27.5 C
Dar es Salaam
Tuesday, February 7, 2023

Contact us: [email protected]

TUNAYOPASWA KUYAAMINI KUHUSU SHULE ZA MSINGI ZA BWENI -6

Na CHRISTIAN BWAYA


MFULULIZO wa makala hizi umeangazia, japo kwa ufupi, mchango wa shule za msingi za bweni katika makuzi ya mtoto mdogo. Jambo lililo dhahiri ni kuwa shule hizi zinasisimua ufahamu wa mtoto na hivyo kuwa fursa muhimu kwa maendeleo ya mtoto kitaaluma. 

Hata hivyo, mchango huu chanya unaotambuliwa katika tafiti zilizofanyika duniani kote, unaambatana na changamoto kadhaa za kitabia kwa mtoto. Kama tulivyoona, watoto wadogo wanaowahishwa bweni wanakuwa kwenye hatari ya kujenga upweke wa nafsi. Upweke huu unaambatana na tabia hasi kama vile kutokujiamini na kutokuwaamini wengine, hasira zisizo na maelezo, kulia lia na ugomvi. 
Ieleweke kuwa hatuyasemi haya kuwatengenezea hatia wazazi wanaopeleka watoto bweni. Lengo, kama tutakavyoona juma lijalo, ni kumsaidia mzazi kufanya uamuzi sahihi unaoongozwa na uelewa.

Katika makala iliyopita, tulianza kuangazia namna gani mazingira ya kimalezi katika shule hizi yanachangia changamoto za kitabia kwa mtoto. Jambo la kwanza, mazingira ya shule za bweni yanamnyima mtoto fursa ya kuwa na ukaribu na mtu mzima anayemwamini. 
Kwa kawaida, mtoto mdogo anahitaji kujenga ukaribu na watu anaowaamini. Anahitaji mtu mzima anayeweza kuwa tayari kusikiliza mashtaka yake, matumaini yake na hata masimulizi ya fahari za mambo mema anayoyafanya mchana kutwa. Mtu wa namna hii anapokosekana mtoto hujikuta katika hali ya upweke na kupungukiwa. 

Katika shule kadhaa nilizotembelea ilibainika kuwa mlezi mmoja aliwaangalia watoto zaidi ya 100 kwa wakati mmoja. Katika mazingira haya, ni vigumu kwa mtoto mmoja mmoja kupata mtu anayeweza kumsikiliza na kutatua changamoto anazokabiliana nazo.
Watoto walilelewa kimakundi na mahitaji yao yalifikiriwa kiujumla jumla kwa kuongozwa na utaratibu rasmi. Mathalani, walezi walihakikisha mtoto anapata chakula, anakuwa msafi, analala mahali salama. Hata hivyo, walikiri hawakuwa na uwezo wa kumsikiliza mtoto mmoja mmoja. Muda huo haukuwapo.

Aidha, katika mazungumzo na watoto, ilikuwa bayana kuwa wengi wao hawakupata nafasi ya kuonana na wazazi wazo kwa zaidi ya miezi mitatu. Wazazi, pengine kwa sababu za msingi kabisa, waliwatuma watu wengine kwenda kuwaona watoto kwa niaba yao.
Watoto walijikuta kihisia wakiishi mbali na watu wazima. Walimu walijali taaluma. Walezi walijali usalama wao kimwili. Wazazi nao walijali kusikia wanaendelea vizuri. Watoto hawa walioishi katika mazingira ya kutengwa kihisia waliamua kutengeneza uhusiano wa kubahatisha na watoto wa umri wao. 

Haikuwa ajabu, katika muktadha huu, kusikia watoto wengi wakijifunza tabia zinazowazidi umri. Hawakuwa na mtu mzima wa karibu kutathmini yale wanayojifunza wakiwa na wenzao ambao kimsingi wanafanana nao kiakili.
Ukilingalisha na watoto wanaoishi nyumbani, tofauti ni kubwa. Mtoto wa nyumbani anaweza asipate fursa ya kukaa na mzazi wake kwa ukaribu. Lakini angalau yeye anakutana naye mara kwa mara hata kama si kwa ukaribu anaouhitaji.

Inawezekana mzazi kwa sababu yoyote ile hapatikani vya kutosha nyumbani, lakini kuna namna mtoto anaweza kuwasiliana naye. Sambamba na hilo, mtoto anayeishi nyumbani anaweza pia kuonana na ndugu zake karibu kila siku. Ndugu hawa wa karibu wanakuwa na fursa ya kujua mwenendo wake na hata kuchukua hatua fulani mapema. Mtoto wa bweni hana fursa hii.

Itaendelea
 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,885FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles