NA ASIFIWE GEORGE, DAR ES SALAAM
JESHI la Polisi Mkoa wa Kinondoni linamshikilia kijana ambaye hakufahamika jina lake, ambaye ni maarufu kwa kuuza madawa ya kulevya.
Taarifa za uhakika zilizolifikia gazeti hili jana, zilieleza kuwa kijana huyo alikamatwa katika oparesheni maalumu inayoendelea Dar es Salaam, ya kuwasaka watu wanaojishughulisha na uuzaji na utumiaji wa mdawa ya kulevya.
Picha za kijana huyo pamoja na mali zake zilisambazwa katika mitandao mbalimbali ya jamii jana zikionyesha mali zake.
MTANZANIA lilimtafuta Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Simon Sirro ambaye alisema taarifa hizo hajazipata hivyo alimtaka mwandishi afuatilie kwa Kamanda wa Mkoa wa Kinondoni.
“Taarifa za tukio hilo bado sijazipata naomba umtafute kamanda wa eneo husika anaweza kukupa ufafanuzi au taarifa za tukio hilo,”alisema Sirro.
Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Christopher Fuime alimtaka mwandishi wa habari hizi kufanya utafiti wa jina la mtuhumiwa aweze kulifuatilia suala hilo.
“Ndugu mwandishi unanipa taarifa ambazo hata huna taarifa kamili hivyo mimi nashindwa kufuatilia tukio hilo, naomba ufanye utafiti wa jina la huyo mtuhumiwa unipatie niweze kujua ukweli wa jambo hilo,”alisema Kamanda Fuime.