27.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

Vigogo kizimbani mgawo Escrow

2Na Kulwa Mzee, Dar es Salaam
SAKATA la uchotwaji wa zaidi ya Sh bilioni 300 kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow, limeanza kuchukua sura mpya baada ya Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru), kuwafikisha mahakamani vigogo wawili wa Serikali.
Vigogo hao, waliofikishwa Mahakama ya Kisutu jijini Dar es Salaam jana, ni Mhandisi Mkuu wa Mradi wa Umeme Vijijini (REA), Theophillo Bwakea na Mkurugenzi wa Huduma za Kisheria wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Rugonzibwa Mujunangoma, ambao kwa pamoja wanadaiwa kupokea rushwa ya Sh milioni 485.1.
Licha ya vigogo hao, taarifa za ndani ya Takukuru zinasema wakati wowote kuanzia sasa, viongozi wengine watafikishwa mahakamani kwa tuhuma hizo.
Taasisi hiyo imewafikisha mahakamani vigogo hao chini ya kifungu namba 15(1) cha sheria ya kuzuia rushwa Namba 11/2007 ambayo kushtakiwa hakuhitaji kibali kutoka kwa Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP).

THEOPHILLO
Mshtakiwa Theophillo, alifikishwa mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Kisutu, Frank Moshi na Wakili wa Serikali kutoka Takukuru, Leonard Swai.
Alisomewa mashtaka ya kupokea rushwa ya Sh milioni 161.7 kutoka kwa Mkurugenzi wa Kampuni ya VIP Engineering, James Rugemalila ambazo ni sehemu ya fedha zilizokuwamo kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow.
Kabla ya kufanya kazi REA, Theophillo alikuwa Wizara ya Nishati na Madini, kitengo cha kusimamia umeme, ambako anadaiwa alishiriki kutunga sera ya kampuni binafsi kuuza umeme Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco)na ilipoanza kutumika, Kampuni ya kufua umeme ya IPTL ilikuwa ya kwanza kupata zabuni.
Wakili wa Serikali, Swai, akisoma mashtaka yanayomkabili Theophillo, alidai Februari 12, 2014 katika Benki ya Mkombozi, mshtakiwa akiwa Mhandisi Mkuu wa REA, kwa rushwa alijipatia Sh milioni 161.7 kupitia akaunti namba 00410102643901 fedha ambazo ni sehemu ya zilizokuwapo katika Akaunti ya Tegeta Escrow.
Alidai fedha hizo aliingiziwa katika akaunti yake na Rugemalila ambaye ni mshauri binafsi wa kimataifa, Mkurugenzi wa VIP Engineering na alikuwa Mkurugenzi wa IPTL.
Fedha hizo, zinadaiwa alipewa zawadi kwa kuwa alikuwa mmoja wa wajumbe walioandaa sera zilizoruhusu sekta binafsi kuuza umeme Tanesco.
Mshtakiwa huyo alikana kutenda makosa hayo.
Upelelezi wa kesi umekamilika na Takukuru hawakuwa na pingamizi kwa mshtakiwa kupewa dhamana isipokuwa waliomba masharti yazingatie kiwango cha fedha na akaunti iliyoingiziwa fedha izuiliwe kutumika hadi kesi itakapomalizika.
Hakimu Moshi, alimwachia mshtakiwa kwa dhamana baada ya kukamilisha masharti ya kuwa na wadhamini wawili ambao ni watumishi wa Serikali ama kutoka taasisi inayotambulika waliotakiwa kuwa na barua za utambulisho na kila mmoja kusaini dhamana ya maandishi ya Sh milioni 25.
Mshtakiwa hatakiwi kusafiri nje ya Dar es Salaam bila kibali cha mahakama na fedha zilizomo katika akaunti aliyoingiziwa fedha hazitakiwi kutumika hadi kesi itakapomalizika.
Mshtakiwa atasomewa maelezo ya awali Januari 29, mwaka huu.

RUGONZIBWA
Mshtakiwa Rugonzibwa alipandishwa kizimbani mbele ya Hakimu Mkazi, Emilius Mchauru na Wakili wa Serikali kutoka Takukuru, Leonard Swai na kusomewa mashtaka ya kupokea rushwa ya Sh milioni 323.4 zilizokuwa katika akaunti ya Tegeta Escrow kutoka kwa Rugemalila.
Kabla ya Rugonzibwa kufanya kazi Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, alikuwa mwanasheria wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (RITA), ambako alihusika na mufilisi wa Kampuni ya IPTL.
Rugonzibwa, aliichunguza IPTL, alisimamia watumishi wake wakati kampuni hiyo iko katika mufilisi na alisimamia mashauri mbalimbali yanayoihusu.
Wakili Swai, akisoma mashtaka mbele ya Hakimu Mchauru, alidai Februari 5, 2014 katika Benki ya Mkombozi, mshtakiwa akiwa Mkurugenzi wa huduma za kisheria wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Mkazi alipokea Sh milioni 323.4 kupitia akaunti yake namba 00120102602001.
Fedha hizo, zinadaiwa ni sehemu ya fedha zilizokuwamo katika akaunti ya Tegeta Escrow ambazo alipokea kutoka kwa Rugemalila.
Mshtakiwa alikana mashtaka, upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na upande wa mashtaka haukuwa na pingamizi kupata dhamana, isipokuwa waliomba akaunti hiyo izuiliwe kutumika hadi kesi itakapomalizika.
Hakimu Mchauru, alimtaka mshtakiwa kuwa na wadhamini wawili kutoka taasisi za Serikali, wasaini dhamana ya maandishi ya Sh milioni 10, mmoja awasilishe fedha nusu ya alizopokea mshtakiwa mahakamani ama atoe hati ya mali isiyohamishika yenye thamani hiyo.
Mshtakiwa pia hatakiwi kutoka nje ya Dar es Salaam bila kibali cha mahakama, na kuhusu fedha katika akaunti, upande wa mashtaka umetakiwa kuwasilisha maombi rasmi ya kutaka akaunti hiyo izuiwe hadi kesi itakapomalizika.
Wadhamini walitimiza masharti ya dhamana, na hakimu aliahirisha kesi hadi kesho kwa ajili ya kupata thamani halisi ya hati iliyowasilishwa mahakamani.

PROFESA TIBAIJUKA
Habari za uhakika zilizoifikia MTANZANIA, zinasema aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka na Rugemalila wako mbioni kufikishwa mahakamani wakati wowote kuanzia sasa.
Chanzo chetu kinasema tayari Profesa Tibaijuka na Rugemalila wana taarifa zote za kufikishwa mahakamani kutoka Takukuru.
Kutokana na kashfa hiyo ya Escrow, aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Frederick Werema alijiuzulu, Profesa Tibaijuka, uteuzi wake ulitenguliwa, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi amesimamishwa kazi, huku Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo akiwekwa kiporo na Rais Jakaya Kikwete hadi uchunguzi dhidi yake utakapokamilika.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles