NA MARKUS MPANGALA
VIONGOZI kadhaa barani Afrika wameondolewa madarakani kwa nguvu baada ya kung’ang’ania madarakani kinyume na sheria ama kwa kusigina Katiba.
Historia hiyo imemkumba Rais wa Algeria Abdelaziz Bouteflika (82), ambaye ametawala madarakani kwa kipindi cha miaka 20.
Baadhi ya viongozi waliopitia misukosuko ya kiutawala ni pamoja na aliyekuwa Rais wa Libya Muammar Gaddafi ambaye alitawala kwa miaka 42.Aling’olewa madarakani baada ya kuzuka machafuko nchini humo.
Mwingine ni Ben Zine El Abidine Ben Ali anajulikana zaidi kama Ben Ali, akiwa Rais wa Tunisia alilazimika kung’atuka madarakani mwaka 2011 aliongoza nchi hiyo tangu mwaka 1987. Aliyekuwa Rais wa Zimbabwe, Robert Mugabe, licha ya umri wake kusonga aliapa kutotoka madarakani, hali iliyosababisha maandamano ya wananchi nchini humo, hivyo kulazimika kujiuzulu.
Aidha, aliyekuwa Rais wa Misri Hosni Mubarak aliyetawala tangu mwaka 1981 hadi 2011 aliondolewa madarakani kwa nguvu ya umma, kwa kile kilichoitwa vuguvugu la mabadiliko ya kisiasa katika nchi za Kiarabu (Arab Spring),
Tunisia na Misri zilikuwa nchi zilizokumbwa na vuguvugu hilo, huku Algeria na mataifa mengine ya kiarabu yakiepuka.
Hata hivyo vuguvugu lile lililoshamiri mwaka 2011, liliiepusha Algeria sasa limeikumba nchi hiyo na kumtimua madarakani Rais Bouteflika.
Maandamano yasiyo na kikomo mitaani ya wananchi wa kawaida pamoja na chama cha wanasheria cha Algeria nacho kiliingia mtaani kuunga mkono juhudi hizo, na hekaheka nyingine katika miji mbalimbali nchini humo zilikuwa na lengo la kuhakikisha kiongozi huyo anang’atuka katika siasa kwa shinikizo.
Wananchi walikubali kupigwa, kutishwa na vyombo vya dola, hata hivyo hakuna kilichowarudisha nyuma kumshinikiza Bouteflika kuondoka madarakani. Sababu ya wananchi hao kutaka hilo ni uamuzi wa rais huyo kutaka kugombea muhula mwigine wa tano katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Aprili 8, mwaka huu.
Mashinikizo hayo yalimfika shingoni. Hatimaye Bouteflika, alitangaza kusogeza mbele uchaguzi wa urais na kusema kuwa hatagombea tena muhula wa tano.
Kama nilivyosema awali, nia ya kugombea kwake ilizuia maandamano ya nchi nzima kwa wiki kadhaa sasa, hilo pekee limedhihirisha nguvu ya umma ilivyoweza kuangusha utawala wa chuma uliodumu miaka mingi nchini humo.
Rais huyo ameliongoza Taifa la Algeria kwa kipindi cha miaka 20 sasa, lakini kwa muda mrefu hakuwa anaonekana katika maeneo ya wazi, kutokana na ugonjwa wa kiharusi alioupata mwaka 2013.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa niaba ya Bouteflika mapema wiki hii ilisema rais huyo hakutangaza tarehe mpya ya uchaguzi, lakini amekuwa akitarajiwa kufanya mabadiliko katika baraza la mawaziri. Hakukua na tamko kuwa rais huyo atajiuzulu kabla ya tarehe mpya ya uchaguzi mkuu.
Katika hatua nyingine nguvu ya umma haikuishia kwa Rais Bouteflika bali ilielekezwa kwa Waziri Mkuu wa Algeria, Ahmed Ouyahia alitangaza kujiuzulu nafasi yake kuchukuliwa na waziri wa mambo ya ndani Noureddine Bedoui ambaye anakabiliwa na kibarua kigumu cha kuunda serikali mpya ambayo itakuwa na kazi ya kuwavutia wananchi ili kuamini itaweza kuhudumu vizuri pamoja na kusonga mbele baada ya kipindi cha utawala wa Bouteflika.
Katika hotuba hiyo iliyotolewa kwa niaba ya Rais Bouteflika amesema, “Hakutakuwa na muhula wa tano kwa Rais Bouteflika, hakuna maswali tena wala wasiwasi katika hilo, ukizingatia hali yangu ya kiafya, na umri wangu, kazi yangu ya mwisho kwa watu wa Algeria ni kuhakikisha wanapata uongozi mpya,”
Awali kabla ya taarifa ya kujiuzulu kwake, wakati wananchi wakiandamana alisema mpango wake katika mhula wa tano ni kuhakikisha hakai sana madarakani, atajiuzulu. Hata hivyo tamko hilo la awali halikuwafanya wananchi warudi nyuma na kuamini atatekeleza, badala yake maanadamano hayakukoma hadi pale lilipokuja tamko la pili.
Tamko la kutogombea kwa Rais Bouteflika, lilipongezwa na mataifa mengine, ikiwemo Ufaransa, ambapo Waziri wa Mambo ya Nje, Jean-Yves Le Drian, aliita uamuzi huo kama taarifa yenye kuchochea furaha kubwa nchini Ufaransa, na serikali yao ilifurahishwa na uamuzi huo na kuwa ni wakati wa kupata serikali mpya ambayo itakuwa imekubaliwa na kukidhi matakwa ya wananchi.
Kwa mara ya mwisho Bouteflika alionekana hadharani wakati akitoa hotuba kwa umma mwaka 2014. Hotuba hiyo ilikuwa na lengo la kutoa shukrani kwa raia wa Algeria kwa kuamini utawala wake baada ya kushinda uchaguzi uliokuwa umetangulia.
Katika hotuba hiyo aliahidi kutekeleza suala la mgawanyo wa madaraka, kuupa nguvu upinzani na kuhakikisha haki za raia zinafuatwa. Baadhi waliona kuwa hii ni ishara ya mabadiliko ya sera katika uongozi, lakini hakukuwa na ushahidi wa kuonekana kwake kwa muda mrefu.
Raia wa nchi hiyo wamekuwa wakibahatika kumuona mara chache kwenye televisheni akisalimiana na ujumbe kutoka nchi za kigeni wanaofika nchini Algeria kwa shughuli mbalimbali za kiserikali.
Au kumuona kwenye ufunguzi wa mkutano mwaka 2016, akionekana amekaa kwenye kiti cha magurudumu, akionekana dhaifu, mwenye uchovu lakini mwenye tahadhari.
Mpaka mwaka 2018, ikawa wazi kuwa Chama chake kimempendekeza kuwania tena uchaguzi wa mwaka huu. Rais huyo alikuwa kwenye ufunguzi wa msikiti na vituo vya treni za umeme katika mji mkuu wa nchi hiyo wa Algeria. Wiki chache baadaye alikuwa kwenye ziara kutazama ujenzi wa msikiti mkubwa wa tatu duniani uliogharimu dola za Marekani bilioni mbili.
Kiongozi huyo alishinda uchaguzi wa mwaka 2014, ingawa hakuwa na kampeni zozote, mpaka sasa hana wapinzani wenye nguvu. Swali kubwa linaloulizwa ni kwanini sasa chama tawala na upinzani umeshindwa kupata wagombea wanaofaa kuongoza taifa hilo?
Vyama vya upinzani nchini humo vina historia ya kugawanyika. Chama tawala National Liberation Front kimetawala tangu Algeria ilipopata uhuru kutoka Ufaransa mwaka 1962 baada ya miaka saba ya vita vya nchini humo. Wachambuzi wa siasa za nchini Algeria wanaona kuwa vijana wenye nguvu wananyang’anywa nguvu zao za uongozi na wazee. Jambo hilo pamoja na mengine yamechochea maandamano ya kila kundi, kuanzia wafanyabiashara, wamachinga, wananchi wa kawaida hadi wanazuoni. Wote walimpinga na sasa amekiri kuwa afya yake ni taabani na anahitaji kupumzika. Hakika ni nguvu ya umma ambayo inatakiwa kutoa somo kwa wananchi wa nchi za Afrika mashariki na viongozi