Na Patricia Kimelemeta, Dar es Salaam
VIBARUA wa Kampuni ya Tarmal iliyoko Mabibo, Dar es Salaam, wamezuia msafara wa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ili asikilize malalamiko yao.
Malalamiko hayo ni ya kutokuwa na mikataba ya kudumu kwa zaidi ya miaka 10 pamoja kutowekewa fedha zao kwenye mfuko wa Pensheni wa PPF.
Kampuni hiyo ni wakala wa Kampuni ya PSI inayohifadhi na kusambaza vifaa vya uzazi wa mpango.
Baada ya kusimamisha msafara huo, Mwenyekiti wa wafanyakazi hao, Amin Athuman alimweleza waziri mkuu kuwa mwajiri wao anashindwa kuwalipa stahiki zao wanapoacha au kusimamishwa kazi jambo ambalo limewatia woga na kushindwa kudai haki zao.
“Tunakuomba Waziri Mkuu utusaidie, tunanyanyasika sana kwenye kampuni hii lakini hatuna pa kukimbilia, ndiyo maana tulipoona msafara wako tuliamua kukusimamisha kuwasilisha malalamiko yetu.
“Licha ya kuwapo matatizo lukuki lakini pia mpaka sasa hakuna mkataba wa kudumu, jambo ambalo limetufanya tuwe vibarua kwa zaidi ya miaka 10 sasa,”alisema Athuman.
Majaliwa aliwaambia wafanyakazi hao kuwa hawezi kulifumbia macho suala hilo kwa sababu linachangia kuongezeka vitendo vya unyanyasaji kazini.
Alimwagiza Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge, Jenista Mhagama na Mikurugenzi wa PPF kufika kwenye ofisi hizo kusikiliza kero za wafanyakazi hao na kuchukua hatua stahiki.
Majaliwa alikumbana na kadhia hiyo ya wafanyakazi wakati akitoka kupokea vifaa tiba vyenye thamani ya Sh bilioni 10 ambavyo vilitolewa na Umoja wa kampuni zinazotengeneza vinywaji baridi.