24.4 C
Dar es Salaam
Wednesday, June 19, 2024

Contact us: [email protected]

Uwekezaji yajivunia mafanikio miaka 60 ya Uhuru

Na Ramadhan Hassan, Dodoma

SERIKALI imesema imepata mafanikio makubwa katika kipindi cha miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania Bara, ikiwamo kuongezeka kwa uwekezaji.

Hayo yameelezwa leo Jumatano Novemba 3, 2021 jijini Dodoma na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Uwekezaji, Geoffrey Mwambe wakati akitoa taarifa ya mafanikio  ya kipindi cha miaka 60 ya uhuru wa Tanzania Bara mbele ya waandishi wa habari.

Mwambe  amesema  mafanikio hayo yametokana na kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji, utoaji wa mikopo kwa wajasiriamali, ujenzi wa miundombinu, utoaji elimu kwa wajasiriamali, utoaji wa huduma za kijamii  na ujenzi wa vituo vya uwezeshaji.

Mwambe amesema tangu Tanzania ipate uhuru, Serikali imechukua hatua ya makusudi ya kukuza uchumi wa Taifa na kuboresha hali ya maisha ya wananchi wake kwa kuhamasisha uwekezaji na ushiriki katika uchumi.

“Serikali inaendelea kuchukua hatua nyingine za kuandaa, kusimamia na kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji ikiwemo sheria, kanuni na maelekezo yote yanayohusu uwekezaji ili kuhakikisha kuwa vikwazo vyote katika uwekezaji vinatambulika na kuondolewa pamoja na kuwa na mazingira rafiki na sawa ya uwekezaji,” amesema.

Ameeleza kuwa Serikali itaendelea kujenga mazingira wezeshi ambayo yatasaidia wananchi na sekta binafsi kuchangia kikamilifu katika ujenzi wa Taifa pamoja na kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini, kuimarisha miundombinu ili kupunguza gharama za uzalishaji.

“Kutengwa kwa maeneo ya biashara, kuongeza ushiriki wa watanzania katika miradi ya kimkakati na miradi mikubwa ya uwekezaji, kuboresha utoaji wa mikopo kwa kupunguza riba na masharti mengine, kutoa elimu kwa wajasiriamali na kudhamini mikopo kwa wajasiriamali.

“Vipo viwanda vipya vilivyowahi kujengwa ambavyo havikuzalisha kabisa, au vilichelewa sana kuanza kuzalisha na hatimaye pia vikazalisha chini ya kiwango cha uwezo kilichowekezwa.

“Uamuzi wa kusambaza viwanda nchini ili kusawazisha maendeleo ulisababisha mara nyingine Viwanda kujengwa mahali ambapo hakuna maji, au umeme, au vyote viwili, bila kusahau hali duni ya miundombinu ya usafiri na usafirishaji,”ameeleza.

Amesema kutokana na jitihada za Serikali za kuweka mazingira wezeshi ya uwekezaji, uwekezaji wa ndani na kutoka nje umekuwa ukiongezeka mwaka hadi mwaka.

Amefafanua kuwa mafanikio hayo yanaweza kupimwa kwa vigezo vitatu vinavyotumika kupima kiwango cha uwekezaji kwa nchi ambavyo ni Uwiano wa Uwekezaji na Pato la Taifa, pamoja na Kiwango cha Uwekezaji Kutoka Nje na kiwango cha Ukuzaji Rasilimali kwa kila mwaka.

Amesema tangu Serikali ilipoanza kutekeleza Sera ya Taifa ya Uwekezaji na Sheria ya Uwekezaji Tanzania, wastani wa uwekezaji unaopimwa kwa kuangalia uwiano wa uwekezaji yaani Ukuzaji Rasilimali kwa Pato la Taifa umekuwa ukiongezeka.

“Takwimu zinaonesha uwiano wa ukuzaji rasilimali kwa Pato la Taifa umekua kutoka asilimia 14.7 mwaka 1997 hadi asilimia 39.7 mwaka 2019. Hivi ni viwango vikubwa ukilinganisha na wastani wa nchi za Afrika wa asilimia 21 – 22 na nchi zilizoendelea wa asilimia 23 hadi 25,”amesema.

Waziri Mwambe amesema uwekezaji wa mitaji kutoka nje umekuwa ukiongezeka kutoka dola za Marekani bilioni 0.73 mwaka 1996 hadi Dola za Marekani bilioni 2.18 mwaka 2013 na hadi Dola za Marekani bilioni 1.01 mwaka 2020.

“Serikali imefanikiwa kuanzisha Kituo cha Utoaji Huduma za Uwekezaji Mahali Pamoja kwa kuleta pamoja wizara na taasisi 12 ambazo ni Wizara ya Kazi (masuala ya vibali vya kazi), Wizara ya Ardhi (masuala ya Ardhi-Derivative Rights), Idara ya Uhamiaji (Masuala ya vibali vya ukaazi, TIC (Kuratibu na Kutoa Cheti cha Vivutio), BRELA (Usajiri wa Kampuni), NIDA, TBS, NEMC, OSHA, TRA, TMDA na TANESCO,”amesema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles