24.9 C
Dar es Salaam
Sunday, April 21, 2024

Contact us: [email protected]

DK. MPANGO: HII NDIYO HALI YA UCHUMI

Na AGATHA CHARLES

SERIKALI imetoa taarifa ya mwenendo wa hali ya uchumi na utekelezaji wa bajeti yake kwa mwaka wa fedha wa 2017/2018 na imesema kwa mwaka huu sekta ya benki iligubikwa na vitu vitatu ikiwamo kuongezeka kwa mikopo chechefu kutoka asilimia 9.1 mwishoni mwa Septemba, mwaka jana hadi asilimia 12.5, Septemba, mwaka huu.

Kauli hiyo ilitolewa Dar es Salaam jana na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, wakati akitoa takwimu za hali ya uchumi, changamoto na matarajio ya Serikali na alisema mwenendo huo ni juu ya wastani unaokubalika na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) wa asilimia tano.

“Pili kupungua kwa kasi ya utoaji wa mikopo wa sekta binafsi na kupungua kwa faida itokanayo na uwekezaji kwenye rasilimali, ilifikia asilimia 2.0 mwishoni mwa Septemba, mwaka huu  ikilinganishwa na asilimia 2.5 ya Septemba, mwaka jana,” alisema Dk. Mpango.

Pia alisema faida itokanayo na uwekezaji wa mitaji ilipungua na kufikia asilimia 8.7 ikilinganishwa na asilimia 12.1 mwaka jana kutokana na kupungua kwa kasi ya utoaji mikopo, kuongezeka kwa gharama za ukwasi (funding costs) pamoja na kuongezeka kwa mikopo chechefu.

Alisema kutokana na mwenendo huo, Serikali imechukua hatua ikiwamo kuhamasisha benki za biashara kuongeza matumizi ya mfumo wa kuhifadhi na kutoa taarifa za wakopaji na BoT kutoa mikopo ya muda mfupi kwa benki za biashara.

“Benki Kuu kushusha riba kutoka asilimia 16.0 hadi 12.0 Machi, mwaka huu na hatimaye 9.0 Agosti, mwaka huu pamoja na kupunguza kiwango cha chini cha amana kinachotakiwa kuwekwa Benki Kuu na benki ya biashara kutoka asimia 10.0 hadi 8.0 kuanzia Aprili 2017,” alisema Dk. Mpango.

Alisema Serikali inaendelea kulipa malimbikizo ya madai yanayohakikiwa kwa lengo la kupunguza kiwango cha mikopo chechefu na kuchochea ukuaji wa shughuli za kiuchumi.

Pamoja na hayo, pia alisema BoT ilipunguza riba inayotozwa Serikali inapolipa kutoka BoT kutoka asilimia 6.5 hadi asilimia 3.0 kuanzia Desemba 12, mwaka huu ili kuchochea utoaji wa mikopo.

Alisema hatua hizo zimesaidia kuongeza ukwasi katika benki ya biashara na kupunguza riba ya mikopo baina ya benki na kufikia wastani wa asilimia 3.53 Novemba, mwaka huu kutoka wastani wa asilimia 14.93 kwa nusu ya kwanza ya mwaka 2016/2017.

“Riba za dhamana za Serikali zilishuka kutoka wastani wa asilimia 15.56 katika nusu tu kwanza ya mwaka 2016/2017 hadi kufikia asilimia 8.76 Novemba, mwaka huu,” alisema Dk. Mpango.

Pamoja na changamoto hizo, alisema bado sekta ya benki ni imara huku uwiano wa mtaji wa msingi kwa rasilimali za benki ukifikia asilimia 18.9 Septemba, mwaka huu ukiwa juu ya kiwango kinachohitajika kisheria cha asilimia 10.0 na asilimia 18.6 iliyofikiwa Septemba, mwaka jana.

Alisema uwiano wa rasilimali kwa amana zinazoweza kubadilishwa kwa muda mfupi kuwa fedha taslimu ilifikia asilimia 37.9 ikilinganishwa na kiwango kinachohitajika kisheria cha asilimia 20.

Alisema benki ambazo zina viwango vya chini ya uwiano zinafuatiliwa na benki kuu kwa karibu ili kulinda utulivu wa fedha na amana za wateja.

Akifafanua zaidi, alisema changamoto kama hizo haziko Tanzania pekee kwa sababu Septemba mwaka huu, Benki ya Taifa ya Rwanda ilitangaza kuwa kiwango cha mikopo chechefu katika soko lake kiliongezeka kutoka asilimia 6.2 Machi, mwaka jana hadi 8.1 Juni, mwaka huu.

“Naomba nisisitize yanayosemwa mtaani kuwa vyuma vimebana Watanzania wajue kuwa ni vyuma vyenye kutu, yaani vipato visivyo halali,” alisema Dk. Mpango.

DENI LA TAIFA

Akizungumzia deni la Taifa, alisema hadi kufikia Septemba, mwaka huu lilifikia Sh bilioni 47,823.1 ikilinganishwa na Sh bilioni 42,552.4 katika kipindi kama hicho mwaka jana.

“Kati ya kasi hiyo, shilingi bilioni 13,417.5 ni deni la taifa la ndani na shilingi bilioni 34,405.6 ni deni la nje. Deni la ndani ni sawa na asilimia 28.1 ya deni lote na deni la nje ni asilimia 71.9,” alisema Dk. Mpango.

Alisema kuongezeka kwa deni hilo kulitokana na kupatikana kwa mikopo mipya ya nje na ndani ili kulipia gharama za miradi ya maendeleo ikiwamo ujenzi wa mradi wa umeme, kuboresha huduma za maji, kuzalisha umeme Kinyerezi na ukarabati wa uwanja wa ndege.

Pia alisema ukuaji wa uchumi unatarajia kufikia asilima 7.0 mwaka huu  ukitarajiwa na uwekezaji katika miundombinu ususan

ujenzi wa reli mpya ya kati, bomba la mafuta kutoka Uganda, Mradi wa Umeme wa Stigler’s Gorge na Mradi wa Umeme wa Kinyerezi.

PATO LA TAIFA

Kuhusu Pato la Taifa alisema limekuwa kwa asilimia 6.8 katika kipindi cha nusu ya kwanza ya mwaka huu kuanzia Januari hadi Juni ikilinganisha na asilimia 7.7 ya kipindi kama hicho mwaka jana.

Akifafanua zaidi alisema tofauti ya mwaka jana na hii ya mwaka huu haimaanishi kuwa uchumi umeporomoka.

“Ukuaji wa uchumi hauendi wima au katika mstari ulioonyooka. Mara zote huenda kama wimbi lenye ukubwa tofauti hasa pale ambapo uzalishaji wa bidhaa au huduma unapokuwa wa msimu. Hivyo wanapodhani ukuaji wa uchumi unatakiwa uongezeke katika kila kipindi wanakosea,” alisema Dk. Mpango.

Akielezea hoja ambayo mara kadhaa imekuwa ikiibuliwa kuwa ukuaji wa uchumi ni wa kitakwimu tu na hauakisi hali halisi ya maisha, alisema ili kuwanufaisha wananchi wengi sharti wengi wawe wanafanya kazi katika sekta zinazokua haraka ili kujipatia kipato.

“Lakini ilivyo hapa nchini kwa sasa wananchi wengi wanaishi vijijini na wanategemea kilimo ambacho kasi ya ukuaji wake bado ni ndogo (asilimia 2.1 mwaka 2016),” alisema Dk. Mpango.

Pia alisema kasi ya ongezeko la watu hapa nchini ya asilimia 2.7 ni kubwa hivyo inatengeneza idadi kubwa ya watu kugawana pato dogo la Taifa na kwamba, kasi kubwa ya ukuaji wa uchumi ndiyo msingi wa kuboresha hali ya maisha nchini.

MFUMUKO WA BEI

Kuhusu mfumuko wa bei, alisema umeendelea kubaki katika kiwango kizuri cha tarakimu moja (wastani wa asilimia 5.4) tangu Januari hadi Novemba, mwaka huu huku Novemba hiyo hiyo ulipungua hadi asilimia 4.4.

Alisema hata kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), wastani wa mfumuko wa bei uliendelea kubaki katika wigo wa tarakimu moja huku Tanzania ikiwa na kiwango cha chini zaidi cha asilimia 5.4 na Kenya ikiwa na kiwango cha juu zaidi cha wastani wa asilimia 8.3.

Thamani ya Shilingi

Kuhusu thamani ya shilingi ya Tanzania, alisema iliendelea kuwa imara ikipungua kwa kiwango kisichozidi asilimia tatu.

Alisema Oktoba, mwaka huu, Dola moja ya Marekani ilibadilishwa kwa wastani wa Sh 2,238.03 ikilinganishwa na wastani wa Sh 2,175.49 katika kipindi kama hicho mwaka jana.

Akiba ya fedha za kigeni

Akizungumzia akiba ya fedha za kigeni, alisema imeongezeka kufikia Dola za Marekani milioni 5,911.2 ambazo zinaiwezesha nchi kununua bidhaa na huduma kutoka nje kwa kipindi cha miezi 5.4 ikilinganishwa na Dola milioni 4,093.7  zilizofikiwa mwaka juzi.

“Kiasi hiki cha sasa cha akiba ya fedha za kigeni hakijawahi kufikiwa kwa zaidi ya miaka 10 na kiko juu ya lengo lililowekwa na nchi wanachama wa EAC la kuwa na akiba ya fedha za kigeni inayokidhi kuagiza bidhaa na huduma nje ya nchi kwa miezi 4.5,” alisema Dk. Mpango.

Mapato ya ndani

Dk. Mpango alisema mapato ya ndani yaliongezeka kwa asilimia 1.0 na kufikia Sh bilioni 4.067.4 ikilinganishwa na Sh bilioni 4,033.1 zilizokusanywa katika kipindi kama hicho mwaka jana.

Alisema kiasi kilichokusanywa cha asilimia 15 kilikuwa pungufu ya lengo la Sh bilioni 4,793.0 katika kipindi hicho.

Dk. Mpango alisema kodi za ndani makusanyo yake yaliongezeka kwa asilimia 7.0 katika kipindi cha robo Julai na Septemba, mwaka huu na kufikia Sh bilioni 845.0 kutoka Sh bilioni 789.4 katika kipindi hicho cha mwaka jana  na kwamba yalifikia asilimia 88 ya lengo la Sh bilioni 961.8.

Misaada na mikopo 

Alisema mwaka 2017/2018 jumla ya Sh bilioni 3,971.1 ziliahidiwa na washirika wa maendeleo katika utekelezaji wa bajeti (asilimia 12.5 ya ajeti yote) lakini hadi kufikia Septemba Sh bilioni 325.9 ndizo zilitolewa.

“Hii ni sawa na asilimia 62.3 ya lengo la kipindi hicho cha robo mwaka. Kati ya fedha zilizotolewa hadi Septemba mwaka huu, Sh bilioni 58.02 zilipokelewa kupitia mifuko ya pamoja ikiwa ni sawa na asilimia 50.6 ya makadirio yaliyowekwa.

Shilingi bilioni 267.9 zilizotolewa kupitia miradi ya maendeleo.

Mikopo ya ndani

Alisema Julai hadi Septemba mwaka huu, Serikali iliweza kukopa Sh bilioni 1,655.3 kutoka soko la ndani sawa na asilimia 96.6 ya lengo la kukopa Sh bilioni 1,714.3.

Alisema kati ya kiasi hicho, Sh bilioni 1,107.1 zililipia hati fungani na dhamana za Serikali zilizoiva huku Sh bilioni 548.2 zikiwa ni mikopo mipya kugharamia miradi ya maendeleo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles