PATRICIA KIMELEMETA, Dar es Salaam
WATENDAJI wanne wa Idara ya Fedha katika Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze, (majina tunayo) wanashikiliwa Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kuhusika na mtandao wa ubadhirifu wa fedha zikiwamo za machimbo ya kokoto zinazotoka Kijiji cha Lugoba.
Akizungumza na gazeti hili jana, Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Zainab Kawawa, alisema watendaji hao walibainika baada ya kufanyika kwa uchunguzi wa siri ulioshirikisha wadau wa Ulinzi na Usalama wa Halmashauri hiyo na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa(Takukuru).
Alisela lengo la uchunguzi huo lili kuangalia chanzo cha upotevu wa mapato pamoja na wahusika wanaoihujumu halmashauri.
Alisema katika uchunguzi huo, walibaini baadhi ya watendaji wa Idara ya fedha, wanahusika kuhujumu mapato hayo kwa kushindwa kutoza ushuru kwenye magari ya kokoto yanayoingia na kutoka.
“Katika uchunguzi wetu tulibaini kuwa baadhi ya watendaji wa Idara ya fedha ya Halmashauri hii wanashirikiana na wadau wa kokoto ili kukwepa ushuru kwa namna moja au nyingine.
“Watendaji hao wamekuwa wakiyaacha magari ya kokoto kupita bila kulipa ushuru, kuwapa risiti feki zinazoonyesha wamelipa wakati siyo kweli pamoja na baadhi ya kampuni kukwepa kulikoa kodi,”alisema Kawawa.
Aliongeza pia, baadhi ya madereva wa magari ya kokoto wamekuwa wakitoa Sh 20,000 hadi 30,000 kwa mkaguzi wa madini aliyekua kituoni wakati huo na magari hayo kuruhusiwa kuondoka bila kulipa ushuru au kodi.
Alisema awali, halmashauri hiyo ilikua inakusanya Sh milioni 400 kushuka chini, lakini baada ya kuteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya hiyo, waliweza kukusanya Sh milioni 500 hadi 600, wakati wana uwezo wa kukusanya hadi Sh milioni 900 kwa mwezi.
Alisema hivyo, basi kukosekana kwa mapato hayo kunasababisha kurudisha nyuma maendeleo ya nchi, jambo ambalo limewafanya kuwashikilia watendaji hao ili waweze kubaini mtandao huo na kuwachukuliwa hatua za kisheria.
Kawawa alisema licha ya kushikiliwa kwa viongozi hao wamebaini kuwa kuna ubadhirifu wa fedha katika soko la samaki na stendi ya mabasi Bagamoyo na soko la mnada wa mifugo la Ruvu darajani.
Alisema katika mnada wa mifugo, watendaji wamekuwa wakiwasilisha Sh 21,000 katika halmashauri hiyo kwa ajili ya ushuru wa mifugo wakati wana uwezo wa kukusanya zaidi ya Sh 500,000 kwa mwezi.
“Nimeshangazwa kuona watendaji wanaleta Sh 21,000 ya fedha za mnada wa mifugo katika soko la Ruvu darajani wakati tuna uwezo wa kukusanya zaidi ya Sh 500,000 kwa mwezi, tayari nimewachukulia hatua za kisheria wale wote wanaotuhumiwa kuhusika na kitendo hicho,”alisema.
Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Wankyo Nyigesa alisema bado wanaendelea kufuatilia suala hilo ili wakithibitika sheria ichukue mkondo wake.