26.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 17, 2024

Contact us: [email protected]

Vijana Kipunguni waelimishwa faida za kuwalinda dada zao wasikeketwe

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

VIJANA 100 na watoto 50 kutoka maeneo mbalimbali ya Kata ya Kipunguni wamepatiwa mafunzo ya namna ya kubaini viashiria vya ukeketaji ili kuwalinda dada zao wasikeketwe.

Mafunzo hayo yametolewa na Shirika lisilo la kiserikali la Sauti ya Jamii Kipunguni ambalo linaendesha kampeni ya kuzuia ukeketaji katika Kata ya Kipunguni.

Akizungumza wakati wa mafunzo hayo Mkurugenzi wa Sauti ya Jamii Kipunguni, Selemani Bishagazi, amesema lengo ni kuwawezesha vijana na watoto wakiona kuna dalili za ukeketaji katika maeneo yao watoe taarifa.

“Mfano kwenye kabila la Kikurya nguvu kubwa anayo mtoto wa kiume, anaweza akaamua dada yake aolewe kwa mahari kiasi gani kwa sababu ndiyo inayotumika pindi yeye atakapotaka kuoa.

“Kwa utamaduni wao wasichana waliokeketwa hulipiwa mahari kubwa ndiyo maana tumeamua kuwaelimisha watambue madhara ya ukeketaji na madhara ya wao kubweteka kusubiri dada aolewe ndiyo wapate mahari,” amesema Bishagazi.

Kwa mujibu wa mkurugenzi huyo mwaka 2014 waliwaokoa watoto 19, 2016 (46), 2018 (34) na 2020 (9).

Vijana kutoka maeneo mbalimbali ya Kata ya Kipunguni wakifuatilia mafunzo ya namna ya kuepuka vitendo vya ukatili hasa ukeketaji ambayo yalitolewa na Shirika lisilokuwa la kiserikali la Sauti ya Jamii Kipunguni.

“Mangariba tuliowaelimisha wakaacha ni wawili na sasa hivi tunashirikiana nao kutoa elimu pia ni wakulima wa mboga,” amesema.

Naye Mwenyekiti wa Sauti ya Jamii Kipunguni, Fatma Abdulrahman, amesema wanataka mwaka huu kusiwe na kesi za ukeketaji na kwamba wanawahamasisha vijana waimbe nyimbo zinazozuia ukeketaji badala ya zile zinazochangia mila hiyo potofu.

“Kulingana na kaulimbiu ya mwaka huu ya Siku 16 za Kupinga Ukatili wananchi wenyewe ndiyo wanabeba jukumu hivyo, tumekaa na wanajamii mmoja mmoja, vijana na watoto ili wajue namna ya kuripoti ama kugundua dalili za maandalizi ya kukeketwa,” amesema Fatma.

Shirika hilo linawahamasisha vijana hao kujiunga na timu za mpira za mtaa ili iwe rahisi kuwafikia na kuendelea kuwapa elimu ili kukomesha vitendo vya ukatili ukiwemo ukeketaji.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles