26.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

Netanyahu kuangukia Ikulu au jela?

HASSAN DAUDI NA MITANDAO

UMEBAKI mwezi mmoja kabla ya Israel kuingia katika Uchaguzi Mkuu, Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Benjamin Netanyahu, ameonyesha nia ya kuwania awamu ya tano madarakani.

Netanyahu, ‘kichwa’ cha masuala ya uchumi, ambaye amekuwa akiushikilia wadhifa huo wa Waziri Mkuu tangu mwaka 2009, ni mbunge na Mwenyekiti wa Chama cha Likud.

Ukikiweka kando chama cha Gantz, Blue and White kinachoongozwa na aliyewahi kuwa Mkuu wa Majeshi, Benny Gantz, ni tishio kwa Netanyahu kushinda mwaka huu.

Hata hivyo, wakati uchaguzi huo ambao unatarajiwa kufanyika Aprili 9, mwaka huu, kiongozi huyo anakabiliwa na kashfa nzito ya matumizi mabaya ya madaraka kwa masilahi yake, hivyo wengi wanatabiri kinaweza kuwa kizingiti kwake kurudi madarakani.

Balaa lililomkumba Netanyahu lilianzia Februari 28, mwaka huu, pale Mwanasheria Mkuu wa Israel, Avichai Mandelblit, alipotangaza wazi kuwa anataka kumfungulia mashitaka kiongozi huyo.

Ikumbukwe kuwa ni Netanyahu ndiye aliyemteua Mandelblit kushika wadhifa huo, hivyo basi, huenda wengine wangefananisha na msemo wa ‘mbwa aliyemng’ata mfugaji wake’.

Mandelblit aliahidi kumfikisha mbele ya sheria Netanyahu, akidai Waziri Mkuu huyo ni fisadi, kwamba uhusiano wake na wafanyabiashara wakubwa si wenye masilahi ya Israel. 

Mwanasheria huyo aliongeza kuwa Netanyahu amekuwa akitumia rasilimali za Israel kuwaneemesha wafanyabiashara matajiri, ambao kwa bahati mbaya humpa zawadi za ‘kipuuzi’ kama pombe na sigara za bei kali.

Ikaelezwa kuwa kuanzia mwaka 2007 hadi 2016, alikuwa amepokea zawadi zenye thamani ya Dola 268,200  za Marekani (ni sawa na Sh milioni 600 za Tanzania) kutoka kwa mfanyabiashara wa Israeli, Arnon Milchan.

“Anakumbana na presha kubwa,” anasema mwandishi wa habari wa gazeti la Haaretz, Anshel Pfeffer, anayeongeza kuwa kashfa hiyo inamchafua Netanyahu katika ulingo wa siasa.

Kashfa nyingine iliyoibuliwa na Mandelblit ni ile aliyomtaja Netanyahu kukutana na kufanya mazungumzo ya siri na Arnon Mozes, mhariri wa muda mrefu wa moja kati ya magazeti yenye wasomaji wengi Israek, Yedioth Ahronoth.

Kipindi fulani, mkewe aitwaye Sara, alihojiwa na polisi juu ya matumizi mkubwa wa fedha za umma, wakati mkewe huyo ‘alipotumbua’ Dola za Marekani 100,000 (zaidi ya Sh milioni 230).

Wanasheria wake walikanusha hilo lakini baadaye ziliibuka taarifa kuwa aliwaambia ni bora aende jela kuliko kukubali kosa na kuutia aibu utawala wa mumewe, Netanyahu.

Akilisimulia hilo, Mandelblit alisema mwanamke huyo, Sara, alidanganya kuwa hakuwa na mpishi aliyeajiriwa na serikali ili aweze kutumia mamilioni kwa kisingizio cha kununua vyakula katika migahawa.

Licha ya Netanyahu kuzikanusha kashfa zinazomkabili, ilifichuliwa kuwa Waziri Mkuu huyo aliahidi ‘zawadi’ kwa chombo hicho cha habari endapo kingekuwa kikiandika mazuri yake tu.

“Hali inavyozidi kuwa hivi, ndivyo anavyokuwa na presha ya kisiasa, hasa kutokana na uwepo wa Chama cha Gantz na hata wapinzani wake ndani ya Chama cha Likud.”

Pia, bado kuna mpinzani wake wa muda mrefu, Gantz, anayekiongoza Chama cha Blue and White, ambaye mara nyingi amekuwa akiahidi kuondoa uchafu uliojaa serikalini.

Wakati wengi wakisubiri kuona Netanyahu akifunguliwa mashitaka, hivi karibuni, mamlaka za Israel ziliweka wazi kuwa hazitafanya hivyo hadi pale Uchaguzi Mkuu utakapomalizika.

Katika hatua nyingine, uamuzi huo, ambao Mandelblit amekubaliana nao, umeonyooshewa kidole, ukitajwa kuwa na lengo la kumwokoa Netanyahu kwa kuwa haitakuwa rahisi kumfungulia mashitaka atakaporudi madarakani.

Waziri wa Fedha wa zamani wa Israel, Yair Lapid, ameliona hilo na hivi karibuni alimjia juu Netanyahu akisema kiongozi huyo anataka kuutumia Uchaguzi Mkuu wa mwezi ujao kukwepa uchunguzi dhidi machafu yake.

Lapid ana shaka kuwa huenda Netanyahu amepanga kufanya figisu katika matokeo ili atakaposhinda, aonekane kuwa bado ni kipenzi cha wananchi wa Israel, hivyo madai ya rushwa yaliyopo ni chuki tu dhidi yake.

“Anataka akili zielekezwe kwenye Uchaguzi na si uchunguzi, akijua wazi atakaposhinda, atakuwa na uwezo wa kuzima kesi zilizopo,” alisema Lapid.

Anachokijua Lapid ni kwamba Netanyahu hawezi kukubali kuondoka madarakani, akifahamu wazi kuwa kufanya hivyo kutamweka kwenye hatari ya kuishia gerezani.

“Madaraka yatampa uwezo wa kujiokoa. Endapo atatoka madarakani, ataishia gerezani tu.” alisema Lapid

Hivyo basi, endapo atabwagwa katika uchaguzi mkuu wa mwezi ujao na kwenda mahakamani na kisha kwenda kutumikia kifungo, Netanyahu atakuwa ameingia katika orodha ndefu ya vigogo wa Serikali ya Israel waliowahi kuyaonja machungu ya kuyatumia vibaya madaraka.

Haijasahaulika kuwa ilikuwa hivyo kwa Ehud Olmert aliyekuwa Waziri Mkuu wa nchi hiyo kuanzia mwaka 2006 hadi 2009, ambapo kwa kosa kama hilo la rushwa, alihukumiwa kifungo cha miaka sita gerezani, ingawa baadaye adhabu hiyo ilipunguzwa na kubaki miezi 18.

Ni kwa maana hiyo, Netanyahu atakuwa Waziri Mkuu wa pili wa Israel kuishi maisha ya jela, akimfuata Olmert aliyeingia mwaka 2016.

Hiyo ilikuwa ni mara ya pili kwa Olmert kuingia gerezani kwani mwaka 2014 alihukumiwa miaka sita, ambayo ilipungua na kubaki miezi 18, kwa kosa la rushwa lakini kipindi hicho alikuwa Meya wa Jerusalem.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles