23 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

JPM amrudishia Bakhresa sukari yake

1NA HARRIETH MANDARI -DAR ES SALAAM

RAIS Dk. John Magufuli, amemwagiza Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Charles Mwijage kumrudishia mfanyabiashara maarufu nchini, Said Salim Bakhresa sukari yake iliyozuiwa bandarini kwa sababu biashara yake ina tija kwa taifa.

Mbali na hayo, Rais pia amelipa Shirika la Umeme (Tanesco) miezi miwili kufikisha huduma ya umeme katika kiwanda cha kusindika matunda na kuzalisha juisi cha Bakhresa Food Products Ltd kilichopo Mwandege wilayani Mkuranga, mkoani Pwani.

Rais alitoa maagizo hayo jana  wakati wa hafla ya uzinduzi wa kiwanda hicho ambapo alisema ameridhishwa na uwekezaji wa kampuni hiyo.

Sukari hiyo ya Bakhresa ilizuiwa katika Bandari ya Dar es Salaam pamoja na wafanyabiashara wengine miezi michache iliyopita wakati Rais Magufuli alipotangaza kusitisha vibali vya kuagiza sukari kutoka nje kwa madai ya kulinda viwanda vya ndani.

Agizo hilo lilisababisha uhaba mkubwa wa sukari ambapo ilipanda na kufikia wastani wa Sh 4,500 hadi 6,000 katika baadhi ya mikoa nchini.

“Tena ndugu  yangu, nitakupa eneo ulime miwa ili upate sukari ya viwandani na ya majumbani, tena nitakupa bure, wewe Bakhresa umenifurahisha sana kwa uwekezaji wako na sukari yako niliyoizuia bandarini leo namwagiza Waziri Mwijage itoke na upatiwe,”alisema  Rais Magufuli bila kufafanua kiasi gani cha sukari kilichozuiwa.

Aidha Rais alisema kutokana na uhaba wa sukari unaoikumba Tanzania kwa miaka mingi ni vyema kushirikiana na wawekekzaji ili kuondokana na tatizo hilo.

Katika tamko lake Rais aliagiza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuipatia kampuni hiyo ya Azam  eneo la ekari 10,000 kwa ajili ya kilimo cha miwa.

“Kupitia kilimo hicho Watanzania wengi watapata ajira na pia kiwanda kitatumia sukari ambayo ni salama kwa afya zetu na pia kuongeza upatikanaji wa sukari hapahapa nchini,” alisema.

Kuhusu Tanesco, Rais Magufuli alisema

suala hilo hawezi kulifumbia macho kwakuwa Tanzania ya viwanda inategemea zaidi upatikanaji wa umeme wa uhakika.

“Saa nyingine  inashangaza kweli, kiwanda kinaanza kujengwa, watu wapo, kinakamilika, watu wapo, kinaanza kufanya kazi watu wapo, kinaajiri watu wote hawa, wanafunga jenereta lao, tena makao makuu ya Wizara ya Nishati na Madini ipo kilomita chache  kutoka hapa,”alisema Rais Magufuli.

Rais pia alisema Serikali yake inaangalia namna ya kukutana na wataalamu kuangalia mfumo mzuri wa  kuwatoza kodi wawekezaji bila usumbufu.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Bakhresa, Aboubakari Salim alisema kuna urasimu mwingi katika upatikananji wa maeneo mapya ya kuanzisha viwanda.

“Tasisi za utozaji kodi zimekuwa nyingi ambapo utendaji wake ni ule ule hivyo zinatupa usumbufu katika utendaji wetu, tungeomba zipungue ili tufanye kazi kwa ufanisi zaidi,”alisema Salim.

Naye Meneja Mawasiliano wa Kampuni ya Azam, Hussein Ally, alisema kiwanda hicho kimeweza kutoa ajira 600 kwa Watanzania,  ambapo kati ya hizo wenye ajira za kudumu ni  380.

Kampuni ya Azam ina jumla ya viwanda 13 ambapo viwanda 11 vipo  Dar es Salaam na vingine viwili vipo Pwani.

Kwa upande wake Waziri wa Viwanda Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage alisema kuwa uwekezaji uliofanywa na makampuni ya Bakhresa unasaidia kuchochea kilimo cha matunda na kutoa fursa ya soko la uhakika kwa wakulima.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles