28.2 C
Dar es Salaam
Friday, November 15, 2024

Contact us: [email protected]

Vijana pimeni DNA kabla ya kufunga ndoa – Ummy Mwalimu

Na AVELINE KITOMARY

SELIMUNDU (sickle cell) ni ugonjwa unaorithiwa kutoka kwa kizazi kimoja hadi kingine. Hutokana na tatizo kwenye chembechembe nyekundu za damu.
Ugonjwa huu unaendelea kuongezeka hapa nchini kutokana na wazazi wa pande zote mbili kushindwa kupima vinasaba (DNA), kabla ya kuoana au kuzaa.
Ikiwa wazazi wote wawili wanachembechembe za sickle cell wanaweza kuzaa mtoto mwenye ugonjwa huo.
Kila ifikapo Juni 19 kwa kila mwaka, Tanzania hujumuika na nchi nyingine duniani katika kuadhimisha siku ya selimundu.
Lengo la maadhimisho hayo ni kuongeza uelewa kwa jamii kuhusu ugonjwa wa Sickle Cell ili kupunguza madhara yatokanayo na ugonjwa huu.
Katika maadhimisho ya mwaka huu, kauli mbiu ni ‘Huduma bora ya Sickle Cell kwa kila mhitaji’ sambamba na kauli mbiu hiyo ujumbe mahususi katika kuadhimisha siku hiyo ni “Chukua hatua panua uwigo.”

Kauli mbiu hiyo pamoja na ujumbe mahususi unalenga kuwashirikisha wadau katika utoaji wa huduma za Sickle cell katika vituo vyote ya tiba ili kumfikia kila mtanzania mwenye kuhitaji.

HALI ILIVYO NCHINI
Takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO), zinaonyesha kuwa zaidi ya watoto 1,000 duniani huzaliwa wakiwa na selimundu kila siku.

Takwimu zilizotolewa na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsi Wazee na Watoto zinaonyesha kuwa hapa nchini watoto takribani 11,000 huzaliwa na ugonjwa wa sickle cell kila mwaka ambao ni sawa na watoto wanane kati ya watoto 1,000 wanaozaliwa.

Akizungumza katika uzinduzi wa mwongozo wa matibabu ya sickle cell nchini, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, anasema takwimu hizo zinaifanya Tanzania kuwa nchi ya nne duniani kwa kuwa na wagonjwa wengi wa sickle cell huku nchi inayoongoza duniani ikiwa ni Nigeria.

“Katika nchi hiyo watoto 20 hadi 30 kati ya 1,000 huzaliwa na tatizo hilo, nchi inayofuata ni India ambayo inaonyesha kuwa watoto 14 kati ya 1,000 wanaozaliwa na tatizo hilo, na nchi ya tatu ni DRC Kongo ambapo watoto 13 kati ya 1,000 huzaliwa na selimundu kila mwaka,” anaeleza Ummy.

Anasema kwa takwimu za Wizara ya Afya, sasa Tanzania ina wagonjwa zaidi ya 200,000 wenye sickle cell, takribani watoto saba kati ya 100 wenye umri wa chini ya miaka mitano hufariki nchini kutokana na ugonjwa huo.

“Takwimu zinaonyesha kuwa asilimia 15 hadi 20 ya Watanzania 100, wana vinasaba vya ugonjwa huu, yaani wana uwezekano wa kupata watoto wenye ugonjwa huo iwapo watakuwa na wenza wenye vinasaba vya sickle cell,” anasema.

HATUA ZINAZOCHUKULIWA

Waziri Ummy anasema ili kuhakikisha kupunguza madhara na vifo kwa watoto wanaozaliwa na sickle cell, Serikali imechukua hatua muhimu kama kujumuisha ugonjwa huo katika Mpango Mkakati wa Taifa wa pili wa magonjwa yasiyoambukizwa mwaka 2016 hadi 2020.

Anasema mwaka 2017 walianzisha kikosi kazi cha Taifa cha sickle cell ambapo pia wakati wa kuzindua Mpango wa Taifa wa kuzuia na kudhibiti magonjwa yasiyoambukizwa Novemba, 2019, ugonjwa huo ulijumuishwa.

“Mafanikio yaliyopatikana kutokana na hatua hizi muhimu ni ongezeko la wagonjwa wanaotibiwa katika vituo vya tiba kutoka 32,457 mwaka 2015 hadi kufikia wagonjwa 61,212 mwaka 2019, sawa na ongezeko la asilimia 88.6.

“Huduma za maabara na utambuzi wa ugonjwa wa sickle cell zimeboreshwa ambapo mwaka 2015 ni Hospitali ya Muhimbili pekee iliyokuwa na uwezo wa kuthibitisha ugonjwa wa sickle cell kwa kutumia ‘HB Eletrophoresis.’

Lakini kwa mwaka huu, kipimo hiki kinafanywa na hospitali sita zikijumuisha Bugando, Mbeya, hospitali za binafsi – St. Gemma, Aga Khan na Regency,” anabinisha.

Anasema hivi karibuni wanatarajia kuanza kutoa huduma za vipimo vya papo kwa hapo (Rapid Diagnostic Tests) katika hospitali zote za mikoa, wilaya na vituo vya afya.

“Dawa muhimu zinazotumika kutibu ugonjwa wa Sickle cell zimeingizwa katika mwongozo wa tiba wa taifa (Standard Treatment Guideline).

“Pia serikali ipo katika hatua za mwisho za kuanzisha huduma ya upandikizaji wa uloto (bone marrow transplant) katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, pia kuna kitabu maalum kidogo (pasipoti) kwa wagonjwa wa sickle cell kwa ajili ya kutunza kumbukumbu za wagonjwa hao,” anafafanunua Ummy.

Ummy anaeleza kuwa mafanikio hayo yanatokana na uboreshwaji wa huduma za afya katika ngazi mbalimbali.

ATAKA VIJANA KUPIMA

Waziri Ummy anasema ugonjwa huo unaweza kuzuilika endapo vijana watapima vinasaba (NDA) ili kujua kama wanachembechembe za sickle cell kabla ya kuoana au kuzaa.

Anasema hali hiyo itawashaidia kuepuka kuzaa watoto wenye selimundu.

“Tumeendelea kutoa elimu ya kupunguza visa vya sickle cell kwa vijana kwa kuzingatia kupima kabla ya kuingia kwenye uhusiano, naendelea kuwashauri vijana walizingatie hili.

“Pia tunaendelea kufanya tafiti za sickle cell nchini zitakazotusaidia kufanya uamuzi wa kisera wenye uthibitisho wa kisayansi unaoendana na mahitaji ya nchi,” anaeleza.

Waziri Ummy anasema ili kuhakikisha upatikanaji wa huduma za afya hususan katika eneo la ugonjwa huo, anawataka waganga wakuu wa mikoa kuhakikisha wanasimamia huduma za wagonjwa wa hao zinazotolewa hospitalini na kwenye vituo vya afya vilivyopo katika mikoa wanayoisimamia.

“Pia wanatakiwa kuanzisha kliniki maalum za sickle cell katika hospitali za rufaa za mikoa na wilaya, pia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, pamoja na Ofisi ya Rais-TAMISEMI itoe elimu ya afya shuleni, vyuoni na jamii kwa ujumla kuhusiana na tatizo hili.

“Kwa watendaji wa wizara, wahakikishe wanasambaza mwongozo wa ugonjwa huo uliozinduliwa katika mikoa yote ili kuhakikisha mipango mizuri iliyomo humo inatekelezwa,” anaagiza.

DALILI ZA SELIMUNDU

Daktari Bingwaa wa Magonjwa ya Damu kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Dk. Elineema Maeda, anasema dalili za ugonjwa huo huanza tangu mtoto akiwa na miezi mitatu hadi sita, ambapo wakati huo huanza kupata maumivu ya viungo.

Anataja dalili zingine kuwa ni kuvimba miguu, mikono, kupungukiwa na damu na kuwa mweupe machoni na mdomoni.

Anasema wakati mwingine anaweza kuwa na njano machoni na watu kudhani kuwa anasumbuliwa na homa ya ini.

Anasema uvimbe hutokea pale ambapo chembechembe zinakuwa hazisogei hivyo damu kupata shida kupita hatimaye chembechembe nyekundu kupasuka na nyongo hutoka.

“Nyongo ikiwa nyingi ini linazidiwa ndio maana watu wa aina hii utakuta wanapata rangi ya njano mdomoni, machoni na vidoleni. Hii inaweza kusababisha mtoto akawa na homa ya mara kwa mara na anapoendelea kukua dalili zinaongezeka.

“Hali hiyo husababisha watoto kupata kiharusi, damu kupungua na kupatwa na vidonda visivyopona,” anafafanua Dk. Maeda.

TIBA YAKE
Dk. Maeda anasema ugonjwa huo unatiba lakini haiponeshi kwa sababu tatizo linakuwa kwenye vinasaba (DNA).

“Mgonjwa hawezi kupona kabisa hivyo, mtoto mwenye tatizo hilo awahishwe hospitali haraka akapate chanjo inaweza kumsaidia kurefusha maisha yake na kumkinga dhidi ya maambukizi ya magonjwa mengine,” anasema.

Anasema mtoto anatakiwa kupata chanjo ya pevic au penisuling kwaajili ya kumlinda na magonjwa ambukizi kwa sababu wanapokuwa na ugonjwa wa sickle cell kinga zao huwa ziko chini,” anabainisha.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles