27.2 C
Dar es Salaam
Thursday, May 23, 2024

Contact us: [email protected]

VIGOGO AFRIKA WAMSAKA ULIMWENGU

Na MOHAMED KASSARA-DAR ES SALAAM


THOMAS ULIMWENGU
THOMAS ULIMWENGU

VIGOGO wa soka Afrika timu ya Al Ahly ya Misri, wametenga dau nono ili kumnasa mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania, Thomas Ulimwengu, baada ya kuvutiwa na kiwango alichokionyesha wakati akicheza katika klabu ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Miamba hiyo ya Afrika iliyowahi kunyakua ubingwa wa michuano ya Klabu Bingwa Afrika kwa mara nne, wamepania kumsajili straika huyo aliyemaliza mkataba wake TP Mazembe mwaka huu.

Klabu ya Al Ahly ambayo imetwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya nchini Misri mara 38, inadaiwa kutenga kiasi cha Dola za Marekani 400,000 (sawa na Sh milioni 868) kwa mwaka kwa ajili ya mshahara wa Ulimwengu.

Wakala wa nyota huyo mwenye umri wa miaka 23, Jamal Kisongo, aliliambia MTANZANIA jana kuwa Ulimwengu anatakiwa na klabu nyingi za Afrika na Ulaya ambapo baadhi tayari zimeanza kutangaza ofa zao.

“Al Ahly wametoa ofa nono lakini mipango yetu tunataka Ulimwengu akacheze soka barani Ulaya,” alisema.

Aidha, Kisongo alisema kuna timu kubwa nchini Ubelgiji inamuhitaji na kutaka akafanye mazoezi, lakini wamekataa ombi lao.

“Utaratibu wa kufanya mazoezi hauwezekani kwa sababu ni kama wanamfanyia majaribio, jambo ambalo si sawa kwa mchezaji ambaye timu yake imeshinda ubingwa wa Afrika,” alisema.

Kisongo alisema kuna timu inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza nchini Uingereza ambayo ilimtaka kwa sharti la kumfanyia majaribio, lakini wakagoma kwa kuwa Ulimwengu ni mchezaji mwenye uwezo mkubwa ambaye ameshinda kila kitu katika ngazi ya klabu.

Straika huyo aliyewahi kukipiga katika timu ya Taifa ya vijana chini ya miaka 20 mwaka 2009 na sasa timu ya taifa Tanzania, ‘Taifa Stars’, saini yake inawindwa na klabu tofauti duniani ikiwamo nchi za Ubelgiji, Hispania, China, Uingereza, Qatar, Dubai, Urusi, Sudan na Misri.

Aidha, wakala huyo alisema Ulimwengu amechelewa kujiunga na timu zinazomtaka kutokana na kusumbuliwa na majeraha ya goti aliyoyapata wakati akiitumikia timu yake ya TP Mazembe, mchezo wa Kombe la Shirikisho barani Afrika.

“Kwa sasa ameanza mazoezi ya kujiweka fiti chini ya uangalizi wa daktari, lakini pia amepata mwaliko wa kufanya mazoezi katika klabu ya Mamelody Sundown ambao ni mabingwa wapya wa Ligi ya Mabingwa barani Afrika,” alisema Kisongo.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles