRIEL MUSHI, DAR ES SALAAM

OPERESHENI Ukuta iliyotangazwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) itakayokwenda sambamba na mikutano ya hadhara na maandamano nchi nzima kuanzia Septemba Mosi, imezua taharuki miongoni mwa makundi mbalimbali nchini.

Akitangaza uamuzi huo juzi Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, alisema operesheni hiyo ina lengo la kuzuia matukio ya ukandamizaji wa haki na demokrasia aliyoda kuwa yanafanywa na Rais Dk. John Magufuli dhidi ya makundi mengine ya kisiasa na kijamii.

Mbowe alisema Kamati Kuu ya chama hicho imeainisha hoja 24 za chimbuko la Ukuta (Umoja wa Kupambana na Udikteta Tanzania), mojawapo ikiwa ni hatua ya Rais Magufuli kupiga marufuku mikutano yote ya hadhara ya vyama vya siasa hadi mwaka 2020.

Siku moja baada ya tamko hilo, Msajili wa vyama vya siasa nchini, jaji Francis Mutungi alitoa taarifa ya kulaani tamko hilo la Chadema akisema limejaa lugha ya uchochezi, kashfa, kuudhi na linahamasisha vurugu na uvunjifu wa amani.

“Nimepokea kwa masikitiko tamko la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) lililotolewa tarehe 27 Julai, 2016 kupitia vyombo vya habari, kuhusu hali ya demokrasia ya vyama vingi hapa nchini.

“Natumia fursa hii kukemea tamko hilo hadharani, kwa mujibu wa kanuni ya 6(2) ya Kanuni za Maadili ya Vyama vya Siasa. Pia nawaasa Chadema wasiendeleze tabia hii,” alisema Jaji Mutungi katika taarifa yake.

CCM yakosoa Ukuta

Kwa upande wake, Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimeitaka Chadema kuzingatia sheria kwa kutii zuio la mikutano ya hadhara lililotolewa na Jeshi la Polisi.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Msemaji wa CCM, Christopher ole Sendeka, alisema Chadema wanapotosha umma kwani Serikali haijazuia mikutano ya kikatiba kwenye majimbo yao.

“Chadema inazungumzia udikteta upi… eti wamezuiwa kufanya mikutano, huo ni uzushi kwani wabunge wake wanafanya mikutano na kuendelea na shughuli nyingine kama kawaida,” alisema Sendeka.

Wakati Sendeka akisema hivyo, wabunge wa Chadema, Wilbroad Qambalo (Karatu) na Cesilia Pareso (Viti Maalumu), walihojiwa juzi na Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha kwa kosa la kufanya mikutano na wananchi bila kibali cha polisi.

ZIARA YA JPM

Mbali na Chadema, taarifa ya ziara zinazotarajiwa kufanywa na Rais Magufuli, ambaye pia ni mwenyekiti wa CCM, Singida na Kahama mkoani Shinyanga kwa lengo la kuwashukuru wananchi kumpigia kura Oktoba mwaka jana, imepokewa kwa hisia tofauti na baadhi ya wasomi, viongozi wa dini na wananchi wa kawaida.

Baadhi ya wachambuzi wa siasa na baadhi ya viongozi wa dini waliozungumza na MTANZANIA walisema kitendo cha rais kuzuia vyama vya upinzani kufanya mikutano kimetokana na udhaifu wa katiba ya mwaka 1977 inayotumika sasa.

MCHUNGAJI LUSEKELO

Mchungaji wa Kanisa la Maombezi (GRC) lililopo Ubungo Kibangu, Dar es Salaam, Anthony Lusekelo maarufu Mzee wa Upako, alisema katiba imempa madaraka makubwa rais ambaye ndiye anateua wakuu wa vyombo vya dola.

“Leo mtawala akitaka mkutano polisi itamzuia vipi wakati mkuu wake ameteuliwa na rais? Rais pia ni Amiri Jeshi Mkuu,” alisema Mzee wa Upako wakati akizungumza na vyombo vya habari juzi.

PROFESA MPANGALA

Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Ruaha (Ruco) Iringa, Profesa Gaudence Mpangala, alisema hali hiyo inaonyesha dhahiri rais anaongoza nchi kwa hisia bila kufuata katiba, na kwamba anatamka kitu pale anapojisikia bila kuzingatia sheria inasema nini.

“Hili la kupiga marufuku mikutano ya hadhara asingelifanya kwa sababu si jambo la muhimu, ina maana hata rais mwenyewe anajifunga miguu, hatakuwa na mikutano ya hadhara, sasa anazunguka mikoani anakutana na wananchi, hii inaleta utata na hisia za ubaguzi wa kuminya vyama vya upinzani.

“Nakumbuka Bavicha (Baraza la Vijana Chadema) walitaka kuzuia mikutano ya CCM, lakini baadaye polisi wakasema iliyozuiwa ni mikutano ya hadhara si ya ndani, sasa Rais anafanya mikutano ya hadhara, hili ni tatizo.

“Rais lazima ajue anaongoza nchi yenye mfumo gani wa siasa na jamii, mfumo wetu ni wa demokrasia ya vyama vingi. Mikutano yake ina utata sambamba na tamko lake,” alisema.

PROFESA SHARIFF

Mhadhiri mstaafu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Abdul Shariff, yeye alisema anachojaribu kukifanya Rais Magufuli alikipiga marufuku yeye mwenyewe.

“Naona Jeshi la Polisi linafanya udanganyifu kuwazuia wapinzani kufanya mikutano ya siasa, hatukuzoea demokrasia… Polisi hawafanyi kazi yao, wanatumikia Serikali badala ya wananchi wote, nadhani wapinzani wangeweza kwenda mahakamani ambako nako najua watawekewa vikwazo,” alisema Profesa Shariff ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Katiba Zanzibar.

PROFESA BAREGU

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu, Agustino Mwanza (SAUT), Profesa Mwesiga Baregu, alisema inaumiza kuona Rais Magufuli anakwenda kuhutubia mkutano Kahama ambako Chadema walizuiliwa kuwashukuru waliowapigia kura.

“Sasa Rais anakwenda kuanzia eneo hilo hilo… Hiki ni kitendo cha wazi cha kuchokoza, sijui ndiyo anatangaza vita na vyama vya upinzani ama la.

“Jeshi la Polisi lilikuwa linasema mikutano ya hadhara imezuiliwa, sasa hii ya kwake ni nini?

“Ngoja tuone kama mikutano ya vyama vingine itazuiliwa, nadhani sasa hata ile mikutano ya Chadema ya Septemba Mosi inatakiwa kuanza mapema kwani mechi imeanza na kipenga kimepulizwa,” alisema Profesa Baregu.

PROFESA SHUMBUSHO

Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Profesa George Shumbusho, alisema anatarajia kuona baada ya Rais Magufuli kumaliza mikutano yake, wapinzani nao waanze yao.

“Iwapo akiwapiga tena marufuku, hakika atakuwa amekosea, na ni sawa na kuirudisha nchi katika mfumo wa chama kimoja. “Nadhani labda Rais hakueleweka ndiyo maana akaamua kufanya mikutano ya hadhara,” alisema.

Juni 23 mwaka huu, Rais Magufuli alipiga marufuku vyama kufanya mikutano ya siasa hadi mwaka 2020.

Rais Magufuli alitoa maarufuku hayo baada ya kukabidhiwa ripoti ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 na Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji mstaafu Damian Lubuva ambapo alisema chama kilichoshinda kiachwe kitekeleze yale waliyoyaahidi katika kampeni za uchaguzi huo.

Kiongozi Mkuu wa Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe, pia alizuiwa kufanya kongamano la ndani la kujadili bajeti ya 2016/2017 kwa madai hayo hayo.

Juni 7, mwaka huu Chadema walizuiwa na Jeshi la Polisi kufanya mikutano na walipolazimisha, ilisambaratishwa kwa mabomu ya machozi kwa madai kuwa hapakuwa na hali ya usalama.

Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Ernest Mangu alipotafutwa kuzungumzia zuio la mikutano kwa vyama vya siasa, simu yake ilipokewa na mlinzi wake ambaye alisema bosi wake alikuwa kwenye kikao wilayani Kahama.

“Kama ni suala la kikazi nakushauri umtafute  Msemaji wa jeshi, Advera Senso,” alisema Mangu.

Senso alipotakiwa kuzungumzia suala hilo, alisema alikuwa na kikao cha dharura na kuomba apelekewe maswali ofisini leo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles