MSHAMBULIAJI wa timu ya Atletico Madrid, Fernando Torres, ameendelea kuikumbuka kadi nyekundu ambayo alioneshwa katika mchezo wa robo fainali ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya Barcelona na kudai kwamba bila kadi hiyo Atletico ingeshinda.
Katika mchezo huo ambao ulipigwa kwenye Uwanja wa Nou Camp, Atletico walikuwa wa kwanza kupata bao, lakini Barcelona walifanikiwa kupata bao la kusawazisha na kuongeza katika ushindi wa mabao 2-1.
Bao la pili la Atletico lilifungwa huku Atletico wakiwa pungufu baada ya mshambuliaji huyo kuoneshwa kadi nyekundu kutokana na utovu wa nidhamu na kuoneshwa kadi mbili za njano. Hata hivyo, Torres amedai kwamba wangeshinda mchezo huo kama wangeendelea kuwa 11.
“Bado ninaifikiria kadi ambayo nilioneshwa kwenye mchezo wa robo fainali kwenye Uwanja wa Nou Camp, ninaamini tulikuwa na kila sababu ya kushinda kama tungeendelea kuwa 11 uwanjani.
“Kadi ya kwanza ya njano ilikuwa sahihi, lakini ya pili haikuwa sahihi, ila ndicho kilichotokea na ninaamini mchezo wa kesho (leo) tunaweza kushinda nyumbani,” alisema Torres.
Timu hizo zinatarajia kushuka dimbani leo hii kwa ajili ya marudiano ambapo lazima mmoja ayaage mashindano baada ya mchezo huo kumalizika.