*Mawaziri watatu, Mkuu wa Mkoa wachukua hatua, watoa maagizo
*Waliohusika wafukuzwa chuo wasakwa, walimu saba mbaroni , Mkuu wa Mkoa avuliwa madaraka
PENDO FUNDISHA NA ELIUD NGONDO, MBEYA
MWANAFUNZI wa kidato cha tatu, katika Shule ya Sekondari ya Kutwa Mbeya (Mbeya Day) ya jijini hapa, Sebastian Chinguku (17), amefanyiwa ukatili kwa kuchapwa fimbo na makofi na walimu wanne.
Tukio hilo la kusikitisha, lilitokea shuleni hapo Septemba 28 mwaka huu, katika ofisi ya walimu shuleni hapo na lilifahamika kuanzia jana kupitia mitandao mbalimbali ya kijamii.
Walimu waliohusika kumchapa mwanafunzi huyo, wamefahamika kuwa ni Franky Msigwa, Deo John na Evance Sanga kutoka Chuo Kikuu Kishiriki cha Dar es Salaam (DUCE) na Sanke Gwamaka kutoka Chuo Kikuu cha Mwalimu Nyerere, Dar es Salaam.
Taarifa zilizopatikana zinasema kwamba, wakati walimu wakimpiga mwanafunzi huyo, mwalimu mwenzao aliyetambulika kwa jina la Esther Harembo kutoka Chuo Kikuu cha Iringa, alikuwa akiwazuia wenzake hao wasimpige mwanafunzi huyo, huku akiwapiga picha na kuwarekodi kwa simu ya mkononi.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, walimu hao walikuwa mafunzoni kwa vitendo shuleni hapo kwa kipindi kadhaa.
Pia inasemekana, walimu hao walimpiga Sebastian baada ya kushindwa kufanya kazi ya somo la kiingereza iliyokuwa imetolewa na Mwalimu Msigwa Septemba 26, mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Katibu Tawala, Mkoa wa Mbeya (RAS), Mariam Mtunguja, alisema kabla mwanafunzi huyo hajapigwa na walimu wake, Mwalimu Msigwa alimpiga kofi baada ya kushindwa kuelewana.
“Siku ya tukio, inasemekana Mwalimu Msigwa alifika darasani na kutaka kujua wanafunzi ambao hawakufanya kazi aliyokuwa ametoa.
“Wanafunzi walijitokeza akiwamo Sebastian ambaye alijitetea kwamba hakuwapo shuleni wakati kazi hiyo inatolewa, hivyo akaomba asamehewe.
“Inavyoonekana, Mwalimu Msigwa hakumwelewa mwanafunzi wake, hivyo akampa adhabu ambayo aliikataa kisha akamwambia apige ‘pushapu’ na baadaye akampiga kofi.
“Mwanafunzi alipopigwa alihoji ni kwanini amepigwa wakati hakuwa na kosa, jambo ambalo lilimuudhi mwalimu huyo na kuamua kuwaita walimu wenzake ili wamsaidie kumwadhibu.
“Wale walimu walioitwa, walikuja na wakamchukua Sebastian hadi ofisini ambako walianza kumpiga fimbo bila utaratibu kama inavyoonekana katika picha za mitandao ya kijamii.
“Lakini, kwa sasa walimu hao wameshaondoka shuleni hapo na kurudi katika vituo vyao vya masomo baada ya muda wao kumalizika mwishoni mwa mwezi uliopita,” alisema Mtunguja huku akishangaa ni kwanini mkuu wa shule hiyo hakutoa taarifa katika vyombo vinavyohusika.
Wakati Mtunguja akieleza hayo, kiongozi wa darasa analosoma Sebastian, Venance Kibanda, alisema yeye na wanafunzi wenzake walisikitishwa na adhabu aliyopewa mwenzao kwa sababu ilikuwa kubwa ikilinganishwa na kosa alilodaiwa kufanya.
“Mwenzetu alimwomba mwalimu ampe nafasi ya kufuata kibali alichopewa na mwalimu wa darasa kuonyesha kwamba siku iliyotolewa kazi, hakuwapo shuleni.
“Wakati anataka kutoka nje, Mwalimu Msigwa alimzuia mlangoni na kuwaita walimu wenzake watatu ambao walifika na kuanza kumwadhibu huku wakimpeleka katika ofisi ya walimu ambako walimpiga kwa fimbo, ngumi na mateke bila huruma.
“Baada ya kumpiga hivyo, walimrudisha darasani kutuonyesha jinsi walivyomwadhibu mwenzetu,” alisema Kibanda.
Mkuu wa Shule hiyo, Magreth Haule, alipotakiwa kuzungumzia tukio hilo, alisema siku ya tukio hakuwapo shuleni na kwamba majukumu yote alimkabidhi makamu wake, Adonath Nombo.
Naye Nombo alipozungumzia suala hilo, alisema wakati walimu wanampiga mwanafunzi huyo, alikuwa kwenye kikao cha wazazi pamoja na baadhi ya walimu.
“Wakati wa tukio nilikuwa kwenye kikao ila majukumu yote niliyaacha kwa walimu hao wa mazoezi,” alisema Mwalimu Nombo.
Baba mzazi wa mwanafunzi huyo, John Chinguku, alipohojiwa juu ya tukio hilo, alionyesha kukerwa na kusema anamwachia Mungu pamoja na Serikali.
“Mwanangu ambaye ni pacha, namfahamu tabia yake, lakini adhabu aliyopewa ni kubwa,” alisema Chinguku kwa kifupi.
Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Mbeya, Dhahiri Kidavashari, alisema wanawashikilia walimu saba wa shule hiyo akiwamo mkuu wa shule.
“Mkuu wa shule, baadhi ya walimu na wanafunzi, tunawashikilia kwa ajili ya mahojiano. Wale waliohusika kumpiga mwanafunzi, bado hatujawakamata, lakini tunawatafuta,” alisema Kamanda Kidavashari.
WAZIRI WA ELIMU
Naye Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako, ametangaza kuwafukuza chuo walimu hao waliompiga mwanafunzi huyo.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Waziri Profesa Ndalichako alisema kitendo kilichofanywa na walimu hao ni cha kikatili kisichoweza kuvumilika.
“Tumechukua uamuzi wa kuwafukuza mara moja kwa kuwa walimu hawa wanafunzi hawafai kuendelea na taaluma hii wakati hatua zaidi za kisheria zikiendelea kuchukuliwa dhidi yao.
“Lakini, natoa onyo kali kwa wanafunzi wanaokwenda kwenye mazoezi ya vitendo, wasiende kinyume na taaluma kwani wakifanya hivyo watakuwa wanapoteza sifa za kuwa walimu,” alisema Profesa Ndalichako.
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI
Wakati hayo yakiendelea, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba, amesema ameviagiza vyombo vya dola jijini Dar es Salaam, viwatafute walimu hao na kuwakamata.
“Nimeelekeza vyombo vya dola viwatafute chuoni na popote walipo. Taarifa zaidi za tukio hilo zinasema wakati mwanafunzi huyo anapigwa, Mwalimu Esther Harembo wa Chuo Kikuu cha Iringa, ndiye aliyekuwa akizuia mwanafunzi asipigwe na ndiye aliyekuwa akisema mwacheni mtamuumiza huku akichukua video,” alisema Nchemba.
WAZIRI SIMBACHAWENE
Nayo Mamlaka ya Nidhamu kwa Walimu, imeagizwa kumvua madaraka Mkuu wa Shule hiyo, kwa sababu ya kushindwa kutoa taarifa ya tukio hilo.
Kauli hiyo, imetolewa jana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi), George Simbachawene.
“Ninaagiza mamlaka husika za kinidhamu kumvua madaraka Mwalimu Magreth kutokana na kukaa kimya huku kukiwa na tukio la unyama dhidi ya mwanafunzi,”alisema Simbachawene.
Pamoja na hayo, alisema Serikali imeshachukua hatua kwa Kamati ya Ulinzi na Usalama, Mkoa wa Mbeya, kuendelea kufuatilia kwa karibu tukio hilo.