28.7 C
Dar es Salaam
Thursday, February 22, 2024

Contact us: [email protected]

Makada sita wa urais CCM kujadiliwa Kamati Kuu ijayo

gzNA ELIAS MSUYA, ZANZIBAR

WAKATI vuguvugu la kuwania kuteuliwa kugombea urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) likiendelea kupamba moto, Kamati Kuu (CC) ya chama hicho imesema adhabu waliyopewa makada sita walioonyesha nia ya kutaka nafasi hiyo, itapitiwa tena Februari na watakaobainika kuendelea kufanya makosa wataongezewa adhabu.
Katibu Mwenezi wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Nape Nnauye, alisema suala hilo ni moja ya maazimio yaliyofikiwa na kikao hicho kilichokutana jana kisiwani Unguja, Zanzibar, chini ya uenyekiti wa Rais Jakaya Kikwete.
Makada hao waliopewa adhabu ya miezi 12 kwa kuanza kampeni mapema, Februari 18 mwaka jana ni Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu), Steven Wasira, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba, Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja na mawaziri wakuu wastaafu, Edward Lowassa na Frederick Sumaye.
Nape alisema baada ya makada hao kumaliza kutumikia adhabu hiyo waliyopewa na chama, itafanyika tathmini ili kuangalia waliokiuka kanuni za adhabu hiyo na wakibainika wataongezewa.
“Kuna makada sita wa CCM waliopewa adhabu kwa kuanza kampeni mapema, adhabu yao itaisha mwezi wa pili. Baada ya kipindi hicho itafanywa tathmini na ikibainika kuna waliokiuka maadili, wataongezewa adhabu,” alisema Nape.
Kuhusu shughuli za chama mwaka huu, Nape alisema bado ratiba ya kuteua viongozi wa chama haijapangwa, bali iliyopo ni ya shughuli za kawaida za chama.
“Kamati Kuu imepitisha ratiba ya shughuli za chama kwa mwaka 2015. Mwaka huu kutakuwa na ratiba ya uteuzi wa wagombea kupitia CCM kwenye vyombo vya dola.
Iliyopitishwa ni ratiba ya shughuli za chama, ratiba ya mchakato wa kuwapata wagombea itapangwa na vikao vijavyo vya chama,” alisema.

KASHFA YA ESCROW
Kamati hiyo pia iliafikiana kuwachukulia hatua makada wake walio kwenye vikao vya uamuzi vya chama ambao wamehusishwa katika kashfa ya Tegeta Escrow.
Viongozi hao ni aliyekuwa Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Profesa Anna Tibaijuka ambaye pia ni mjumbe wa Kamati Kuu, Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge na Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja wote wakiwa wajumbe wa Halmashauri Kuu.
“Kamati Kuu imeiagiza kamati ndogo ya maadili iwachukulie hatua viongozi waliohusika kwenye sakata la Escrow ambao wapo kwenye vikao vya uamuzi vya chama,” alisema Nape na kuongeza:
“Mtakumbuka katika sakata hili wapo viongozi wetu wa chama ambao wapo kwenye vikao vya maamuzi kwa maana Kamati Kuu na Halmashauri Kuu na kwa namna moja ama nyingine vitendo vyao vimehusishwa na ukiukwaji wa maadili…Kwa kweli hatua ni kuondoka kwenye vikao vya maamuzi.”
Alisema ili kutekeleza agizo hilo la Kamati Kuu, kamati ndogo ya maadili itakutana Januari 19 chini ya Makamu Mwenyekiti wa chama hicho – Bara, Philip Mangula.
Kutokana na hatua hiyo, Kamati Kuu inaonekana kumkwepa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Muhongo ambaye ni miongoni mwa wanasiasa na watendaji wa Serikali waliotajwa katika mapendekezo ya Bunge wakitakiwa kuwajibishwa.
Akizungumza na wazee wa Mkoa wa Dar es Salaam Desemba 22, 2014, Rais Kikwete alisema amemweka kiporo Profesa Muhongo ili kupisha uchunguzi dhidi yake.
Wengine waliotakiwa kuwajibishwa katika mapendekezo ya Bunge ni pamoja aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Werema ambaye alijiuzulu, aliyekuwa Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini, Maswi aliyesimamishwa kazi na Majaji Aloysius Mujuluzi na Profesa Jaji Eudes Ruhangisa.
Nape alisema chama hicho kimesikitishwa na kashfa hiyo na kuwataka wale wote waliopewa dhamana kujenga utamaduni wa kuwajibika na wasipowajibika, waliowapa dhamana wawawajibishe.
“Chama Cha Mapinduzi kimesikitishwa sana na sakata hili… Baada ya kupokea taarifa na kuijadili, Kamati Kuu imeiagiza Serikali kutekekeleza maazimio ya Bunge yaliyobaki.
“Kamati Kuu inawataka wale wote waliopewa dhamana wajenge utamaduni wa kuwajibika na wasipowajibika, waliowapa dhamana wawawajibishe,” alisema Nape.
Nape alisema CCM inaongoza kwa kuwawajibisha wanachama wake kulinganisha na vyama vingine.
“Chama hiki kina uzoefu wa kuwawajibisha watu wote wanaokiuka maadili, tulianza na Maalim Seif (Sharif Hamad- sasa Katibu Mkuu wa CUF) na uko mlolongo mrefu.
“Kama unatoka Zanzibar tulimfukuza Mansour hapa… alianza CUF akaja CCM amerudi kwao. Kama ni mfano wa kuwajibisha hatujaanza jana…” alisema Nape.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
583,000SubscribersSubscribe

Latest Articles