24.8 C
Dar es Salaam
Wednesday, October 2, 2024

Contact us: [email protected]

Vijana 181 wenye ulemavu wa akili wanufaika ufundi stadi

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Vijana 181 wenye ulemavu wa akili kutoka Manispaa ya Morogoro na Halmashauri ya Mji Mdogo Ifakara wamepatiwa mafunzo ya ufundi stadi kuwawezesha kuondokana na utegemezi na kujikwamua kiuchumi.

Mafunzo hayo yametolewa kwa ushirikiano wa Shirika lisilokuwa la kiserikali linaloshughulikia maendeleo ya wanawake na vijana (Mwayodeo) la mkoani Morogoro na Taasisi ya Vaasa kupitia ufadhili wa Wizara ya Mambo ya Nje nchini Finland.

Akizungumza Oktoba Mosi,2024 jijini Dar es Salaam wakati wa kuwasilisha matokeo ya mradi wa Kukuza Stadi za Ufundi kwa vijana wenye ulemavu wa akili, Mkurugenzi wa Mwayodeo, Venance Mlali, amesema mradi huo wa miaka minne umeshirikisha vijana wenye umri wa miaka 18 hadi 30.

Mkazi wa Manispaa ya Morogoro, Siasa Swamlo, akizungumza jinsi mwanawe alivyonufaika kupitia mradi wa Kukuza Stadi za Ufundi kwa vijana wenye ulemavu wa akili.

Amesema vijana hao walipatiwa mafunzo ya miezi mitatu katika fani za upishi, useremala, ushonaji, ujenzi, ufundi bomba, useketaji nguo na kutunza bustani yametolewa kupitia vyuo vya Veta Kihonda, Bigwa, Social Centre, Ifakara.

“Lengo kubwa tunataka kijana akipata stadi aweze kuzitumia kuboresha maisha yake, wengi wamefanikiwa kujiajiri na wengine wameajiriwa katika maeneo mbalimbali. Kuna binti kutoka Ifakara ameajiriwa kwenye mgahawa Sumbawanga, wako ambao wamechukuliwa na mafundi bomba na wengine wanajenga.

“Binti mwingine aliyejifunza ushonaji Veta Kihonda ameajiriwa na Kiwanda cha Mazava Morogoro na anafanya vizuri, wengine waliojifunza ushonaji baadhi yao tumewapa vyerehani wanashona vizuri na wengine wameajiriwa na mafundi, wako ambao wanatengeneza chipsi wanauza kwahiyo kila mtu ana kitu cha kufanya,” amesema Mlali.

Hata hivyo amesema muda wa miezi mitatu hautoshi kwa kuwa vijana hao huchukua muda mrefu kujifunza na kuelewa kutokana na changamoto waliyonayo na kushauri uongezwe.

Amesema pia katika vyuo vingi vya ufundi bado kuna changamoto ya walimu wabobezi wa kufundisha watoto wenye ulemavu wa akili ambapo mwaka wa kwanza wa mradi waliutumia kuandaa walimu na mazingira ya kufundishia.

“Tulikuwa na mfululizo wa mafunzo kwa walimu, vyuo vyote ambavyo tumefanya nao kazi tuliwajengea uwezo na sasa tuna timu nzuri ya walimu. Tulitengeneza mafunzo kazini ya wiki mbili,” amesema Mlali.

Mmoja wa vijana walionufaika na mafunzo hayo Judith Stephano (24) amesema amejifunza upishi ambao umemwezesha kujiajiri na sasa anapika vitu mbalimbali ikiwemo mikate na kuuza.

Naye mzazi mwenye mtoto mwenye ulemavu wa akili, Siasa Swamlo, amesema mwanawe wa kike mwenye miaka 21 alikuwa haelewi chochote huku akiogopa watu lakini kupitia mradi huo amebadilika na amepata ujuzi wa kushona nguo.

“Muda wa miezi mitatu ingawa ni mchache lakini mwanangu amefanya vizuri, baada ya kumaliza Veta niliona asibaki nyumbani nilimtafutia fundi ili aendelee kumpa ujuzi kwa miaka miwili.

“Baada ya kuhitimu alisema anatafuta kazi, nilikuwa na mashaka kutokana na hali yake lakini alifanikiwa kupata Mazava na mpaka sasa ana mwaka mmoja sijasikia malalamiko yoyote,” amesema Swamlo.

Mkurugenzi wa Shirika linaloshughulikia maendeleo ya wanawake na vijana (Mwayodeo), Venance Mlali, akizungumza kuhusu mradi wa Kukuza Stadi za Ufundi kwa vijana wenye ulemavu wa akili, Dar es Salaam.

Mkurugenzi wa Elimu Maalumu katika Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk. Magreth Matonya, amesema wanatamani mradi huo uendelee kutekelezwa kwa sababu bado kuna changamoto ya kukuza stadi za ufundi kwa watoto wenye ulemavu.

Amesema kwa sasa kuna vyuo 10 vya Serikali na vyuo vikuu 21 vinavyopokea watoto wenye ulemavu na tayari mtaala umeandaliwa na jitihada zinazoendelea ni kuwapa ujuzi walimu wa namna ya kuwabaini na kuwafundisha watoto husika.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles