29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

VIGOGO WAPIGANA VIKUMBO KURUDISHA FOMU TUME YA MAADILI

NA VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM

HAKUKALIKI. Hivi ndivyo unavyoweza kusema ikiwa ni siku moja tu tangu Rais Dk. John Magufuli, arejeshe fomu ya tamko la rasilimali na madeni katika ofisi za Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma.

Baada ya kurejesha fomu zake, Rais Magufuli, aliiagiza sekretarieti hiyo kutopokea tena fomu ya kiongozi yeyote wa umma atakayekuwa hajarejesha hadi kufikia kesho (Desemba 31, mwaka huu).

Tarehe hiyo inatambulika kuwa ndiyo siku ya mwisho kwa viongozi kurejesha fomu hizo na baada ya hapo adhabu mbalimbali zinaweza kuchukuliwa kwa mujibu wa sheria dhidi ya wale wasiozirejesha.

Akizungumza na waandishi wa habari kijijini kwake Namahema ‘A’ wilayani Ruangwa mkoani Lindi jana jioni, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, alisema ameshawasilisha tamko la viongozi wa umma kuhusu rasilimali na madeni katika sekretarieti hiyo tangu juzi Alhamisi.

Alisema fomu hizo zilipokelewa jana na ameshapatiwa barua ya kupokea tamko hilo.

“Nimewaita hapa ili kuthibitisha kuwa nimetekeleza takwa hilo la kisheria na tayari Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi ya Umma imekiri kupokea tamko langu kwa barua hii hapa,” alisema na kuongeza huku akionyesha barua hiyo iliyosainiwa juzi na Kamishna wa sekretarieti hiyo, Jaji mstaafu Harold Nsekela.

“Kwa kuzingatia mfano ulioonyeshwa na Rais Magufuli, ninawaagiza viongozi wote wanaotakiwa kujaza fomu hizo kwa mujibu wa sheria, wafanye hivyo na kuziwasilisha ifikapo tarehe 31 Desemba, 2017 saa 10 jioni,” alisisitiza.

Alisema anawakumbusha mawaziri, naibu mawaziri, makatibu wakuu, naibu makatibu wakuu wote na viongozi wote walioko katika ngazi za uteuzi wahakikishe wanatimiza takwa ambalo liko kwa mujibu wa kifungu cha 9 na cha 11 cha Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma namba 13 ya mwaka 1995.

Pia MTANZANIA Jumamosi jana lilipiga kambi katika ofisi za sekretarieti hiyo zilizopo eneo la Posta Mpya, Dar es Salaam katika Jengo la Sukari House na kushuhudia vigogo wa Serikali wakimiminika kuzirejesha fomu zao.

Vigogo hao wakiwamo wakuu wa mikoa, wakurugenzi wa wizara na taasisi mbalimbali za Serikali, makamanda kutoka Jeshi la Polisi na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), walionekana wakiingia katika ofisi hizo.

Vigogo hao walikuwa wamebeba bahasha zilizoonesha wazi kuwa ndizo walizotumia kuhifadhi fomu zao na walipotoka hawakuwa nazo tena mikononi.

Kutokana na wingi wa idadi ya watu waliokuwa wakiingia kuwasilisha fomu zao ndani ya jengo hilo, iliwalazimu walinzi kuwaruhusu kupita pasipo kujaza daftari maalumu la wageni kwa sababu walizidiwa na wingi wao.

Baadhi ya vigogo hao walipoulizwa kwanini wamechelewa kuwasilisha fomu zao hadi kusubiri mwishoni, walisema bado wapo ndani ya wakati.

Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Sophia Mjema, alisema: “Binafsi sijachelewa, bado nipo ndani ya wakati unaotambulika kwa mujibu wa sheria, nimeshawasilisha fomu zangu.”

Naye Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Ally Hapi, alisema alikuwa likizo na bado haijaisha ndipo akaona ni vema kuziwasilisha jana.

“Sijachelewa, nilikuwa likizo na inaisha Januari 2, mwakani, nilirudi kabla ya tangazo la tume ili kutimiza sheria, namshukuru Rais Magufuli amekuwa mstari wa mbele kuonyesha kwamba hakuna kiongozi ambaye yupo juu ya sheria na tutaendelea kuyaishi yale anayotuelekeza,” alisema.

Kwa upande wake, Mbunge wa Ubungo (Chadema), Saed Kubenea, naye ni miongoni mwa viongozi waliofika katika ofisi hizo lakini akizungumza na MTANZANIA Jumamosi alisema yeye tayari alishawasilisha fomu zake siku za nyuma.

“Nimekuja kuwasilisha za jamaa yangu, zangu nilishazileta siku nyingi lakini pia imebidi nihakiki tena kama kweli zipo, nimeziona. Kuna changamoto hiyo kwamba unapoleta hakuna cheti unachopewa kuthibitisha ulishawasilisha,” alisema na kuongeza:

“Hakuna hata mahala ambapo unatakiwa kusaini kwamba umeshawasilisha, imebidi nihakiki, hakuna utaratibu mzuri, unaweza kuleta na baadaye ukaambiwa hazipo.

“Kwa watu kama sisi (wapinzani) wakati mwingine tunaona sheria zinapotekelezwa inabidi tufuatilie, ni wajibu tutekeleze hizi sheria tulizotunga, lazima tuwasilishe fomu.

“Lakini hawa wanazozisimamia wasimamie kwa haki bila kuangalia sura ya mtu, chama cha mtu wala jambo lolote, kuna kesi zipo wazi lakini tume haijazifanyia kazi, kuna mabilioni yalichotwa katika sakata la Escrow pale Stanbic hawakwenda kuchunguza.

“Kuna malalamiko, tume hii naijua vizuri inasimamiwa na Kamati ya Bunge na mimi ni mjumbe katika kamati hiyo, inalaumiwa kwa kutotekeleza kazi zake au wanazitekeleza kwa jicho la chongo, katika hili itimize wajibu wake bila kuangalia mtu.”

Wakati viongozi hao wakieleza hayo, wapo waliokataa kuzungumza na waandishi wa habari.

Awali, Jaji Nsekela, alisema idadi ya viongozi wanaorejesha fomu hizo iliongezeka maradufu jana tofauti na siku za nyuma.

“Bado kuna viongozi ambao hawajawasilisha fomu zao, nitoe rai kwao watekeleze jambo hilo, tunatambua kesho (leo) si siku ya kazi, lakini tunalazimika kufungua ofisi zetu ili kuwapa nafasi warejeshe fomu hizo.

“Ofisi za makao makuu zitakuwa wazi pamoja na ofisi zetu za Kanda ya Kati Dodoma, Kanda ya Ziwa Mwanza, Kanda ya Nyanda za Juu Kusini Mbeya, Kanda ya Kusini Mtwara, Kanda ya Magharibi Tabora, Kanda ya Kaskazini Arusha na Kanda ya Mashariki Kibaha kuanzia saa mbili kamili asubuhi hadi saa 10 jioni,” alisema.

Alisema pamoja na sheria kutozuia kiongozi kumtuma mtu yeyote kumuwasilishia fomu hizo, lakini inawezekana watakuwapo watakaozijaza vibaya.

“Zinapokuja maofisa wetu huzikagua na katika ukurasa wa mwisho inaeleza tamko hilo lazima litolewe mbele ya wakili ikiwa wakili hakusaini pale, faili hilo likiletwa hiyo itakuwa ni hatari kwake na itaonesha yeye mwenyewe hakuwa makini, analetaje fomu ambayo haina muhuri wa wakili.

“Maana yake itakuwa ametoa hilo tamko bila kuapa, ikiwa anatuma mwakilishi wake alete hakuna tatizo lakini ahakikishe kilichojazwa mule ndani ni sahihi, vinginevyo tukianza kupitia sisi itamletea matatizo,” alisema.

Pia Mwanasheria Mkuu wa sekretarieti hiyo, Filotheus Manula, aliwasisitiza viongozi kujenga tabia ya kurejesha fomu hizo mapema ili kuepuka changamoto zinazoweza kujitokeza mwishoni.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles