25 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 19, 2024

Contact us: [email protected]

Vigogo wafichua ushauri waliopewa na mzee Apson

Grace Shitundu

MAZISHI ya aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa, Apson Mwang’onda, yamekutanisha viongozi mbalimbali ambao wameelezea alama aliyoiacha kiongozi huyo.

Viongozi hao walizungumza kwa nyakati tofauti katika shughuli ya mazishi ya Mkurugenzi huyo mstaafu yaliyofanyika Kijiji cha Old Vwawa, Mbozi mkoani Mbeya baada ya kufariki dunia Oktoba 7 akiwa katika matibabu nchini Afrika Kusini.

Wakizungumza kwa nyakati tofatuti, viongozi hao walisema pamoja na nafasi aliyokuwa nayo Apson, alikuwa akitoa ushauri wenye hekima katika mambo mbalimbali.

DIWANI ATHUMAN

Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa (TISS), Diwani Athuman, alisema  Apson alimtaka kuzingatia haki katika utekelezaji wake wa majukumu katika kazi hiyo.

Alisema miaka 13 iliyopita alimwita na kumtaka kuongeza juhudi, kutenda haki na kuwa na ushirikiano na wenzake

 “Mzee Apson amefanya mambo mengi sana na yanayozungumzwa naweza kuyashuhudia, miaka 13 iliyopita akiwa karibu na kustaafu, mimi sikuwa nafanya naye kazi kwa karibu, lakini alikuwa anajua kuwa mimi ni kijana wake, aliniita nyumbani kwake, nilimkuta na mafaili mengi, nilipoingia aliacha na tukaanza kuzungumza.

 “Aliniambia ‘kijana wangu natambua unafanya majukumu yako vizuri, lakini nataka nikuongezee nguvu, jitahidi ufanye vizuri zaidi, zingatia kutenda haki, kazi unayoifanya inahitaji kuitekeleza kwa haki, penda kushirikiana na wengine, jitume katika kazi’. Hiyo ilikuwa ni mwaka 2006, miaka 13 iliyopita nikiwa ofisa wa kati,” alieleza Diwani.

Alisema Apson alikuwa anaheshimu wakubwa na wadogo pamoja na kwamba hakuwa anafanya naye kazi kwa ukaribu, lakini alikumbuka na kumwita.

Aidha alisema kwamba Apson ameacha alama kubwa katika idara hiyo ambayo inatakiwa kuenziwa.

“Mzee Apson katika muda wote alipokuwa mtumishi na alipokuwa mkurugenzi wa Idara ya Usalama wa Taifa, ameacha alama kubwa ndani ya Idara ya Usalama wa Taifa, ameacha alama kubwa katika nchi, amefanya mambo mengi kwa faida ya nchi.

“Alikuwa ‘committed’, alikuwaa anajituma, kimsingi sisi wana-idara tumeachiwa alama kubwa sana, ni vyema tukatafakari kuona ni kwa namna gani tutamuezi mzee Apson,” alisema Diwani.

Rashid Othman ambaye alichukua nafasi ya Apson baada ya kustaafu, alisema kuwa mzee huyo aliishi kwa hekima na kati ya mambo ambayo alikuwa akimfunza ni kwamba mamlaka, uongozi usimpe kiburi.

MBOMA

Mkuu wa majeshi mstaafu, Robart Mboma, alisema Apson alikuwa mbunifu, alifanya kazi yake vizuri na kipindi cha uongozi wake alikuwa ni mshauri wake katika masuala ya usalama wa taifa.

“Mimi niposhika madaraka yale nilianza kuangalia kazi za usalama wa taifa, kukawa na njaa, lakini swala hilo halikuandikwa katika mambo ya usalama wa taifa, Apson alinipigia simu kuwa kuna usalama wa taifa unataka kuharibika kwa sababu ya njaa.

“Alikuja kueleza jinsi mtu alivyokuwa na njaa anavyoweza kubadilika na akili zake zinavyowezakuwa na akafanya kitu chochote,” alisema.

Alisema Apson alikuwa anafanya kazi zake kwa bidii, kukiwa na tatizo yeye atachukua muda na kufikiri kwa haraka na kuja kutoa mawazo yake kwenye kikao.

MWAKIPESILE

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya mstaafu, John Mwakipesile, ambaye alikuwa rafiki wa Apson alisema kuwa aliweza kuwa naye karibu kwa kuwa alikuwa anamfuata fuata kwa ajili ya hekima yake.

“Katika mazungumzo yote ambayo tulikuwa nayo kipindi hicho, nikagundua kuwa ana hekima kubwa sana, jasiri mwenye upendo, usitaje tatizo lako kwake, analinunua lile tatizo linakuwa la kwake na kama ana uwezo atakusaidia hata kama hujaomba,” alisema.

Alisema Apson alikuwa na kipaji cha aina yake, alikuwa anapendwa na watu, mkarimu, mnyenyekevu.

Mwakipesile alisema Apson alikuwa na damu ya uongozi ndani yake kwani alitoka katika familia ya kichifu.

MBOWE

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, alisema Apson alikuwa ni kiongozi muhimu katika taifa na alikuwa anamshauri mara kwa mara.

“Nimekuja hapa kwa sababu kuu tatu, kwanza mzee Apson tulifahamiana, alinipenda, tulikuwa na ukaribu japo wa masaa kadhaa, lakini tulikuwa na ukaribu wa kutosha, alikuwa ananishauri mara kadhaa, nami nilifaidia na ushauri wa mzee huyu.

“Ningependa nitoe ujumbe mmoja muhimu sana kwa viongozi wote, hasa vyombo vya ulinzi na usalama, kwani hii ndiyo fursa ambayo nimeipata.

 “Tunaheshimu wajibu unaofanywa na vyombo ya usalama, tunathamini kazi inayofanywa kwa niaba ya taifa letu, watuone kama watu wa sehemu ya umoja na mshikamano wetu, tunaoweza kuwasaidia kujenga amani na usalama wa nchi,” alisema.

Alisema taifa linastahili kujengana na kupendana, hivyo yeye na chama chake wako tayari kushirikiana na chombo chochote ili kufanya nchi hii inakuwa mahali bora na salama pa kuishi.

FRED LOWASSA

Fred Lowassa ambaye alikuwa anamwakilisha baba yake, Edward Lowassa alisema kwamba kifo cha Apson ni pigo kwa baba yake kwani alikuwa akimshauri.

“Baba amesema mzee Apson hakuwa rafiki yake tu bali ni kaka yake wa kwanza, ushauri wake wote wakati anaingia kwenye uongozi alikuwa anaupata kwa mzee Apson,” alisema Fred.

THOMAS MWANGONDA

Mtoto wa marehemu, Thomas Apson Mwangonda ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Mwanga, alitoa shukrani kwa Rais Magufuli kwa kumhudumia kwa ukaribu baba yake na kusema kuwa aliupokea msiba huo kwa masikitiko makubwa.

“Rais alimfahamu mzee Apson kivyake, mimi hata sifahamu walifahamiana vipi, lakini rais amekuwa akijitoa kwa watu wengi, na baba yetu alipata nafasi ya kuhudumiwa na rais kwa ukaribu na upendo mkubwa sana,” alisema.

Tom alielezea namna alivyopigiwa simu na Rais Magufuli baada ya msiba kutokea.

Alisema alidhani ni ‘alarm’ kwani alipigiwa saa nane na nusu usiku.

“Rais aliongea kwa maneno ya uchungu sana, kwa unyenyekevu sana, vile mnavyomuona akiwa jukwani ni tofauti kabisa akiwa katika mambo ya kifamilia, hivyo nataka mtambue kuwa mna Rais anayewapenda,” alisema Tom.

Pia aliwashukuru viongozi wengine wa Serikali, wastaafu, wakiwamo wa idara ya usalama wa taifa na watu wote waliojumuika nao katika kipindi hiki.

MATALUMA

Msemaji wa familia, Emmanuel Mataluma alisema Apson alikuwa na uweledi na alikuwa mshauri mzuri na kwa maana hiyo aliweka msingi imara wa utendaji kazi wa idara  ambao viongozi waliofuata wameendelea kuuimarisha.

Mataluma alisema Agosti 20, mwaka huu  Apson alilazwa katika Hospitali ya Emilio Mzena na baadaye Agosti 21 alihamishwa katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) mkoani Dar es Salaam.

“Hata hivyo Septemba 14 alikwenda Afrika Kusini kwa ajili ya matibabu zaidi, lakini pamoja na juhudi zote Oktoba 7 mwaka huu mzee Apson alifariki dunia,” alisema.

Marehemu Apson ameacha mke, watoto watano na wajukuu nane.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles