25 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

Vigogo wanane Polisi watajwa kumrithi DCI

Rais Dk.John Magufuli
Rais Dk.John Magufuli

NA MWANDISHI WETU,

MAOFISA wanane wa ngazi za juu katika Jeshi la Polisi wanatajwa kurithi mikoba ya aliyekuwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI),Diwani Athuman.

Juzi, Rais Dk.John Magufuli alitengua uteuzi wa DCI Athuman,ingawa hadi sasa haijaelezwa wazi kwa nini alichukua uamuzi huo.

Kuondolewa kwa kigogo huyo wa polisi aliyedumu kwenye nafasi hiyo kwa mwaka mmoja na miezi minne, kumezua minong’ono mingi ingawa bado usiri mkubwa umetanda juu ya suala hilo.

Hata hivyo, MTANZANIA imepata taarifa za uhakika kutoka ndani ya jeshi hilo kuwa mchakato wa kumpata DCI mpya unahusisha maofi sa wanane ambao wamewahi kushika nyadhifa mbalimbali katika Jeshi la Polisi nchini.

Miongoni mwa maofisa hao ni aliyewahi kuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela.

Kenyela alijijengea umaarufu mkubwa wa kutoa taarifa za matukio na kuwa karibu na wananchi wakati akiwa kiongozi wa mkoa huo wa polisi.

Akiwa na taaluma ya uanasheria, anasifika na kuelezwa kuwa na uzoefu, uadilifu na kutokuwa na papara katika majukumu yake.

Pia ofisa huyo wa polisi amewahi kuwa mkuu wa mashtaka Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na Kivukoni, zote za Dar es Salaam.

Mwingine ni Naibu Kamishna wa jeshi hilo (DCP),Aziz Mohamed.

Kitaaluma, Mohamed ni mwanasheria na hadi sasa anasoma masomo ya juu katika Chuo cha Ulinzi cha Taifa (NDC), Dar es Salaam.

“Huyu ni mpelelezi mzuri, wote tuliofanya naye kazi tunamtambua, tunajua akiwa RCP wa Mkoa wa Mjini Magharibi kule Zanzibar alishughulikia mambo mengi na mazito.

“Kuhusu huyo jamaa, taifa lina hazina ya intelijensia ya kutosha. Kama Rais Magufuli anataka watendaji makini  unaamini atafanikiwa,”kilisema chanzo chetu ingawa kumbumbuku zinaonyesha nafasi ya DCI haijawahi kushikwa na kigogo wa polisi kutoka Zanzibar.

Kigogo mwingine anayetajwa ni Mkurugenzi wa Oparesheni na Mafunzo, Nsato Marjani.

Huyu anasifika kwa kufanya kazi ya upelelezi kwa kipindi kirefu katika mikoa mbalimbali kabla ya kuhamishiwa makao makuu ya polisi.

Inaelezwa kuwa hata alipohamishiwa makao makuu idara ya upelelezi, amefanikiwa kwa kiasi kikubwa kuimarisha idara hiyo.

Ofisa mwingine anayetajwa katika nafasi hiyo ni Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha (DCP),Charles Mkumbo.

Huyu anatajwa kwenye nafasi hiyo kutokana na uzoefu wa muda mrefu kwenye upelelezi.

Yeye anasifika kwa kufanya kazi kubwa alipokuwa mkuu wa upelelezi Kituo cha Polisi Oysterbay Dar es Salaam ambako aliweza kupambana na kuvunja mtandao ya ujambazi uliokuwa ukitokea katika benki.

Kutokana na kazi kubwa hiyo, alihamishiwa Mkoa wa Manyara kuwa RPC kabla ya kupelekwa Mkoa wa Arusha ambako kwa kiasi kikubwa ameweza kudhibiti matukio mengi ya uhalifu.

Mwingine anayetajwa ni Kamishina wa Polisi, Robert Boaz.

Huyu anatajwa kutokana na kuwa na uwezo katika masuala ya upelelezi.

Aliwahi kuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro ambako alipambana na kufanikiwa kudhibiti ujambazi hasa sehemu za mijini na mipakani.

Aliyewahi kuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, David Misime anaelezwa kuwa mmoja wa makamanda wa polisi wenye uwezo mkubwa wa kukabiliana na hoja na mazingira yoyote ya kazi anakopangiwa.

Anasifika kwa kuimarisha ulinzi katika maeneo mengi ya Mkoa wa Dodoma kwa kipindi chote alichokaa hapo kabla ya kuhamishiwa makao makuu ya polisi na kupangiwa majukumu mengine.

Inaelezwa kuwa amebobea mno katika masula ya upelelezi na hadi sasa yuko ofisi ya DCI ambako anaendelea na majukumu ya kazi.

“Misime amezunguka mikoa mingine ana uzoefu mkubwa… tena jambo jema mpaka sasa yuko ndani ya ofi si ya DCI anakoendelea na majukumu yake”

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles