23.4 C
Dar es Salaam
Friday, June 21, 2024

Contact us: [email protected]

VENUS WILLIAMS AIKOSA FAINALI US OPEN

NEW YORK, MAREKANI

BINGWA namba moja wa zamani wa mchezo wa tenisi duniani kwa upande wa wanawake, Venus Williams, ametupwa nje kwenye michuano ya wazi ya US dhidi ya mpinzani wake, Sloane Stephens.

Venus alipewa nafasi kubwa ya kufanya vizuri kwenye michuano hiyo baada ya mdogo wake, Serena Williams, kushindwa kushiriki kutokana na mambo ya uzazi, hivyo waliamini Venus angeweza kuiwakilisha vizuri familia hiyo.

Katika mchezo huo wa juzi, Venus alijikuta akichezea kichapo cha seti 6-1, 0-6 na 7-5, kwenye mchezo huo wa nusu fainali, wakati huo mpinzani wa Venus, Sloane akitokea majeruhi na kuweza kushinda mchezo huo.

Sloane anashika nafasi ya 83 kwa ubora duniani upande wa wanawake, huku Venus akishika nafasi ya tisa, lakini alishindwa kuonesha uwezo wake huku wadau wa mchezo huo wakidai umri wa Venus unaanza kumtupa mkono akiwa na miaka 37 sasa, wakati huo Sloane akiwa na miaka 24.

Sloane anatarajia kucheza fainali dhidi ya Mmarekani mwenzake, Madison Keys, mwenye umri wa miaka 22 akiwa anashika nafasi ya 16 kwa ubora duniani upande wa wanawake, fainali hiyo itapigwa kesho.

Fainali hiyo itakuwa ya kwanza kwa nyota wawili wa nchini Marekani kukutana huku mara ya mwisho ikiwa mwaka 2002 ambapo ndugu kutoka familia moja, Serena Williams na dada yake Venus walipokutana, lakini Venus aliipoteza fainali hiyo.

Safari hii kwenye michezo ya nusu fainali walikutana mastaa wote wanne kutoka nchini Marekani na ndio maana fainali wanakutana mabingwa kutoka nchi hiyo.

Sloane amedai kukutana fainali na nyota mwenzake kutoka nchini Marekani ina maana kubwa sana kwa Taifa hilo katika upande wa tenisi.

“Tuliweza kuingia wachezaji wanne hatua ya nusu fainali wote tukitokea hapa nchini Marekani, hii inamaanisha kwamba Marekani kwa sasa katika tenisi tunafanya vizuri.

“Kwa upande wangu ninajivunia kuwa katika nafasi hii, lengo langu kubwa ni kutwaa ubingwa, haikuwa kazi rahisi kuweza kushinda mbele ya bingwa namba moja wa zamani Venus, lakini ninashukuru nimeweza kushinda mbele ya mbabe huyo.

“Hakuna maneno mazuri ambayo ninaweza kuyasema yakaelezea hisia zangu jinsi zilivyo baada ya kufika fainali, ila nawashukuru mashabiki kwa sapoti yao,” alisema Sloane.

Venus mara ya mwisho kufika fainali katika michuano hiyo ilikuwa mwaka 2002, hivyo hadi sasa ni miaka 15 hajafanikiwa kufika fainali.

“Kila wakati nimekuwa nikipambana kuhakikisha ninatwaa taji, lakini hali imekuwa tofauti kutokana na ushindani ninaokutana nao, lakini ndivyo tenisi ilivyo,” alisema Venus.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles