25.8 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 16, 2024

Contact us: [email protected]

BOT YACHUNGUZA HESABU ZA AIRTEL

  • Yaagiza benki zote kuwasilisha taarifa za akaunti za kampuni hiyo

Na MWANDISHI WETU

BENKI Kuu ya Tanzania (BoT), imeziagiza benki na taasisi za fedha zilizo na akaunti za fedha zinazomilikiwa na Kampuni ya Airtel Tanzania, kuwasilisha taarifa za uendeshaji wa akaunti hizo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa juzi kwenda kwa benki na taasisi hizo na kusainiwa na Mkurugenzi wa Idara ya Usimamizi wa Benki wa BoT, Kened Nyoni, ilisema inahitaji kupitia hesabu zote za uendeshaji wa akaunti za fedha zinazohusisha kampuni za simu za Celtel, Zain na Airtel ili iweze kufanya ukaguzi.

“Ili kuwezesha ukaguzi huo, benki zote zilizo na akaunti au ziliwahi kuwa na akaunti za kampuni za mawasiliano ya simu zilizotajwa zinatakiwa kuwasilisha taarifa zote za uendeshaji wa akaunti za fedha za kampuni hizo,” ilisema taarifa hiyo.

Pia taarifa hiyo ilisema BoT inahitaji taarifa za akaunti zote za kampuni hizo kwa mara moja kwa kuanzia Januari mosi, 2000 hadi Desemba 27, mwaka huu (miaka 17) zinapaswa kuwasilishwa katika mifumo miwili tofauti ya nakala (hard copy na soft copy) kabla ya saa tano asubuhi ya jana (Desemba 29, mwaka huu).

MTANZANIA Jumamosi lilimtafuta Nyoni kwa njia simu ili atoe ufafanuzi wa taarifa na alikiri ni kweli wameomba taarifa za akaunti zote za Airtel katika benki na taasisi nyingine za fedha.

“Ni taarifa za ukweli ambazo tumetuma kwa benki, hata wiki iliyopita tulituma pia.

“Taarifa hizo zilitumwa kwa benki tu, isipokuwa kuna mtu ambaye hana maadili ametuma katika mitandao ya kijamii,” alisema Nyoni.

Taarifa ya BoT imekuja baada ya hivi karibuni Rais Dk. John Magufuli, kumtaka Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, kufuatilia kwa karibu umiliki wa Airtel kabla ya mwaka huu kuisha kwa kuwa taarifa alizonazo ni kwamba kampuni hiyo ni mali ya Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL).

Siku moja baada ya Magufuli kutoa agizo hilo, Bodi ya Wakurugenzi ya TTCL ilijitokeza na kuitaka Airtel kukabidhi mali za kampuni hiyo kwao kwa kuwa ndio wamiliki halali kabla ya kuchukuliwa hatua za kisheria.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TTCL, Omary Nundu, akizungumza hivi karibuni alisema baada ya kuifanyia uchunguzi walibaini kuwa Airtel ilisajiliwa na TTCL, masafa ni ya TTCL, mali zilizotumika kuianzisha ni za TTCL hivyo hawawezi kusema ni kampuni yao isipokuwa kipindi hicho kulikuwa na viongozi wasio waaminifu ambao hakutaka kuwataja kwa kuwa wanajijua walishiriki kuipora kampuni hiyo na kuwapa wageni na sasa ni vema wakairudisha kwa ustaarabu.

“Kwa sababu kila ukichimba unakuta mambo mazito zaidi, tumeomba Serikali ilichukue jambo hili, sisi masilahi yetu ikiwezekana ile Kampuni ya Celtel turudishiwe,” alisema Nundu.

Pia alisema mchakato uliotumiwa kuipata Celtel ni haramu na hadi sasa ipo kiharamu hivyo ni lazima irudishwe na si kuwapa hisa.

Naye Ofisa Mtendaji Mkuu wa TTCL, Waziri Kindamba, alisema menejimenti na wafanyakazi wa kampuni hiyo wanaunga mkono jitihada zinazofanywa na bodi hiyo ili kuhakikisha haki ya Watanzania inapatikana baada ya kudhulumiwa na wajanja wachache.

“Tumekubali kujitoa sadaka ya mwili na nafsi katika hili, lengo ni kuhakikisha kampuni hiyo ambayo ni mali halali ya Watanzania inarudishwa,” alisema Kindamba.

Airtel ilisajiliwa Novemba 3, 1998 na uongozi wa TTCL kwa mtaji wa Sh bilioni 200 kwa jina la Cellnet na kwa mujibu wa Nundu iliuzwa kijanja na waliokuwa viongozi wa Bodi ya TTCL.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles