27.5 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

‘Zitengwe fedha upimaji wa sampuli kukabili magonjwa ya dharura’

Wauguzi wa Idara ya Magonjwa ya Dharura (EMD) katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), wakimuhudumia mgonjwa.
Wauguzi wa Idara ya Magonjwa ya Dharura (EMD) katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), wakimuhudumia mgonjwa.

NA CHRISTINA GAULUHANGA, DAR ES SALAAM

SERIKALI ilianzisha Wakala wa Mkemia Mkuu wa Serikali kwa lengo la kuchunguza sampuli mbalimbali za viwandani na majumbani na kuhakikisha kunakuwepo na matumizi salama ya kemikali.

Tangu kuanzishwa kwa wakala huo kumekuwa na changamoto mbalimbali ikiwemo uhaba wa vitendea kazi bora na vya kisasa pamoja na ukosefu wa bajeti.

Mkemia Mkuu wa Serikali, Profesa Samwel Manyele, anasema taasisi hiyo ina wachunguzi ambao wamesajiliwa kufanya majukumu katika vitengo mbalimbali.

Anataja vitengo vilivyopo katika ofisi hiyo ni pamoja na ubora wa mifumo, Tehama, ununuzi, sheria na ukaguzi wa ndani ambapo wana ofisi katika kanda mbalimbali ambao hushirikiana na wafanyakazi hao kukusanya taarifa na kuziwasilisha na kuhakikisha kesi za jinai zinaendeshwa sawa na kufanya ukaguzi wa kemikali.

Mkemia Mkuu ni msimamizi wa wachunguzi wa serikali ambaye anasimamia uadilifu, maadili na sifa kuhakikisha zinasimamiwa ipasavyo.

Mkemia Mkuu ndiye kioo cha taasisi, msajili wa kemikali nchini, mdhibiti wa vinasaba vya watanzania, mshauri wa serikali katika masuala ya kemikali, chombo kinachokutanisha Tanzania na masuala ya kemilikali na mtaalamu mshauri  Umoja wa Mataifa kuhusu masuala ya kemilikali.

MAFANIKIO

Anasema wamefanikiwa kufanya utambuzi wa miili, uchunguzi wa jinai hasa katika mashauri yanayopelekwa mahakamani, sampuli za dawa za kulevya ambapo vielelezo 20,800 vimechunguzwa, ukarabati wa maabara, mifumo uendeshaji sayansi jinai imeboreshwa na wamefungua kitengo cha uratibu matukio ya sumu.

Anasema huduma ya vinasaba sayansi ililenga kutatua kesi za jinai ambapo wamejitahidi kuboresha mifumo ili kupatikana kwa majibu sahihi na kwa wakati.

Pia anasema bidhaa zinazopimwa na kupata ithibati ya maabara ya mkemia mkuu wa serikali nchini, hivi sasa zitakuwa na fursa ya kupata soko zuri ndani na nje ya nchi kutokana na maabara hiyo kupata hati ya ubora wa Kimataiga (ISO).

Pia anasema wametengeneza rejista upya na kuorodhesha wadau wote ambao hadi sasa wana wadau 4,000.

Profesa Manyela anasema mipaka yote nchini sasa wanafanya ukaguzi ambapo idadi ya wanaokaguliwa imeongezeka na maabara imeboreshwa inapokea sampuli tofauti.

Anasema wamekuwa wakifanya ukaguzi wa kemilikali zinazoingia nchini na kutoka ndani ya nchi kwa ajili ya usalama wa raia na serikali kwa ujumla.

CHANGAMOTO

Anasema wanakabiliwa na uhaba wa fedha hivyo kulazimika kuendesha shughuli mbalimbali kwa kutumia mapato yao ya ndani.

“Wateja wetu wakubwa ni Serikali kwakuwa tumekuwa tukifanya shughuli za upimaji sampuli mbalimbali kwa ajili ya vielelezo mahakamani jambo ambalo linatuwia vigumu kufanya shughuli kwa wakati,”anasema Profesa Manyele.

Anasema wamekuwa wakipokea malalamiko kutoka kwa wateja ambao wamekuwa wakishinikiza vipimo vyao mbalimbali kufanyika uchunguzi kwa haraka wakati vingine vinahitaji utaalamu wa kina.

Profesa Manyele anasema imefika wakati wananchi waone haja ya kufika katika ofisi zao ili kujionea shughuli mbalimbali wazifanyazo na changamoto wanazokabiliana nazo.

Anasema malengo yao ni kuhakikisha wanafungua ofisi nyingi mikoani ili waweze kutoa huduma za karibu kwa wananchi wa mikoa yote.

“Kwa sasa tumejipanga kukabiliana na changamoto hasa zile za kusafiri kwenda mikoani hivyo tutaanzisha matawi huko ili kurahisisha shughuli zetu,”anasema Profesa Manyele.

Anaiomba Serikali iendelee kuiwezesha ofisi hiyo kwakuwa imekuwa ikifanya shughuli muhimu za jamii ambazo zinahitaji mitambo ya kisasa na umakini.

Anasema uchakavu wa mitambo inaweza ikawa kikwazo cha utendaji kazi na kusababisha hata majibu ya vipimo kuchelewa kupatikana kwa wakati.

Pia anasema ipo haja ya kuangalia namna ofisi hiyo itakavyoweza kupata fedha za dharura ili waweze kukabiliana upimaji wa sampuli pindi panapotokea magonjwa ya dharura au mlipuko.

Profesa Manyele anasema sheria ya manunuzi nayo imekuwa kikwazo kwao hasa katika kununua kifaa kilichoharibika hivyo kunahitajika marekebisho ya sheria hiyo.

‘’Sheria ya manunuzi wakati fulani nayo imekuwa ikitubana kwa sababu kifaa kinapoharibika huwa tunahitaji kununua haraka na kukifunga ili tuendelee na kazi lakini kutokana na mchakato wa sheria hiyo tunajikuta tunachukua muda mrefu,”anasema Profesa Manyele.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles