KOCHA wa timu ya Manchester United, Louis Van Gaal, amesema ndoto zake ni kurudi kuifundisha klabu yake ya zamani ya Ajax.
Van Gaal aliwahi kuwa kocha msaidizi wa klabu ya Ajax mwaka 1988 hadi 1991, kabla ya kuwa kocha mkuu kuanzia 1991 hadi 1997, lakini kocha huyo anatarajia kuondoka baada ya kumalizika kwa msimu huu.
Kocha huyo ambaye amebakisha mwaka mmoja wa kuitumikia klabu hiyo, amedai akiondoka atatamani kujiunga na klabu ya vijana ya Ajax ‘Eredivisie’ kwa ajili ya kuisimamia kwa miaka 10 ijayo.
“Nina ndoto ya kurudi kuifundisha Ajax, ninaamini bado nina nafasi ya kuwa kiongozi wa klabu hiyo kwa kuwa ni kama timu yangu ya nyumbani.
“Najua siwezi kuendelea kuwa kocha wa Manchester United msimu ujao, hivyo lazima nitafute sehemu sahihi ya kuendelea kuwa kocha, lakini Ajax ni sehemu yangu sahihi,” alisema Van Gaal.
Klabu hiyo ya United ilipokea kichapo cha mabao 3-0 dhidi ya Tottenham katika michuano ya Ligi Kuu nchini England, lakini kocha huyo anaamini timu hiyo itamaliza katika nafasi nne za juu.