UNACHOKIONA kinaweza kuwa si kitu kipya kwako, lakini kinachovutia kutazama licha ya kwamba unafahamu ni kinyume cha sheria tuzijuazo za usalama barabarani.
Nchini Tanzania si mara moja tumeshuhudia vyombo vya moto vikipakia mizigo au abiria kwa staili ya mishikaki kama inavyojulikana hapa nchini katika hali inayohatarisha usalama barabarani.
Kwa mfano; utaona bajaji imebeba kitanda au mbao, pikipiki imebeba magunia ya mkaa kiasi cha kumfanya dereva ashindwe kuona kinachojiri nyuma yake.
Kadhalika unaweza kuona gari ya mizigo aina ya Suzuki Carry ikiwa imebeba mabomba marefu yanayotokeza nje na hali kadhalika gari lililoelemewa na mizigo likichechemea upande.
Mifano ni mingi na madereva wanaofanya hivyo kimsingi si tu wanavunja sheria bali pia kuhatarisha usalama wao, abiria na wapita njia. Usisahau pia uharibifu wa miundombinu inayojengwa kwa fedha nyingi za walipa kodi.
Kwa sababu hiyo, si rahisi katika jiji lenye askari wa usalama barabarani waliotapakaa kila kona kama Dar es Salaam kukutana na aina hiyo ya ubebaji mizigo au abiria kwa staili ya mishikaki tena bila kuvaa kofia ngumu bila kukamatwa.
Pengine utaishuhudia zaidi katika maeneo ya nje ya jiji au miji nchini Tanzania na kwingineko duniani.
Lakini kwa nchini Vietnam ubebaji wa abiria kwa staili ya mishikaki na mizigo mikubwa katika vyombo vya moto ni jambo la kawaida mno, kiasi cha kuwa kivutio kwa watalii na wageni.
Tukiachana na magari, uendeshaji pikipiki, ambazo ndizo makusudio ya safu yetu hii leo kwa kukata kona katika mitaa ya jiji lenye shughuli nyingi ni jambo gumu mno.
Licha ya ugumu huo kuna nyongeza ya mzigo mkub
wa uliopakiwa pengine wa mamia ya trei za mayai, vyombo vya vyumbani, fenicha, wanyama au binadamu.
Katika hali hiyo ugumu huo wa uendeshaji unaongezeka maradufu na hivyo kuonekana kama jambo lisilowezekana.
Nchini Vietnam linawezekana kiasi kwamba linaonekana kama sehemu ya sanaa, yaani sanaa ya ubebaji mizigo ya aina yake.
Kukutana na magari, pikikipi au baiskeli barabarani ikiwa imejaa mizigo kiasi cha dereva kupata shida kuona nyuma ni jambo la kawaida.
Tukirudi katika pikipiki maarufu bodaboda, kuanzia matembezi ya kifamilia, utakutana na watu watatu, wanne, watano, sita na au zaidi wakiwa wamebana kama mishikaki.
Hao ni pamoja na watoto wa ukubwa na umri tofauti na wakati mwingine vichanga.
Watalii au wageni hawaishi kukodolea macho tu sanaa hiyo ya ubebaji abiria na mizigo katika mitaa ya mji mkuu wa nchi hiyo Ho Chi Minh bali pia kuchukua picha za kumbukumbu au zawadi kwa marafiki au wapendwa wao.
Hayo ni sehemu ya maisha ya Vietnam, ambapo pikipiki au bodaboda ni usafiri maarufu wa teksi, ambazo kadiri zinavyojaza mizigo au abiria ndivyo kipato kinavyoongezeka.